'
Thursday, May 3, 2012
TIMU ZA MAJESHI ZAONGEZEKA LIGI KUU
MICHUANO ya soka ya fainali za ligi daraja la kwanza Tanzania Bara, ilimalizika hivi karibuni mjini Tanga kwa timu tatu za kwanza kupata tiketi ya kucheza ligi kuu msimu ujao.
Polisi Morogoro ilimaliza ligi hiyo ikiwa ya kwanza baada ya kupata pointi 20, ikifuatiwa na Mgambo Shooting ya Tanga iliyopata pointi 15 na Prisons ya Mbeya iliyopata pointi 14.
Timu zingine zilizoshiriki katika ligi hiyo, pointi zao kwenye mabano ni Polisi Dar es Salaam (13), Mbeya City Council (11), Rhino Rangers ya Tabora (8), Mlale JKT ya Ruvuma (8), Polisi Tabora (6) na Transit Camp ya Dar es Salaam (2).
Timu hizo tatu zitachukuwa nafasi ya Polisi Dodoma na Moro United, ambazo tayari zimeshashuka daraja kutoka ligi kuu baada ya kushika nafasi mbili za mwisho. Timu ya tatu itajulikana baada ya mechi za mwisho za ligi hiyo, inayotarajiwa kumalizika keshokutwa.
Kwa mujibu wa msimamo wa ligi kuu, timu zilizopo hatarini kuungana na Moro United na Polisi Dodoma kushuka daraja ni Villa Squad, African Lyon na Toto African.
Villa Squad inashika nafasi ya tatu kutoka mkiani, ikiwa na pointi 23 baada ya kucheza mechi 24 wakati juu yake zipo African Lyon yenye pointi 24 na Toto African yenye pointi 26.
Katika mechi za mwisho, Toto African itacheza na Coastal Union mjini Tanga, African Lyon na JKT Ruvu, Villa Squad na Ruvu Shooting.
Kupanda daraja kwa timu za Polisi Moro, Mgambo Shooting na Prisons kumeongeza idadi ya timu zinazomilikiwa na majeshi ya ulinzi na usalama katika ligi hiyo.
Katika msimu huu wa ligi, idadi ya timu za majeshi zilikuwa nne, lakini baada ya kupanda kwa timu hizo tatu, idadi hiyo itaongezeka na kuwa sita.
Timu za majeshi, ambazo tayari zipo ligi kuu na zimeshajihakikishia kubaki kwenye ligi hiyo msimu ujao ni JKT Oljoro, JKT Ruvu na Ruvu Shooting, ambazo zinamilikiwa na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT).
Prisons, inayomilikiwa na Jeshi la Magereza, siyo timu ngeni katika ligi hiyo. Iliwahi kushiriki kwa kipindi kirefu miaka ya nyuma kabla ya kushuka daraja misimu mitatu iliyopita.
Timu hiyo imewahi kutoa nyota wengi waliowahi kuzichezea Simba na Yanga na hata kikosi cha timu ya taifa, Taifa Stars. Baadhi ya nyota hao ni kipa Ivo Mapunda, aliyewahi kuichezea Yanga na ambaye kwa sasa anacheza soka ya kulipwa katika klabu ya Gor Mahia ya Kenya.
Nyota wengine waliotokea Prisons ni Primus Kasonzo, Shadrack Nsajigwa, Stephano Mwasika, Yona Ndabila na Henry Morris, ambao wamewahi kutamba kwa nyakati tofauti katika timu hizo kongwe.
Nsajigwa na Mwasika bado wamo kwenye kikosi cha Yanga. Lakini kuna habari kuwa, Nsajigwa huenda akastaafu kucheza soka baada ya msimu huu kumalizika.
Polisi Moro imewahi kucheza ligi kuu kwa miaka kadhaa kabla ya kuvurunda misimu miwili iliyopita na kushuka daraja. Timu hiyo yenye maskani yake mjini Morogoro imerejea tena kwenye ligi kuu, ikichukua nafasi ya maafande wenzao wa Polisi Dodoma.
Kwa mujibu wa taratibu za jeshi hilo, upo uwezekano mkubwa kwa wachezaji walikuwemo kwenye kikosi cha Polisi Dodoma kuhamishiwa Polisi Moro kwa ajili ya kuiongezea nguvu.
Mgambo Shooting ni timu nyingine inayomilikiwa na Jeshi la Kujenga Taifa na ni mara yake ya kwanza kufuzu kucheza ligi kuu. Uwepo wake kwenye ligi hiyo kumeongeza idadi ya timu za jeshi hilo kwenye ligi kuu kuwa nne msimu ujao.
Timu pekee za uraiani, ambazo zitaendelea kuwepo kwenye ligi hiyo msimu ujao ni Simba, Yanga, Coastal Union na Toto African wakati majaliwa ya Villa Squad na African Lyon bado hayajajulikana. Timu
zinazomilikiwa na kampuni ni Azam, Mtibwa Sugar na Kagera Sugar.
Hata katika mechi za fainali ya ligi daraja la kwanza, idadi kubwa ya timu zilizoshiriki na kubaki kwenye ligi hiyo zilikuwa za majeshi. Timu hizo ni Polisi Dar es Salaam, Rhino Rangers ya Tabora na Transit Camp ya Dar es Salaam, zinazomilikiwa na Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ), JKT Mlale ya Ruvuma na Polisi Tabora.
Iwapo vyama vya soka vya mikoa havitafanya jitihada za makusudi za kufufua timu za mitaani kama vile Milambo, Majimaji, AFC, Lipuli, Katavi Rangers, African Sports upo uwezekano mkubwa katika miaka michache ijayo, ligi hiyo kutawaliwa zaidi na timu za majeshi.
Hata hivyo, ukweli ni kwamba uwepo wa timu nyingi za majeshi katika ligi kuu umetokana na huduma nzuri zinazopata muda wote wa mashindano. Pia timu hizo za majeshi zimekuwa zikitoa ajira kwa vijana wengi wenye vipaji vya kucheza soka na hivyo kuachana na maisha ya mitaani.
Timu zilizokuwa zikitamba miaka ya nyuma, zilizokuwa zikimilikiwa na bodi za mazao, mashirika na kampuni kama vile Pamba, RTC, Ushirika, CDA, Reli, Waziri Mkuu, Pilsner, Ndovu sasa hazipo tena na uwezekano wa kuzifufua haupo.
Ni vyema viongozi wa vyama vya soka vya mikoa wafanye jitihada za kuzifufua baadhi ya timu hizo ili kuongeza ushindani zaidi wa kisoka kwa timu za mikoa. Hii pia itasaidia kuibua vipaji vingi vya vijana na kuwaendeleza kisoka ili hatimaye waje kuwa hazina kubwa ya taifa katika miaka ijayo.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment