KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, May 24, 2012

NCHUNGA KIBOKO, ATEUA WAJUMBE WAPYA KAMATI YA UTENDAJI

WAKATI wazee wa klabu ya Yanga wakimshinikiza Mwenyekiti wao, Lloyd Nchunga ajiuzulu, kiongozi huyo amezidi kuwa king’ang’anizi baada ya kutangaza kuteua wajumbe wawili wapya wa kamati ya utendaji.
Akizungumza kwa njia ya simu mjini Dar es Salaam jana, Nchunga aliwataja wajumbe hao wapya kuwa ni Dk. Maneno Tamba na Thobias Lingarangara.
Nchunga alisema uteuzi huo ulianza rasmi juzi na kuongeza kuwa, wajumbe hao wanachukua nafasi ya Ally Mayay na marehemu Theonest Rutashoborwa.
Kuteuliwa kwa wajumbe hao kunaifanya kamati hiyo sasa iwe na wajumbe sita. Wengine ni Salum Rupia, Tito Osoro, Sarah Ramadhani na Mbaraka Igangula, ambaye hata hivyo kuna taarifa kuwa alitangaza kujiuzulu juzi.
Nchunga alisema ameamua kuwateua wajumbe hao kutokana na mamlaka aliyonayo kikatiba na kwamba lengo ni kuifanya kamati ya utendaji iwe hai zaidi.
Wajumbe wa kamati hiyo waliojiuzulu hadi sasa ni Seif Ahmed, Mohamed Bhinda, Mzee Yusuph na Pascal Kihanga. Mwingine ni makamu mwenyekiti wa zamani wa klabu hiyo, Davis Mosha. “Nimewateua wajumbe hao wawili kutokana na mamlaka niliyonayo kikatiba kupitia kifungu cha 29 ibara ya (3) ya katiba ya Yanga,”alisema.
Kwa mujibu wa Nchunga, kifungu hicho kinaeleza kuwa, uongozi wa Yanga unaweza kujaza nafasi za wajumbe wa kamati ya utendaji waliojiuzulu ama kufariki dunia.
Alipoulizwa kuhusu msimamo wake, kufuatia shinikizo la kumtaka ajiuzulu kutokana na tuhuma mbalimbali, Nchunga alisema bado yeye ni kiongozi halali wa Yanga.
Alikanusha taarifa zilizozaa mjini Dar es Salaam jana kwamba, amewasilisha barua ya kujiuzulu kwa wajumbe wa kamati ya utendaji na angetangaza rasmi uamuzi wake huo kwa waandishi wa habari kesho.
"Sina mawazo wala mpango huo. Hao wanaosema hivyo wana ajenda zao, mimi naendelea kuitumikia klabu yangu, nashirikiana vyema na viongozi wenzangu kuanza kazi ya kusajili wachezaji wapya kimya kimya,"alisema Nchunga.

No comments:

Post a Comment