KIPA Juma Kaseja akipata maelekezo kutoka kwa Kocha Kim Poulsen wakati wa mechi hiyo.
TIMU ya soka ya Taifa, Taifa Stars mwishoni mwa wiki iliyopita ilitoka suluhu na Malawi katika mechi ya kirafiki ya kimataifa iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Mechi hiyo ilikuwa ya kuipima nguvu Taifa Stars kabla ya kuvaana na Ivory Coast katika mechi ya michuano ya kuwania kufuzu kucheza fainali za Kombe la Dunia za 2014 itakayopigwa Juni 2 mwaka huu mjini Abidjan.
Licha ya kucheza nyumbani, Taifa Stars ilishindwa kuwapa burudani mashabiki wake kutokana na kuonyesha kiwango cha chini, tofauti na wapinzani wao, ambao walitawala sehemu kubwa ya mchezo huo.
Hali hiyo ilisababisha baadhi ya mashabiki waliokosa uvumilivu, kuwazomea wachezaji wa Taifa Stars kila walipofanya makosa uwanjani na kuishangilia Malawi.
Uchezaji huo mbovu pia ulionekana kumchukiza kocha mkuu wa timu hiyo, Kim Poulsen ambapo kuna wakati aliinuka kwenye benchi na kuwafokea wachezaji wake kwa kuwanyoonyesha mikono akiwataka wapeleke mpira mbele.
Kilichompandisha hasira Kim ni kuona wachezaji wake kila mara wakirejesha mipira nyuma hata pale walipotakiwa kusukuma mashambulizi mbele, uchezaji ambao pia uliwafanya mashabiki wazomee.
Katika mechi hiyo, Taifa Stars ililifikia lango la Malawi mara nne na kupata nafasi nzuri za kufunga mabao, lakini umaliziaji mbovu wa washambuliaji wake ulikuwa kikwazo.
Kwa mfano, kuna wakati Mwinyi Kazimoto alitoa chumba safi kwa Mbwana Samatta aliyeingia na mpira ndani ya 18 kisha akatoa pasi iliyomgonga beki mmoja wa Malawi na kugonga mwamba wa pembeni wa goli.
Samatta na Mrisho Ngassa ni washambuliaji pekee waliokuwa wakijaribu kulazimisha mashambulizi kwenye lango la Malawi, lakini walishindwa kupata ushirikiano mzuri kutoka kwa Haruna Moshi na Kazimoto.
Tatizo lingine kubwa lilijitokeza kwa baadhi ya wachezaji, ambao hawakuwa katika kiwango cha kawaida. Kwa mfano, haieleweki ni kwa nini kocha Kim alimpanga Kazimoto kucheza nafasi ya winga wa pembeni badala ya kiungo, ambayo ndiyo ameizoea.
Mchezaji mwingine aliyeonekana kucheza chini ya kiwango ni beki wa kushoto, Waziri Salum, ambaye alitolewa kipindi cha pili na nafasi yake kuchukuliwa na Amir Maftah.
Kiungo Shabani Nditi naye alifanya makosa mengi uwanjani ikiwa ni pamoja na kushindwa kuiunganisha vyema safu ya ulinzi na ushambuliaji na kutoa pasi butu ama kunyang’anywa mipira na wachezaji wa timu pinzani karibu na eneo la hatari.
Kiungo mwenzake, Frank Damayo naye hakuwa kwenye kiwango cha kawaida na haieleweki kwa nini kocha Kim alishindwa kumpumzisha katika kipindi cha pili kutokana na kutojiamini na pasi zake kupotea bure uwanjani.
Mabeki Kelvin Yondani, Aggrey Morris na Shomari Kapombe pamoja na kipa Juma Kaseja walionyesha uhodari mkubwa wa kuwazuia washambuliaji wa timu pinzani. Kama isingekuwa uhodari wa Kaseja, huenda Wamalawi wangepata hata mabao mawili.
Kilichowashangaza zaidi mashabiki waliohudhuria mechi hiyo ni kuona kocha Kim akishindwa kufanya mabadiliko mengine ya wachezaji katika kipindi cha pili.
Wakati Kocha Kina Phiri wa Malawi alifanya mabadiliko ya wachezaji watano, Kim alifanya mabadiliko ya mchezaji mmoja pekee. Hali hii ilisababisha maswali mengi kwa mashabiki iwapo kocha huyo hakuwa akijiamini.
Kwa maoni ya mashabiki wengi waliohudhuria mechi hiyo, Kim alipaswa kufanya mabadiliko ya wachezaji hata wanne ili kupima uwezo wao kwa sababu mechi hiyo ilikuwa ya kirafiki kwa lengo la kujipima nguvu.
Kitendo cha Kim kutofanya mabadiliko mengine zaidi kilitafsiriwa na baadhi ya mashabiki kuwa, kilionyesha woga wa kuhofia kufungwa nyumbani katika mechi yake ya kwanza. Huu ulikuwa udhaifu mkubwa kwa kocha huyo.
Baadhi ya mashabiki walisema ni bora kocha huyo angeingiza wachezaji wengine katika nafasi zilizopwaya ili aweze kupata kikosi cha kwanza kwa ajili ya kukabiliana na Ivory Coast.
Vinginevyo kama kocha huyo atakitegemea kikosi kilichocheza tangu mwanzo dhidi ya Malawi, Watanzania wasitarajie makubwa kutoka kwa Ivory Coast kwa sababu kilishindwa kucheza kitimu.
Pengine ni vyema kwa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kuitautia Taifa Stars mechi nyingine ya kirafiki ya kimataifa ili Kim aweze kupata nafasi ya kupima wachezaji wengine na hatimaye kuwa na kikosi cha kwanza. Kim alikiri baada ya mchezo huo kuwa, kikosi chake kilikosa umakini na aliahidi kukifanyia marekebisho kabla ya pambano lao dhidi ya Ivory Coast. Ni marekebishi gani hayo? Tusubiri tuone.
Kikosi kilichocheza mechi hiyo ni kifuatacho: Juma Kaseja, Shomari Kapombe, Wazir Salum/Amir Maftah, Aggrey Morris, Kelvin Yondan, Shaban Nditi, Mrisho Ngasa, Frank Domayo, Mbwana Samatta, Haruna Moshi ‘Boban’ na Mwinyi Kazimoto.
No comments:
Post a Comment