KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, May 24, 2012

Kumng'oa Nchunga kwa staili hii ni sawa na mchezo wa kitoto

Lloyd Nchunga

Katibu wa baraza la wazee la Yanga, Ibrahim Akilimali

Wanachama wa Yanga waliohudhuria mkutano uliotangaza kumng'oa Nchunga


BARAZA la wazee la klabu ya Yanga mwishoni mwa wiki iliyopita lilitangaza kumng’oa madarakani Mwenyekiti wa Klabu hiyo, Lloyd Nchunga kwa tuhuma za kushindwa kuiongoza vyema.
Mkutano huo, unaodaiwa kuhudhuriwa na wanachama zaidi ya 700, uliitishwa na Katibu wa baraza la wazee, Ibrahim Akilimali na kufanyika makao makuu ya klabu hiyo mitaa ya Twiga na Jangwani, Dar es Salaam.
Katika mkutano huo, wanachama hao, ambao inadaiwa kuwa wengine walitoka mikoa ya jirani, kwa kauli moja waliamua kuanzia sasa Yanga iendeshwe kwa mfumo wa kampuni, ikiwa ni kutekeleza sharti lililotolewa na mfadhili wa zamani wa klabu hiyo, Yusuph Manji.
Uamuzi mwingine uliofikiwa katika mkutano huo ni kuundwa kwa kamati maalumu, itakayokuwa ikisimamia masuala yote ya klabu hiyo pamoja na usajili wa wachezaji kwa ajili ya msimu ujao wa ligi.
Kilichofanywa na wanachama hao wa Yanga katika mkutano huo, hakina tofauti na kile walichokifanya Juni 7, 2010 wakati walipotangaza kumng’oa madarakani aliyekuwa mwenyekiti wa klabu hiyo, Imani Madega.
Tofauti pekee iliyopo ni kwamba uongozi wa Nchunga ulishaanza kuyumba kutokana na viongozi wengi waliochaguliwa katika uchaguzi wa mwaka juzi kujiuzulu kwa sababu mbalimbali.
Alianza makamu mwenyekiti, Davis Mosha akifuatiwa na wajumbe wa kamati ya utendaji, Seif Ahmed, Ally Mayay na Tito Osoro. Wajumbe wengine, Mohamed Bhinda, Mzee Yusuph na Paschal Kihanga nao walitangaza kujiuzulu wakati wa mkutano huo.
Mara baada ya mapinduzi ya mwaka juzi ya kumng’oa Madega, niliandika makala ndefu katika gazeti hili kuhusu mkutano uliofikia uamuzi huo kutokuwa halali kutokana na kukiuka katiba.
Karibu kila gazeti liliandika taarifa za mkutano huo kivyake wakati huo. Yapo yaliyoandika kuwa, uongozi wa Madega uliondolewa madarakani na mengine yaliripoti kuwa, umesimamishwa.
Vyombo vingine vilikwenda mbali zaidi kwa kuripoti kuwa, katika mkutano huo, wanachama walimteua Jaji Mkwawa, ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ya Yanga, kuchukua nafasi ya Madega hadi uchaguzi mkuu utakapofanyika.
Hali hiyo ilisababisha wananchi wengi washindwe kutambua ni kipi hasa kilichotokea kwenye mkutano huo. Walibaki kujiuliza je, ni kweli kwamba uongozi wa Madega uliondolewa madarakani? Kwa kigezo na taratibu zipi?
Wengine walishindwa kutambua lengo hasa la mkutano huo lilikuwa lipi? Je, ilikuwa ni marekebisho ya katiba na yalipitishwa? Na kama mkutano huo ulikuwa wa kujadili katiba, kwa nini wanachama walichukua uamuzi wa kumuondoa madarakani Madega?
Hivyo ndivyo ilivyofanyika. Baada ya Madega kuwauliza wanachama mara tatu, iwapo waliyakubali marekebisho hayo ya katiba yaliyotolewa na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na kumjibu ndio, aliamua kufunga mkutano na kutangaza kuwa, uchaguzi mkuu utafanyika Julai 4 mwaka 2010.Alifanya hivyo kwa sababu ajenda ya mkutano huo ilishamalizika.
Ujasiri wa Madega katika kusimamia katiba ya Yanga ndio uliomwezesha kuendelea kuwepo madarakani hadi uchaguzi mkuu ulipofanyika na kupatikana viongozi wapya, akiwemo Nchunga.
Katika hali ya kushangaza, tatizo hili limejirudia tena safari hii. Baraza la wazee la Yanga limeitisha mkutano wa wanachama na kutangaza kumng’oa madarakani Nchunga kwa kigezo cha kushindwa kuiongoza vyema klabu hiyo.
Kabla ya mkutano huo, wazee hao walishatoa tamko la kutaka kuchukua timu kwa madai kuwa, uongozi ulishindwa kuisimamia vyema na kusababisha wachezaji kudai mishahara ya miezi mitatu na posho za zaidi ya mechi 15.
Mbali na kutaka kuchukua timu, jaribio ambalo lilikwama, wazee hao pia walitoa tamko la kumtaka Nchunga ajiuzulu, vinginevyo wangetumia nguvu kumuondoa. Hata hivyo, Nchunga hakubabaika, bado aliendelea kusimama kwenye katiba.
Katika mazungumzo yake na waandishi wa habari, Nchunga alitangaza kuitisha mkutano mkuu Julai 15, mwaka huu, na kwamba mkutano huo ndio utakaotoa uamuzi wa mwisho iwapo abaki madarakani ama aondoke.
Nchunga alisema hawezi kuondoka madarakani kwa shinikizo la wazee kwa sababu hawatambuliki kikatiba. Alisisitiza kuwa, yeye alichaguliwa na wanachama na ndio wenye uamuzi wa mwisho juu yake.
Swali la kujiuliza ni je, mkutano uliotangaza kumng’oa Nchunga ulikuwa halali kikatiba? Na je, uamuzi uliotolewa katika mkutano huo unakubalika?
Kwa mujibu wa katiba ya Yanga ya mwaka 2008 ibara ya 22, inayohusu mkutano mkuu wa dharura, anayepaswa kuuitisha ni mwenyekiti kwa kushauriana na kamati yake ya utendaji.
Kipengele cha pili cha ibara hiyo kinasema kuwa, mkutano huo utaitishwa iwapo tu nusu ya wanachama watawasilisha maombi kwa kamati ya utendaji kwa maandishi na kamati hiyo itawajibika kuuitisha katika kipindi kisichozidi siku 30 baada ya kuwasilishwa kwa ombi hilo.
Kipengele cha tatu cha ibara hiyo kinasema kuwa, taarifa ya mkutano huo inapaswa kutolewa siku 15 kabla ya kufanyika kwake na ajenda na nyaraka zingine zitapelekwa kwa wajumbe siku saba kabla ya mkutano.
Kipengele cha tano cha ibara hiyo kinaeleza kuwa, endapo mkutano mkuu wa dharura utaitishwa kwa juhudi za kamati ya utendaji, ndiyo itakayoandaa ajenda na kama utaitishwa kwa ombi la nusu ya wanachama, ajenda itakuwa masuala yaliyopendekezwa na wanachama.
Kwa maana hiyo, kilichofanywa na wazee wa Yanga ni sawa na mchezo wa kujifurahisha kwa sababu mkutano waliouitisha ni batili na uamuzi wake pia ni batili.
Kikatiba, wazee wa Yanga hawatambuliki hivyo hawana mamlaka ya kuitisha na kuongoza mkutano wa wanachama. Waliopaswa kufanya hivyo iwapo mwenyekiti atagoma ni wajumbe wa kamati ya utendaji.
Inawezekana wazee hao walifikia uamuzi huo kutokana na wajumbe wengi wa kamati ya utendaji kujiuzulu, lakini sababu hiyo haina msingi kwa kuwa taratibu nzima katika kuitisha mkutano huo hazikufuatwa.
Klabu ya Yanga kwa sasa inao wanachama zaidi ya 4000, hivyo nusu ya hao ndio waliopaswa kujiorodhesha majina yao na kuwasilisha maombi ya kutaka uitishwe mkutano wa dharura kwa mwenyekiti. Hilo halikufanyika.
Idadi ya wanachama waliohudhuria mkutano huo na uhalali wao nayo inatia shaka. Si rahisi kuamini iwapo watu wote waliohudhuria mkutano huo walikuwa wanachama halali wa Yanga na iwapo walifika 700. Inawezekana kabisa kuwa takwimu hiyo ilikuwa ya kughushi kwa lengo la kuufanya mkutano huo uonekane umehudhuriwa na wanachama wengi wakati si kweli.
Katiba ya Yanga hailitambui baraza la wazee. Baraza hilo lipo kwa lengo tu la kuwaenzi wazee hao na pia kuchota hekima na busara zao. Hivyo inapotokea baraza hilo linakuwa mstari wa mbele kukiuka katiba na kuongoza mapinduzi, ni hali ya kushangaza kidogo.
Inasikitisha zaidi kuona kuwa, waandishi wa habari nao wameingia kwenye mtego wa kuripoti matukio bila kuhoji uhalali wake. Wameshindwa kuainisha katika taarifa zao iwapo mkutano ulioitishwa na wazee wa Yanga ulikuwa halali au la. Wameripoti habari za upande mmoja.
Walichopaswa kufanya ni kutazama katiba ya Yanga inasema nini kuhusu kuitishwa kwa mkutano huo na je, ulikuwa halali au vipi? Wangefanya hivyo, wasomaji wao wangeweza kutambua mara moja kuwa, kilichofanywa na wanachama wale ni mchezo wa kitoto.
Lengo la makala hii si kumtetea Nchunga na viongozi wenzake. Lengo ni kuwakumbusha wanachama wa Yanga umuhimu wa kuheshimu na kufuata katiba ya klabu yao katika kupitisha maamuzi mbalimbali.
Kwa mujibu wa maelekezo ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), kiongozi wa wa chama ama klabu zilizo chini yake hawezi kuondolewa kwa njia ya mapinduzi. Kujaribu kuwawajibisha viongozi kwa njia hiyo ni kuvunja katiba na pia kuzusha mgogoro mkubwa zaidi, ambao unaweza kurudisha nyuma maendeleo ya klabu.
Kama alivyosema Katibu Mkuu wa TFF, Angetile Osiah, shirikisho lake haliwezi kufanya kazi na kamati ya utendaji yoyote ile ya mwanachama wake, ambayo haikuchaguliwa kikatiba hata kama itakuwa ya uongozi wa muda. Hii maana yake ni kwamba TFF haiungi mkono mapinduzi hayo na bado inautambua uongozi wa Nchunga.
Ni kweli kwamba uongozi wa Nchunga unaonekana kuyumba na kupoteza mwelekeo na imani kwa wanachama na mashabiki wa klabu hiyo, hasa baada ya timu kufanya vibaya katika ligi na tuhuma za wachezaji kutolipwa mishahara na posho zao kwa wakati.
Lingekuwa jambo la busara kwa Nchunga kukubaliana na ukweli huo na kujiweka kando ili kupisha viongozi wengine. Lakini si busara hata kidogo kwa wazee wa Yanga kuitisha na kuongoza mkutano wa kumpindua Nchunga wakati hawatambuliki kikatiba na hawakufuata taratibu. Huku ni kuleta vurugu zaidi ndani ya Yanga.
Mwenyekiti wa zamani wa Yanga, Tarimba Abbas alinukuliwa na gazeti hili wiki iliyopita akisema kuwa, japokuwa hawatambuliki kikatiba, wazee ni watu muhimu katika klabu hiyo, lakini alionya kuwa, hawapaswi kutumiwa vibaya.
Alichokionya Tarimba ndicho kilichojitokeza kwenye mkutano huo. Ni wazi kuwa, wapo watu nyuma ya wazee hao, ambao ndio walioshawishi kufanyika kwa mkutano huo kwa lengo la kumng’oa Nchunga. Hilo ni kosa kubwa na ni ukiukaji wa katiba, ambao haupaswi kupewa nafasi. Ikumbukwe kuwa ni wanachama wenyewe wa Yanga walioamua kumchagua Nchunga, tena kwa mbwembwe nyingi wakati wa uchaguzi mkuu wa klabu hiyo uliofanyika kwenye ukumbi wa PTA, Sabasaba, Dar es Salaam.
Kulikuwepo na wagombea wengine wazuri na wenye uzoefu wa uongozi katika nafasi ya mwenyekiti kama vile Francis Kifukwe na Mbaraka Igangula, lakini kwa mshangao wa wengi, wanachama wakaamua kumchagua Nchunga, ambaye hakuwa na uzoefu wowote wa uongozi.
Hii maana yake ni kwamba, wanachama wa Yanga wamevuna walichopanda. Waliowashawishi kumchagua Nchunga wapo pembeni wamekaa kimya, kama vile hawaoni kinachotokea. Waswahili wanasema mtoto akililia wembe mpe, ukimkata ndipo atakapojua madhara yake.
Nina hakika iwapo Yanga ingekuwa chini ya Kifukwe ama Igangula, ingekuwa mbali hivi sasa na hata ile ndoto ya Manji ya kutaka klabu hiyo iendeshwe kwa mfumo wa kampuni, ingekuwa imeshatimia.
Kilichotokea katika mkutano huo kinapaswa kuwa funzo kubwa kwa wanachama wa Yanga kwamba wasikubali ‘kupelekeshwa’ na watu wachache wenye lengo la kuweka mbele zaidi maslahi yao binafsi badala ya klabu. Wanapaswa kukumbuka msemo wa Kiswahili unaosema, ‘Majuto mjukuu’.
Ni dhahiri kwamba wanachama wa Yanga waliingia kwenye mkutano huo wakiwa tayari wameshaandaliwa kutenda walichoagizwa na ‘watu’ wao. Hili ni jambo la hatari kwa mustakabali wa Yanga na endapo wanachama hawatakuwa makini, watakuja kujuta baadaye.
Busara inahitajika sana kwa pande zinazopingana ndani ya Yanga kutafakari kwa makini hatma ya klabu yao kwa sasa. Ni vyema pande hizo zikakaa pamoja na kukubaliana kipi kifanyike ili kuiokoa klabu hiyo isiingie kwenye mgogoro mkubwa zaidi na pia ili iweze kushughulikia masuala muhimu kama vile usajili wa wachezaji kwa ajili ya msimu ujao wa ligi.
Ni kweli Nchunga ana matatizo yake, lakini ukweli unabaki palepale kwamba, taratibu zilizotumika kumwondoa madarakani katika mkutano huo hazikuwa halali na hakuna kipengele chochote kwenye katiba ya klabu hiyo ya Yanga kinachozungumzia uwepo wa baraza la wazee na kama wana mamlaka ya kuitisha na kuendesha mkutano wa wanachama.
Julai 15 haipo mbali. Ndiyo siku, ambayo Nchunga amepanga kuitisha mkutano mkuu wa wanachama kwa lengo la kujadili masuala mbalimbali yanayoihusu klabu hiyo na kwamba atakuwa tayari kuondoka iwapo wanachama wataamua hivyo. Kwa nini wazee wa Yanga hawataki kusubiri siku hiyo? Kuna kitu gani kilichojificha nyuma ya wazee hawa? Kwa nini wanashinikiza Nchunga aondoke hivi sasa? Wanaharakia nini?
Hebu tujiulize, hivi kwa utaratibu huu wa kuondoa viongozi madarakani, ni mtu gani na heshima zake atakubali kugombea nafasi mojawapo ya uongozi ndani ya Yanga? Tusubiri, tuone.

No comments:

Post a Comment