KOCHA Mkuu wa timu ya soka ya Zanzibar, Zanzibar Heroes, Hemed Suleiman 'Moroko' ametangaza kikosi cha wachezaji 18 kitakachoshiriki katika mashindano maalumu ya Kombe la Dunia kwa nchi zisizo wanachama wa Shirikisho la Soka la Dunia (FIFA), 'Viva World Cup'.
Mashindano hayo yamepangwa kuanza kutimua vumbi Juni 4 mwaka huu nchini Kurdistan, kaskazini mwa Iraq na yatazishirikisha timu za mataifa tisa.
Ofisa Habari wa Chama cha Soka cha Zanzibar (ZFA), Munir Zakaria aliwaambia waandishi wa habari mjini hapa juzi kuwa, kikosi hicho kimeshaanza kambi kwa ajili ya kujiandaa na mashindano hayo.
Aliwataja wachezaji walioitwa kwenye kikosi hicho, timu wanazotoka zikiwa kwenye mabano kuwa ni Ismail Khamis (Mafunzo), Awadh Juma (Mtibwa Sugar), Khamis Mcha (Azam FC), Juma Othman Mmanga (Jamhuri), Mohammed Abdulrahim (Mafunzo), Abdulhalim Humud na Abdughan Gulam (wote Azam FC).
Wengine ni Abbas Nassor (Miembeni United), Ali Badru (Al Canal, Misri), Amir Hamad (JKT Oljoro), Abdi Kassim 'Babi' (Azam FC), Suleiman Kassim (African Lyon), Nadir Haroub (Yanga SC), Ali Mohammed (Super Falcon), Yussuf Makame (Mafunzo), Salum Shebe (Al Mudheiby, Oman), Sabri Ramadhan (Omani Club) na Gharib Mussa (African Lyon).
Zakaria alisema wachezaji wanne wanaocheza ligi kuu Tanzania Bara hawakuitwa kutokana na kuwemo kwenye kikosi cha timu ya Taifa, Taifa Stars, kinachojiandaa kwa mechi ya kufuzu kucheza fainali za Kombe la Dunia za mwaka 2014 dhidi ya Ivory Coast.
Aliwataja nyota hao kuwa ni Nassor Masoud 'Cholo' (Simba SC), Aggrey Morris, Waziri Salum na Mwadini Ali wanaokipiga na Azam FC.
Kwa mujibu wa Zakaria, kikosi hicho cha Zanzibar Heroes kitakuwa kikifanya mazoezi kwenye uwanja wa Mao Dzedong na kitakuwa chini ya Moroko akisaidiwa na Hafidh Muhidin.
Wakati huo huo, Zakaria amesema Zanzibar Heroes inatarajiwa kucheza mechi moja ya kirafiki ya kujipima nguvu dhidi ya Malawi.
Ofisa huyo wa ZFA alisema mechi hiyo inatarajiwa kupigwa Mei 28 mwaka huu kuanzia saa 2.30 usiku kwenye Uwanja wa Amaan.
Alisema timu hiyo inatarajiwa kuwasili Zanzibar asubuhi ya siku hiyo kwa boti ikitokea Dar es Salaam, ambako itacheza mechi yake ya kwanza ya kirafiki keshokutwa dhidi ya Taifa Stars.
Zakaria alisema Zanzibar Heroes inatarajiwa kuondoka nchini Juni 2 mwaka huu kwenda Iraq kwa ajili ya kushiriki katika mashindano hayo.
Alisema timu hiyo itaagwa Juni Mosi mwaka huu kwa kukabidhiwa bendera ya taifa na itaondoka Zanzibar kwa ndege ya Precision Air kabla ya kuunganisha ndege ya Qatar Airways.
No comments:
Post a Comment