KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Friday, May 11, 2012

Twiga Stars kuumana na Zimbabwe leo



TIMU ya soka ya Taifa ya wanawake, Twiga Stars leo itashuka dimbani kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kumenyana na timu ya taifa ya wanawake ya Zimbabwe.
Pambano hilo la kirafiki la kimataifa, limepangwa kuanza saa 10 jioni na litachezeshwa na mwamuzi Judith Gamba kutoka Arusha.
Zimbabwe iliwasili nchini juzi saa 1.30 usiku kwa ndege ya Shirika la Ndege la Afrika Kusini, ikiwa na msafara wa wachezaji 20 na viongozi wanane.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini Dar es Salaam, Kocha Mkuu wa Zimbabwe, Rosemary Mugadza alisema wamefurahia kupata nafasi ya kucheza na Twiga Stars kwa sababu ni moja ya timu nzuri barani Afrika.
Rosemary alisema mechi hiyo itakuwa kipimo tosha kwa Zimbabwe kabla ya pambano lao la michuano ya kuwania ubingwa wa Afrika dhidi ya Nigeria.
Alisema anaifahamu vyema Twiga Stars kwa sababu walicheza nayo mara mbili mwaka jana. Mara ya kwanza ilikuwa kwenye hatua ya nusu fainali ya mashindano ya Kombe la COSAFA, ambapo Zimbabwe ilishinda kwa penalti 4-2.
Zilikutana kwa mara ya pili katika michezo ya All Africa Games, iliyofanyika Maputo-Msumbiji, ambapo zilitoka sare ya mabao 2-2. Mabao ya Twiga Stars yalifungwa na Asha Rashid na Mwanahamisi Sharuwa.
Rosemary alisema sababu nyingine iliyowafanya watake kucheza na Twiga Stars ni kwa vile iliwahi kukutana na Nigeria katika mashindano ya fainali za Afrika mwaka 2010 nchini Afrika Kusini, ambapo Twiga Stars ilichapwa mabao 2-1.
Kwa mujibu wa Rosemary, mechi hiyo itakuwa ya pili ya kujipima nguvu kwa timu yake kabal ya kuivaa Nigeria. Mwishoni mwa wiki iliyopita, Zimbabwe ilivaana na Zambia mjini Harare na kuibuka na ushindi wa mabao 2-1.
Twiga Stars ipo kwenye maandalizi ya mechi yake ya raundi ya pili ya mashindano ya Afrika dhidi ya Ethiopia. Katika mechi ya raundi ya kwanza, Twiga Stars iliitoa Eritrea.
Viingilio katika mechi hiyo ni sh. 1,000 kwa maeneo yote ya uwanja isipokuwa VIP A, ambacho ni sh. 10,000 na VIP B kiingilio chake ni sh. 5,000.

No comments:

Post a Comment