'
Friday, May 18, 2012
Nchunga: Sijiuzulu ng'o
MWENYEKITI wa klabu ya Yanga, Lloyd Nchunga amesisitiza msimamo wake wa kutojiuzulu wadhifa huo kwa sababu ya shinikizo la baadhi ya wanachama.
Akizungumza na kituo cha Redio One jana asubuhi, Nchunga alisema hawezi kuondoka madarakani kwa shinikizo la wanachama kwa sababu alichaguliwa kikatiba.
Nchunga alisema kama kuna wanachama wasiomtaka, wanapaswa kufuata katiba katika kumuondoa badala ya kufanya vikao batili.
Alisema katiba za Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na ya Shirikisho la Soka la Dunia (FIFA) zinazuia viongozi wake kuondolewa madarakani kwa kutumia mbinu chafu.
Nchunga alisema kutokana na katiba za klabu zote za ligi kuu kufuata katiba za TFF na FIFA, kipengele hicho kinapaswa kuheshimiwa na wanachama wa Yanga.
Alisema atakuwa tayari kung’atuka madarakani iwapo tu wanachama watamtaka afanye hivyo katika mkutano mkuu aliouitisha Julai 17 mwaka huu.
Mwenyekiti huyo alisema anashangazwa na kauli za wazee wa klabu ya Yanga kutaka kutumia kikao alichokiitisha kati yao keshokutwa kumshinikiza ajiuzulu.
Alisema wazee wa Yanga hawamo kwenye katiba ya klabu hiyo, lakini wamekuwa wakipewa heshima kutokana na busara na ukongwe wao katika soka.
“Hata rais anapotaka kuzungumza na wananchi, amekuwa akiwatumia wazee wa Dar es Salaam, lakini hawamo kwenye katiba ya nchi,”alisema.
“Naomba nisieleweke vibaya ama kaulihii isichukuliwe kuwa ni tusi kwa wazee,” aliongeza.
Mwenyekiti huyo wa Yanga alionya kuwa, iwapo wanachama watakuwa wakitumia kigezo cha timu kufungwa na Simba kumuondoa kiongozi madarakani, hakuna kiongozi atakayeweza kumaliza muda wake.
“Ukitumia kigezo hicho kumwondoa kiongozi madarakani, nafasi hiyo inaweza kutumia vibaya. Watu watakuwa wanawatengenezea viongozi mazingira ya kutoka kila timu inapofungwa na Simba,”alisema.
Nchunga alisema japokuwa baadhi ya wazee wamesusia kikao cha keshokutwa, baadhi yao wamemwahidi kwamba watahudhuria na kutoa maoni yao kuhusu jinsi ya kutatua mgogoro huo.
Alitoa mwito kwa wadau wa Yanga kujitokeza kutatua mgogoro huo kwa lengo la kuweka mambo sawa.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment