'
Friday, May 18, 2012
Moyo wa kumchangia Sajuki uendelezwe kwa wasanii wengine
HATIMAYE msanii nyota wa filamu nchini, Sadiki Juma Kilowoko ‘Sajuki’ ameondoka nchini kwenda India kwa ajili ya kupatiwa matibabu.
Sajuki aliondoka nchini Jumapili iliyopita saa nane mchana kwa ndege ya Shirika la Ndege la Emirates akiwa amefuata na mkewe, Wastara Juma ‘Stara’.
Msanii huyo amekwenda India kwa ajili ya kupatiwa matibabu ya kuondoa uvimbe tumboni, ambao umekuwa ukimsumbua kwa miezi kadhaa na kusababisha afya yake idhoofu.
Kuondoka kwa Sajuki kwenda India kumetokana na jitihada kubwa zilizofanywa na wasanii wenzake pamoja na wadau mbalimbali wa sanaa ya filamu, ambao walichangisha fedha kwa ajili ya matibabu yake.
Mbali na wadau hao, kituo cha redio cha Clouds FM kupitia mtangazaji wake, Dina Marios pamoja na kikundi cha Orijino Komedi kupitia msanii wake, Emmanuel Mgaya ‘Masanja’ waliandaa vipindi maalumu kwa ajili ya kuwahamasisha watu mbalimbali kumchangia msanii huyo.
Kadhalika, msanii nyota wa kike wa filamu nchini, Jacqueline Wolper alionyesha moyo wa aina yake baada ya kumchangia msanii huyo dola 10,000 za Marekani (sawa na sh. milioni 15) ili kufanikisha matibabu yake.
Rais wa Shirikishio la Wasanii Tanzania (TAFF), Simon Mwakifamba alisema juzi kuwa, jumla ya sh. milioni 30 zilipatikana kutokana na michango iliyotolewa na wadau mbalimbali.
Kwa mujibu wa Mwakifamba, malengo yalikuwa ni kukusanya sh. milioni 25 zilizokuwa zikihitajika kwa ajili ya kugharamia matibabu ya msanii huyo, hivyo wamevuka malengo.
Mwakifamba amewashukuru wadau mbalimbali waliojitokeza kumchangia msanii huyo na kuwaomba waendeleze moyo huo kwa wasanii wengine wenye matatizo.
Alisema Sajuki anatarajiwa kupatiwa matibabu katika hospitali moja iliyopo katika mji wa Mumbai nchini India. Hakuweza kukumbuka jina la hospitali hiyo.
Sajuki aliwahi kutibiwa kwa mara ya kwanza kwenye hospitali hiyo mwaka jana na kutakiwa arudi tena kwa matibabu zaidi, lakini tatizo kubwa lilikuwa gharama.
“Nimeguswa sana na tatizo lake, si kwamba nina fedha nyingi na sina shida, bali ni moyo wa kusaidia kuokoa uhai wa mwenzetu ili atibiwe na kurudi katika shughuli zake za filamu. Tulizoea kuwa naye location na kwenye tasnia ya filamu kwa ujumla, na sasa anaumwa na hajiwezi, nimeumia sana,”alisema Wolper alipokuwa akizungumzia uamuzi wake wa kumchangia msanii huyo.
Mmoja wa wabunge waliomchangia msanii huyo, Iddi Azzan alisema ameguswa na hali ya msanii huyo, ambaye afya yake ilikuwa ikizidi kuzorota kadri siku zilivyosonga mbele.
Azzan, ambaye ni mbunge wa Kinondoni (CCM) alitoa mchango wa sh. milioni moja baada ya kuhamasishwa kufanya hivyo na msanii Masanja wa Orijino Komedi.
Wabunge wengine waliojitokeza kumchangia msanii huyo ni Ester Bulaya (Viti Maalumu-CCM) na Halima Mdee (Kawe-Chadema), ambao kila mmoja alitoa sh. 500,000.
Wasanii wengine wa filamu na muziki, wameamua kutunga na kuimba wimbo maalumu kwa ajili ya kumchangia Sajuki. Fedha zote zitakazopatikana kutokana na mauzo ya wimbo huo, zitaingizwa kwenye akaunti ya msanii huyo.
Akichangia fedha hizo, Halima alisema wasanii wa filamu pamoja na kuwa na muonekano katika jamii, wapo nyuma katika masuala ya kijamii.
Halima alisema baya zaidi ni kwa wasanii hao kukosa umoja na ushirikiano katika masuala yao na kuongeza kuwa, ameligundua hilo kutokana na kuugua kwa Sajuki.
“Wasanii wa filamu wapo nyuma sana, kila mtu anajijali yeye tu, hana msaada kwa mwenzake. Leo hii Sajuki anaumwa na alikuwa akihitaji msaada wa kifedha ili akatibiwe nje ya nchi, lakini hakuna hata msanii mmoja aliyefanya juhudi zozote, hata kuchangisha fedha hizo. Tatizo lililomkuta Sajuki si tatizo la pekee yake, mtu yoyote linaweza kumkuta,”alisema Halima.
Mbunge huyo alimpongeza msanii wa kundi la Orijino Komedi, Masanja kwa kubuni na kuvunja vipindi vyao na kutumia muda huo kuchangisha fedha kwa ajili ya kumsafirisha Sajuki kwenda India.
Halima alisema yeye na wabunge wenzake, wataendelea kuibana serikali Bungeni kuhusu maslahi ya wasanii na aliahidi kulizungumzia suala hilo wakati wa hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo katika Bunge la mwezi wa sita.
Moyo ulioonyeshwa na Wolper na wadau wengine wa sanaa ya filamu nchini katika kumchangia Sajuki unastahili kupongezwa na uwe mfano wa kuigwa kwa wasanii wengine.
Wolper ameonyesha moyo wa aina yake kwani angeweza kutumia kiasi cha fedha alichotoa kwa matumizi mengine yoyote ikiwa ni pamoja na kustarehe, lakini ameguswa na hali ya Sajuki.
Ni vyema wasanii wengine nchini, hasa wenye uwezo kifedha waige mfano wa Wolper. Na hata wale wasiokuwa na uwezo mkubwa wanapaswa kukumbuka kuwa, kutoa ni moyo si utajiri.
Wasanii wanapaswa kukumbuka kuwa, leo limetokea kwa Sajuki, lakini kesho na keshokutwa linaweza kutokea kwa msanii mwingine yoyote.
Si vyema kwa wasanii kusubiri msanii mwenzao apoteze maisha ndipo wajitokeze kwa wingi kuchangia mazishi na gharama zingine pamoja na kuonyesha mbwembwe msibani, wakati fedha hizo zingeweza kuokoa maisha yake.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment