KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, May 24, 2012

Azam itakuwa kama TP Mazembe-Idrissa Nassoro

SWALI: Ukiwa mmoja wa viongozi wa Azam, mmejisikiaje baada ya timu kumaliza michuano ya ligi kuu msimu huu ikiwa nafasi ya pili na kupata nafasi ya kucheza michuano ya kimataifa?
JIBU: Huu ni msimu wetu wa nne kushiriki katika michuano ya ligi kuu. Tangu mwaka wetu wa kwanza kucheza ligi hiyo, tulijiwekea malengo na lengo letu kubwa msimu huo lilikuwa ni kubaki katika ligi kuu. Tulijiwekea lengo hilo kwa sababu huko nyuma ilikuwa ni kawaida kwa timu kupanda na kushuka katika ligi kuu kutokana na mazingira mabovu yaliyokuwepo wakati huo. Tulimaliza ligi tukiwa nafasi ya tano.
SWALI: Baada ya hapo mikakati yenu mingine iliyofuata ilikuwa ipi?
JIBU: Katika mwaka wetu wa pili, tukiwa chini ya Kocha Itamar Amorin, tulijiwekea malengo tumalize ligi tukiwa katika nafasi nne za kwanza. Na kama unavyojua, Azam ni timu inayodhaminiwa na kampuni zilizo chini ya Azam na malengo ya hizi kampuni ni kufanya biashara.
Hivyo kwa Tanzania naweza kusema tumejijenga vizuri na tumejitanua hadi katika nchi jirani za Rwanda, Uganda, Malawi na Msumbiji, lengo likiwa ni kujitangaza zaidi kibiashara. Hivyo dhamira yetu nyingine ya dhati tuliyonayo ni kuinua soka ya Tanzania.
Katika msimu wetu wa tatu tulijiwekea malengo ya kushika nafasi tatu za kwanza, lakini hatukufanikiwa. Mwaka huu tukajiwekea lengo la kushika nafasi mbili za kwanza na tunashukuru Mungu kwamba tumefanikiwa.
SWALI: Kwa maana hiyo, unataka kusema kwamba lengo la kuanzishwa kwa Azam ni kutangaza bidhaa zinazozalishwa na kampuni hii?
JIBU: Wadhamini wetu wanatudhamini kwa nguvu zote. Sisi kama klabu ya mpira, malengo yetu ni kufika mbali zaidi. Kwa wale wanaodhani kwamba Azam ni nguvu ya soda, nadhani wamekosea. Malengo yetu ni kuendelea kuwepo kwa miaka mingi zaidi. Tunashukuru kwamba tumeshaanza kutoa mguu nje kwa kushiriki katika michuano ya kimataifa. Lengo letu ni kuandika historia mpya ya soka Tanzania.
Tunazipongeza sana Simba na Yanga kwa sababu zimeiwakilisha nchi yetu kwa miaka mingi katika michuano ya kimataifa na zimefanya mambo mengi mazuri, zimetwaa ubingwa wa kihistoria wa Afrika Mashariki kwa miaka mingi na pia michuano ya klabu za Afrika na haya si mafanikio ya kubeza. Kila mtu anatamani kufikia mafanikio hayo.
Sisi ndio kwanza tumeanza. Ni kama watoto, tumeanza kutia mguu. Matarajio yetu ni kufika mbali zaidi kule, ambako wenzetu hawa wameshindwa kufika.
SWALI: Hivi sasa mmeshapata nafasi ya kucheza mashindano ya kimataifa mwakani. Nini hasa malengo yenu katika mashindano hayo?
JIBU: Malengo yetu ni kufika mbali zaidi. Lakini waswahili wanasema mipango si matumizi. Unaweza kusema tumejiandaa kufanya vizuri, lakini hayo hayatawezekana bila ya kuwa na viongozi wazuri, makocha wazuri na wachezaji wazuri na mashabiki wa kuwahamasisha kwa sababu nao ni nguvu ya timu na wana mchango mkubwa.
Cha muhimu ni kuiboresha zaidi timu yetu. Tunaye kocha mzuri, ambaye kwa sasa yupo kwao Uingereza kwa mapumziko. Tunao vijana wazuri. Tutakachokifanya ni kumsikiliza mwalimu anasema nini. Tayari tunao vijana, ambao mwalimu aliwapendekeza na tumeshamalizana nao.
SWALI: Azam imeanza hivi karibuni, lakini imeweza kufanya mambo makubwa kama vile kujenga uwanja, hosteli na kuendeshwa kwa utaratibu wa kuvutia. Nini siri ya mafanikio haya?
JIBU: Ndoto kubwa ya viongozi wetu kuanzia mwenyekiti, mkurugenzi na viongozi wa bodi ni kuifanya Azam iwe kama TP Mazembe. Lakini kama ujuavyo, Rome ni mji mkubwa na mzuri, lakini haukujengwa kwa siku moja. TP Mazembe ni timu kubwa, lakini haikutengenezwa kwa siku moja.
Kama unavyojua, tuna miaka minne tu hadi sasa ndio tumepata nafasi ya kupeperusha bendera ya Tanzania kimataifa, lakini hatuna sababu ya kurudi hapa na kusema hatukuandaliwa vizuri ama kutimiziwa mahitaji yetu. Kama ni visingizio, basi vitakuwa nje ya sababu hizo. Dhamira tuliyonayo ni kufika mbali zaidi. Kama wengine wameweza, kwa nini sisi tushindwe.
SWALI: Vipi kuhusu usajili wenu wa wachezaji kwa ajili ya msimu ujao na michuano ya kimataifa?
JIBU: Kwa mujibu wa sheria za kimataifa, kila timu inaruhusiwa kusajili wachezaji watano wa kigeni na tukiwa katikati ya ligi, tulimuuza kipa wetu Obren Cirkovic, hivyo tulikuwa na nafasi moja na tumeshaijaza kwa kusajili mchezaji mwingine wa kigeni kutoka nje ya nchi na tupo mbioni kuongeza kipa mwingine. Mchezaji wa kigeni tuliyemsajili anaitwa George Otieno, alikuwa mchezaji bora katika ligi ya Kenya mwaka jana na aliwahi kucheza soka ya kulipwa Denmark.
SWALI: Vipi kuhusu Yaw Berko na Emmanuel Okwi, kuna taarifa kwamba Azam inataka kuwasajili kwa ajili ya msimu ujao?
JIBU: Napenda kuchukua nafasi hii nikiwa katibu mkuu wa Azam kusema kwamba, hatuna mpango wa kumsajili Yaw Berko wala Emmanuel Okwi.
SWALI: Unadhani wachezaji mlionao sasa wanatosha kushiriki vyema katika michuano ya kimataifa na kuiwezesha Azam kufanya vizuri?
JIBU: Kwa uzuri wa timu yetu na mipango tuliyonayo, tuna uhakika mkubwa wa kufanya vizuri kwa vile vijana wetu wengi ni damu changa na wana ari kubwa.
SWALI: Vipi kuhusu kocha John Stewart, mtaendelea kuwa naye msimu ujao?
JIBU: Napenda kuchukua fursa hii kumpongeza sana Stewart kwa kuisaidia Azam kufikia malengo yake. Kama unakumbuka vizuri, kwa kipindi cha miaka 12 iliyopita, hakuna timu nyingine iliyoweza kushika nafasi ya kwanza na ya pili katika ligi kuu zaidi ya Simba na Yanga. Tuna imani naye kubwa na ametujengea msingi mzuri katika timu yetu. Hatuoni kocha mwingine anayeweza kutufaa zaidi yake kwa sasa. Kazi aliyoifanya ni kubwa na tunampongeza kwa hilo kwa sababu ni kocha mzoefu. Sote ni mashahidi na tumeona jinsi alivyoibadili timu ya Zanzibar.
SWALI: Kuna madai kuwa mafanikio yenu katika ligi ya msimu huu yamekuja dakika za mwisho na yametokana na kuiga mchezo mchafu, ambao umekuwa ukifanywa na klabu za ligi kuu. Je, kuna ukweli wowote kuhusu madai haya?
JIBU: Nilitarajia swali hilo. Kusema kweli mazoea yana tabu. Binadamu akizoea jambo, anakuwa na tabu anapolikosa. Hata Mtibwa walipochukua ubingwa mwaka 2000, yalimkuta haya haya. Hata Kajumulo naye yalimkuta hayo hayo. Nadhani hata Moro United ilifanyiwa hivyo.
Azam tangu mwanzo hatukuwa na malalamiko yoyote na wadhamini wetu ni wale wale. Tulikuwa na kocha Santos, akaja Itamar na tulikuwa na wachezaji wengi wa kigeni kama vile akina Dani Wagaruka na wengineo. Hata msimu huu ulipoanza, hatukusikia malalamiko yoyote. Tulikuwa tunakebehiwa tu kwamba nafasi yenu ya tatu inawasubiri palepale.
Lakini tuliposhiriki mashindano ya Kombe la Mapinduzi kule Zanzibar, tulitwaa ubingwa baada ya kuzifunga Simba na Yanga. Tuliporudi na kombe hili, wakalikebehi kwamba ni kombe la mbuzi. Matatizo yakaanza baada ya kuongoza ligi. Wakasema mengi, lakini napenda kuwahakikishia mashabiki wetu kwamba Azam ni timu nzuri na ina uwezo wa kuzifunga Simba na Yanga wakati wowote.
Katika mechi yetu ya kwanza ya ligi dhidi ya Yanga, tuliwafunga 1-0.Tulipokutana kwenye mechi ya hisani, tuliwafunga 2-0, tulipocheza Kombe la Mapinduzi, tuliwafunga 3-0 na tuliporudiana kwenye ligi, tukawafunga 3-1. Sasa ina maana Azam tumewahonga Yanga katika mechi zote nne?
Mechi yetu dhidi ya Polisi Dodoma ilikuwa ya kufa na kupona kwa sababu ilikuwa tukiwafunga, tunashika nafasi ya pili na wao wakifungwa, wanateremka daraja. Katika mazingira haya, kila timu ilicheza kwa kupania kushinda. Na hivyo ndivyo ilivyokuwa.
Tangu tulipoanza kucheza na Polisi Dodoma, tumekutana nao katika mechi sita na tumewafunga zote. Sasa kulikuwa na ajabu gani Azam kuifunga Polisi katika mechi ile?
SWALI: Na vipi kuhusu mechi yenu na Mtibwa, ambayo iliamriwa irudiwe? Mlicheza mara ya kwanza, mkatoka sare, lakini mkapewa ushindi. Mliporudiana, mkafungwa. Vipi?
JIBU: Nisingependa kuzungumzia yaliyopo chini ya pazia, lakini mechi ile ilikuwa na taharuki na ni kweli kwamba Mtibwa waligomea mechi yetu ya awali na wachezaji kutoka nje ya uwanja na kanuni zipo wazi kuhusu jambo hilo, lakini kama unavyojua nchi yetu, unapoingia katika mambo mengine, ujue wazi kwamba unapambana na Simba na Yanga.
Mtibwa walitoka uwanjani, lakini mwamuzi akaambiwa alivunja mchezo. Sheria zipo wazi. Wanasema mwamuzi alitakuwa kusubiri kwa dakika 15, lakini kisheria, pale tu mchezaji wa mwisho anapotoka uwanjani, mwamuzi anaruhusiwa kuvunja mchezo pale pale.
Mwisho wa siku tukajikuta tukicheza mechi mbili ndani ya siku tatu, lakini tuliyakubali yote hayo. Waswahili wanasema funika kombe mwanaharamu apite ama asiyekubali kushindwa si mshindani. Tuliadhibiwa, tukaambiwa turudiane na Mtibwa kwenye uwanja mwingine, kisheria timu inahamishiwa uwanja mwingine kama kulitokea vurugu. Tumefungwa na Simba, wametwaa ubingwa, tunawapongeza kwa hilo.
SWALI: Vipi ndani ya Azam, hakuna zile siasa za Usimba na Uyanga?
JIBU: Ni kweli zipo siasa hizo katika timu za ligi. Kwa mfano, Toto African wana uhusiano wa karibu na Yanga kama ilivyo kwa Simba na Coastal Union. Lakini kwa Azam, hicho kitu hakipo kabisa ndio sababu umeona tuliifunga Yanga katika mechi zote nne msimu huu.
SWALI: Kuna mipango yoyote ya kuuboresha zaidi uwanja wa Chamazi ili uweze kutumika kwa mechi za kimataifa?
JIBU: Hicho kitu kipo na michoro ya uwanja huo ipo kwa sababu tunalo eneo lingine kubwa jirani na uwanja wetu wa sasa. Hivyo moja ya mikakati yetu ya baadaye ni kuwa na uwanja mwingine mkubwa wa kisasa, ambao tutakuwa tukiutumia kwa mechi za kimataifa.

No comments:

Post a Comment