SERIKALI imewataka wachezaji wa timu ya soka ya Taifa, Taifa Stars kutoogopa majina ya wachezaji wa Ivory Coast, badala yake wawaone ni watu wa kawaida.
Mwito huo umetolewa na Naibu Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Amos Makalla alipokuwa akizungumza na wachezaji wa timu hiyo wakati wa hafla ya kukabidhi bendera ya taifa.
Makalla alisema Ivory Coast inaundwa na wachezaji wa kawaida kama waliopo Taifa Stars na kama ni kuwazidi, wanaweza kufanya hivyo katika vitu vichache.
Alisema wachezaji wa Taifa Stars wanapaswa kuonyesha soka ya ushindani na kupata matokeo mazuri, yatakayowaweka katika nafasi nzuri ya kufuzu kucheza fainali za Kombe la Dunia za 2014.
Taifa Stars inatarajiwa kuondoka nchini leo alfajiri kwenda Abidjan kwa ajili ya pambano lao dhidi ya Ivory Coast lililopangwa kufanyika keshokutwa mjini humo.
Makalla alisema wachezaji wa Taifa Stars wanao uwezo wa kuhimili mikikimikiki ya wenzao wa Ivory Coast na kusisitiza kuwa, jambo la muhimu ni kuondoa hofu na kucheza kwa kujituma.
Alisema iwapo Taifa Stars haitapata matokeo mazuri katika mchezo huo, mashabiki wake watakasirika na kupunguza mapenzi yao kwa timu hiyo.
"Mnakwenda kucheza na timu, ambayo inaundwa na wachezaji wa kawaida kama nyinyi na mna uwezo wa kuwafunga, hivyo mkikutana nao onyesheni uwezo wenu na mbinu zenu, ambazo mmefundishwa na mwalimu wenu na mwisho mtafanikisha malengo yenu," alisema Makalla.
Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Leodegar Tenga alisema nidhamu na kujituma kwa wachezaji wa timu hiyo kutafanikisha ushindi na kuiweka Tanzania katika msimamo mzuri wa mashindano.
Tenga alisema anaamini wachezaji wa Taifa Stars watapambana vyema na kupata matokeo mazuri, ambayo ndiyo dhamira ya kila mtu na hapo ndipo mwanzo mzuri wa timu hiyo utakapoonekana baada ya kuanza kufundishwa na Kocha Kim Poulsen.
Kikosi cha Taifa Stars kilichoondoka leo alfajiri kinaundwa na makipa Juma Kaseja, Mwadini Ally na Deogratius Munishi. Mabeki ni Nassor Masoud Cholo, Aggrey Morris, Amir Maftah, Erasto Nyoni, Kelvin Yondani, Waziri Salum, Shomari Kapombe na Juma Nyoso. Viungo ni Mwinyi Kazimoto, Salum Abubakar,Jonas Mkude , Shabani Nditi, Edward Christopher, Mrisho Ngasa na Frank Domayo wakati washambuliaji ni Mbwana Samata, Ramadhan Singano, Simon Msuva, Haruna Moshi na John Bocco.
Viongozi wanaofuatana na timu hiyo ni Kocha Poulsen, Sylvester Marsh (kocha msaidizi), Juma Pondamali (kocha wa makipa), Leopold Mukebezi (meneja wa timu), Juma Mwankemwa (daktari wa timu), Frank Mhonda (Physiotherapist) na Alfred Chimela (mtunza vifaa). Msafara huo unaongozwa na mjumbe wa kamati ya utendaji ya TFF, Crescentius Magori wakati naibu kiongozi wa msafara ni Makamu wa Rais wa Chama cha Mpira wa Miguu Zanzibar (ZFA), Haji Ameir Haji.
No comments:
Post a Comment