KAMATI ya Uchaguzi ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), imeamua nafasi za
uongozi wa Yanga zilizoachwa wazi baada ya kujiuzulu viongozi mbalimbali
wa klabu hiyo zijazwe Julai 15 mwaka huu.
Taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa Dar es Salaam jana na Mwenyekiti
wa kamati hiyo, Deogratius Lyato ilieleza kuwa kutokana na mazingira hayo
Kamati ya Uchaguzi ya Yanga ianze mchakato huo wa uchaguzi kuanzia Juni mosi mwaka huu
kulingana na Katiba ya Yanga ibara ya 28 inayozungumzia nafasi iliyo wazi.
Lyato alisema Kamati ya Uchaguzi ya TFF iliyokutana jana iliamua mchakato
huo uanze na uzingatie kikamilifu kanuni za uchaguzi za wanachama wa TFF
na kwamba nafasi zilizo wazi zitajazwa Julai 15 katika Mkutano wa uchaguzi
ambao mahali patapangwa na Kamati ya Uchaguzi ya Yanga kwa kushirikiana
na Sekretarieti ya klabu hiyo.
Alisema Mkutano wa Uchaguzi utakuwa na ajenda moja tu ya uchaguzi kujaza
nafasi zilizo wazi za Wajumbe wa Kamati ya Utendaji wa kuchaguliwa na
kwamba Kamati ya Uchaguzi ya Yanga iandae na isimamie shughuli za
uchaguzi kwa kushirikiana na Sekretarieti ya Yanga kwa mujibu wa kanuni za
uchaguzi za wanachama wa TFF chini ya usimamizi wa Kamati ya Uchaguzi ya
TFF na Katiba ya Yanga ibara ya 45(1) na (2).
Alisema hatua ya kuiagiza Yanga iitishe uchaguzi inatokana na kupata
ufafanuzi kutoka kwa Kamati ya Sheria, Maadili na Hadhi za Wachezaji ya TFF
iliyokutana juzi.
Kamati hiyo ya Sheria iliombwa kutoa mwongozo wa nini kifanyike ndani ya
Yanga baada ya wajumbe wake kadhaa kujiuzulu, hivyo Kamati ya Uchaguzi
ya Yanga ilikuwa imeomba mwongozo huo TFF.
Akitangaza muongozo huo kama walivyoombwa na Kamati ya Uchaguzi ya
Yanga mapema jana, Mwenyekiti wa Kamati ya Sheria, Maadili na Hadhi kwa
Wachezaji ya TFF, Alex Mgongolwa alisema kujiuzulu kwa wajumbe wengi wa
Kamati ya Utendaji wa klabu hiyo kunawaondolea nguvu ya kimaamuzi
wajumbe waliosalia kwa mujibu wa Katiba ya klabu hiyo na kwamba kwa sasa
shughuli za uongozi wa klabu zitafanywa na Sekretarieti ya klabu hiyo mpaka
Mkutano Mkuu utakapoitishwa kujaza nafasi hizo.
Alisema Wajumbe wa Kamati ya Utendaji ya Klabu hiyo ambao hawajatangaza
kujiuzulu ni pamoja na Salumu Rupia, Titto Ossoro, Sarah Ramadhani na
Mohamedi Bhinda hawana nguvu za kimaamuzi na hivyo hawawezi kuongoza
klabu hiyo mpaka mkutano mkuu utakapofanyika.
Mgongolwa alisema ili wajumbe hao wawe na nguvu ya kimaamuzi kwa
mujibu wa Katiba ya Yanga ni kwa idadi yao inapaswa kuwa asilimia 50 na
kwa sababu wajumbe waliojiuzulu ni wengi kuliko waliobakia, wanakosa
nguvu ya kimaamuzi.
Alisema hata wajumbe watatu walioteuliwa na Mwenyekiti wa Klabu hiyo kabla
hajajiuzulu ni batili kwa mujibu wa Katiba ya Yanga kwani uteuzi huo
unafanywa na Wajumbe wa Kamati ya Utendaji ambapo idadi yao tayari
ilikuwa haikidhi kufanya uteuzi huo kwani wajumbe waliojiuzulu walikuwa
wengi.
Wajumbe kadhaa wa Kamati ya Utendaji ya Yanga walitangaza kujiuzulu
kuongoza klabu hiyo hivi karibuni akiwemo Mwenyekiti Lloyd Nchunga
kutokana na sababu mbalimbali.
No comments:
Post a Comment