MWENYEKITI wa zamani wa Baraza la Michezo Nchini (BMT) na kilichokuwa Chama cha Soka nchini (FAT), Luteni Kanali mstaafu, Iddi Kipingu ni miongoni mwa wanachama wanaopigiwa debe Yanga kuwania nafasi ya mwenyekiti.
Kipingu amekuwa akipigiwa debe na wanachama wengi wa Yanga kuwania wadhifa huo kutokana na uzoefu mkubwa alionao katika uongozi wa michezo.
Mbali na uzoefu, sifa nyingine inayowafanya wanachama wa Yanga wampigie debe Kipingu kuwania wadhifa huo ni uadilifu na msimamo wake katika uongozi.
Baadhi ya wanachama wa Yanga waliozungumza na Burudani wiki hii mjini Dar es Salaam walisema, Kipingu ndiye mwanachama pekee mwenye uwezo wa kuitoa klabu hiyo ilipo sasa na kuifikisha mbali.
Wanachama wengine, ambao wamekuwa wakipigiwa debe kuwania wadhifa huo ni pamoja na mwenyekiti wa zamani wa klabu hiyo, Francis Kifukwe na makamu wenyeviti wa zamani, Mbaraka Igangula na Davis Mosha.
Akizungumza na Burudani kwa njia ya simu jana, Kipingu alithibitisha kupokea maombi hayo kutoka kwa wanachama wengi wa Yanga, lakini alisema bado anatafakari.
Fomu za kuwania nafasi mbalimbali za uongozi Yanga zinatarajiwa kuanza kutolewa keshokutwa wakati uchaguzi mkuu wa klabu hiyo umepangwa kufanyika Julai 15 mwaka huu.
Kipingu alisema kwa sasa hawezi kuamua iwapo atagombea nafasi hiyo kutokana na sababu mbalimbali. Alizitaja baadhi ya sababu hizo kuwa ni pamoja na kutojua vyema tatizo linaloikabili Yanga kwa sasa.
"Naweza kusema nipo tayari kugombea nafasi hiyo, lakini kwanza nataka kiitishwe kikao cha wadau wa Yanga ili tujadiliane kwanza tatizo ni nini kabla ya mimi kuchukua fomu,"alisema Kipingu.
Alisema anapenda kuiona Yanga ikirejea katika hali nzuri na kumalizika kwa tofauti zote zilizojitokeza hivi karibuni miongoni mwa wanachama.
"Unajua uongozi ni ushirikiano. Napenda kuona tunakubaliana kwanza ndipo nichukue fomu. Nataka wawepo watu wote muhimu, wakiwemo wale wazee 20, wafadhili na viongozi wa zamani ili tuweze kuwekana sawa na tuwe na lengo moja, nami nitaingia,"alisema Kipingu.
Kwa sasa, Yanga haina uongozi wa kuchaguliwa baada ya aliyekuwa mwenyekiti, Lloyd Nchunga kuamua kujiuzulu, kutokana na shinikizo kubwa la wanachama na wazee wa klabu hiyo.
Kufuatia kujiuzulu kwa Nchunga, klabu hiyo kwa sasa ipo chini ya sekretarieti ya Yanga, inayoongozwa na Katibu Mkuu, Celestine Mwesigwa.
No comments:
Post a Comment