'
Friday, May 18, 2012
Azam yakana kuhonga waamuzi
KLABU ya Azam imesema mafanikio yake katika michuano ya soka ya ligi kuu ya Tanzania Bara msimu huu, yametokana na kujiwekea malengo na si kuhonga waamuzi.
Azam imesema kiwango cha soka cha timu hiyo kwa sasa kipo juu na ndio sababu imekuwa ikitoa vipigo mara kwa mara kwa timu kongwe za Simba na Yanga.
Akihojiwa na kituo cha redio cha Uhuru FM wiki hii, Katibu Mkuu wa Azam, Idrisa Nassoro alisema madai ya kuhonga waamuzi hayana msingi na ni wivu wa watu wasioitakia mema timu hiyo.
Alisema kwa sasa, Simba na Yanga si chochote kwa Azam na ndio sababu walizifunga katika michuano ya Kombe la Mapinduzi na katika ligi kuu ya Tanzania Bara.
Nassoro alisema madai ya Azam kuhonga waamuzi, yalianza kujitokeza baada ya timu hiyo kushika nafasi za juu katika msimamo wa ligi kuu na yalitokana na hofu ya wapinzani wao.
“Mwaka huu pekee, Yanga tumeifunga mara nne mfululizo. Tuliifunga bao 1-0 katika mzunguko wa kwanza wa ligi, tukaifunga mabao 2-0 katika mechi ya hisani, tukaifunga mabao 3-0 kombe la Mapinduzi na kisha tukaifunga mabao 3-1 mechi ya marudiano ya ligi,”alisema.
Katibu Mkuu huyo wa Azam pia alieleza kushangazwa na uamuzi wa Kamati ya Nidhamu na Usuluhishi ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), kuamuru pambano kati yao na Mtibwa Sugar lirudiwe.
Alisema uamuzi huo ulilenga kuibeba Mtibwa kwa vile wachezaji wake waligoma penalti katika mechi ya awali na kutoka nje ya uwanja na kwa mujibu wa kanuni, timu hiyo ilipaswa kushushwa daraja.
“Kanuni zipo wazi, lakini yalijengwa mazingira ili Mtibwa isiteremke daraja, mwamuzi akasingiziwa kamaliza mpira kabla ya wakati, Azam hatukuwa tumefanya kosa lolote, lakini tumeadhibiwa,”alisema.
Nassoro alisema ndani ya Azam, hakuna siasa za Usimba na Uyanga na kusisitiza kuwa, ndoto za viongozi ni kuiona timu hiyo ikipata mafanikio makubwa zaidi kisoka.
Alisema watu wanaodhani kwamba Azam itakufa hivi karibuni, wanaota ndoto za mchana kwa vile lengo lao ni kujulikana zaidi kimataifa.
Kiongozi huyo wa Azam alisema, tangu walipoanza kushiriki michuano ya ligi kuu, wamekuwa na malengo ikiwa ni pamoja na kushika nafasi mbili za juu ili wapate nafasi ya kucheza mashindano ya kimataifa.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment