'
Friday, May 18, 2012
SIMBA YAPATA MSIBA MZITO, MAFISANGO AFARIKI DUNIA
KIFO cha kiungo wa kimataifa wa Rwanda na klabu ya Simba, Patrick Mafisango kilichotokea usiku wa kuanzia jana mazingira yake yalikuwa ya kusikitisha, gazeti la Majira limeripoti leo.
Vilio vilitawala nyumbani kwa mchezaji huyo huku kila mmoja akiwa haamini kile kilichotokea, hasa kwa wachezaji wenzake, ambao baadhi yao walishindwa kujizuia kutokwa machozi.
Akizungumzia mazingira ya ajali hiyo, rafiki wa marehemu aliyejitambulisha kwa jina la Olya Ilemba, ambaye alishuhudia kifo hicho alisema, mauti yalimfika Mafisango wakati wakitoka kujirusha katika klabu ya Maisha, ambako bendi ya FM Academia ilikuwa ikitumbuiza.
"Baada ya muziki kumalizika, tuliondoka mimi, Mafisango na watu wengine watatu. Mafisango ndiye aliyekuwa akiendesha gari aina ya Toyota Cresta, lakini alikuwa akiendesha kwa mwendo wa kasi sana. Tulipomuuliza akasema, amechoka anahitaji kupumzika hivyo tumuache,"alisema Olya.
Aliongeza kuwa, walipofika maeneo ya Chuo ch Ufundi Chang'ombe (VETA) mwisho wa ukuta, walikutana na mwendesha guta, hivyo Mafisango akajaribu kumkwepa, lakini ikatokea pikipiki, ambayo ilikuwa katika mwendo wa kasi.
Olya alisema wakati Mafisango akijaribu kumkwepa mwendesha pikipiki, bahati mbaya gari lake liliacha njia na kuparamia mtaro pamoja na baadhi ya miti iliyokuwepo kwenye eneo hilo.
"Kwa kweli ile ajali ilikuwa mbaya sana kwani baada ya gari kusimama, tulimfuata Mafisango na kumkuta jicho lake la upande wa kushoto likiwa limechomoka huku akiwa ameumia vibaya kichwani. Tukajaribu kuuondoa mwili wake, ambao ulikuwa umegandamizwa na usukani,"alisema.
Olya alisema baada ya kumtoa, rafiki yao mwingine alikuwa amechanganyikiwa na baada ya kuhisi kuwa Mafisango amefariki, alimwambia ajikaze ili wampeleke hospitali.
Alisema bahati zuri teksi ilikuwa ikipita karibu yao, hivyo walimchukua na kumpeleka hadi Hospitali ya Taifa Muhimbili, ambako walithibitisha kifo chake.
"Inauma sana, Mafisango ni kipenzi chetu, ametuacha wakati ambapo tunamuhitaji sana, tena ilikuwa aondoke jana kwenda kwao Rwanda kujiunga na timu ya taifa, lakini safari yake imekuwa kifo,"alisema
Msiba wa Mafisango upo Chang'ombe Maduka Mawili kwenye nyumba aliyokuwa akiishi pamoja na wachezaji wenzake, Gervas Kago kutoka Jamhuri ya Afrika ya Kati na Derrick Walulya kutoka Uganda.
Taarifa zinasema kuwa, mwili wa Mafisango unatarajiwa kuagwa leo saa nne asubuhi kwenye uwanja wa klabu ya Sigara, Chang'ombe, Dar es Salaam. Marehemu ameacha mke na mtoto mmoja wa kiume, Chris Paul.
Akizungumzia kifo hicho, kiungo wa kimataifa wa Rwanda na klabu ya Yanga, Haruna Niyonzima alisema ajali hiyo ilitokea saa chache kabla ya wao kusafiri kwenda kujiunga na timu yao ya taifa.
Alisema wakati akijiandaa kwenda uwanja wa ndege wa Julius Nyerere, aligundua kwamba alisahau pasi yake ya kusafiria na wakati akirudi nyumbani, ndipo alipopokea simu ikimtaarifu kuhusu ajali na kifo cha mchezaji mwenzake.
"Sikuamini mpaka nilipokwenda Muhimbili,"alisema Niyonzima huku akitokwa na machozi ya uchungu.
Alisema siku chache zilizopita, Mafisango alimkumbusha aitunze jezi yake namba 30, ambayo alibadilishana naye siku Simba ilipocheza na Yanga na kuibuka na ushindi wa mabao 5-0. Alisema Mafisango alimtaka asigawe jezi hiyo kwa mtu yeyote bali iwe kumbukumbu yake.
"Kumbe jamaa ndio alikuwa anakufa, nitamkumbuka daima,"alisema.
Wachezaji wa timu ya Taifa, Taifa Stars waliokuwa mazoezini kwenye uwanja wa Karume baadhi yao walishindwa kuendelea na mazoezi na kubaki wakilia kwa simanzi.
Kipa Juma Kaseja na beki Amir Maftah ndio walioonekana wakilia kwa uchungu zaidi wakati Haruna Moshi baada ya mazoezi, aliamua kwenda moja kwa moja kwenye chumba cha maiti cha Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.
Mafisango ni mzaliwa wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo lakini alipewa uraia wa Rwanda na kuichezea timu ya taifa ya nchi hiyo katika michuano ya kimataifa. Aliingia nchini mwaka juzi na kujiunga na Azam kabla ya mwaka jana kuhamia Simba.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
This comment has been removed by a blog administrator.
ReplyDelete