'
Saturday, May 12, 2012
STARA: Moyo wangu unavuja damu
MCHEZA filamu nyota wa bongo movie, Wastara Juma amesema kwa sasa yupo kwenye wakati mgumu kutokana na kuuguliwa na mumewe, Sajuki.
Wastara, maarufu zaidi kwa jina la Stara alisema mjini Dar es Salaam wiki hii kuwa, alikuwa akipata faraja kubwa kutoka kwa mumewe tangu alipopata ajali na kuvunjika mguu, lakini hali sasa imekuwa kinyume.
Sajuki, ambaye pia ni mmoja wa waigizaji nyota wa bongo movie, anasumbuliwa na maradhi ya tumbo na anahitajika kwenda kufanyiwa operesheni nchini India.
Stara alisema kwa sasa Sajuki ndiye anayetegemea faraja kubwa kutoka kwake. Stara na Sajuki wamefanikiwa kupata mtoto mmoja.
“Kinachonifanya nitabasamu ni kwa sababu namwamini Mungu, lakini moyo wangu unavuja damu, naumia sana,” alisema Stara.
“Jamii inaniona ni mtu wa kulialia tu, maisha yangu nimepitia mitihani mingi, umri wangu ni mdogo, lakini nimekomaa kama mtu mwenye umri wa miaka sitini,”aliongeza mwanadada huyo mwenye sura yenye mvuto.
“Nikiona matukio, nasikitika, lakini najua mengi na nimepitia mengi sana, maisha yangu yametawaliwa na mitihani,”alisema Stara akionekana dhahiri kuwa na masikitiko makubwa.
Stara alisema tangu alipoanza kumuuguza Sajuki mwaka jana, amelazimika kusimama kufanyakazi baada ya kubainika kwamba ana uja uzito wa mumewe.
Alisema madaktari walimshauri atumie muda mwingi kupumzika, lakini ilikuwa vigumu kwa sababu hakuwa na msaada wowote. Alisema aliamua kuendelea kufanyakazi ikiwa ni pamoja na kuomba misaada kwa ndugu wa karibu.
“Mara nyingi najifanya mjinga tu, lakini nimepitia mengi sana katika maisha haya, filamu ninazoigiza ni sehemu ya maisha yangu, mitihani niliyopitia, naumia sana, lakini bado namshukru Mungu kwa kila jambo,”alisema Stars.
“Mungu ana makusudi na mimi, siku hizi ni vigumu sana kumtegemea ndugu au jamaa, kila mtu ana mambo yake yanayomkabili, si rahisi kutoa msaada kwako,” aliongeza.
Kwa sasa, Stara anatafuta zaidi ya sh. milioni 25 kwa ajili ya matibabu ya Sajuki, ambaye anatumia dawa akiwa nyumbani, lakini anatakiwa kwenda India kwa ajili ya matibabu zaidi mwishoni mwa mwezi huu. Dawa anazotumia dozi kwa wiki ni dola 1,000.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment