Na Abood Mahmoud, Zanzibar
MABINGWA wa soka wa Tanzania Bara, Simba jana walianza vyema michuano
ya kuwania Kombe la Ujirani baada ya kuichapa Mafunzo mabao 2-1 katika
mechi iliyochezwa kwenye Uwanja wa Amaan, Zanzibar.
Wakati Simba iliibuka na ushindi huo mnono, Azam FC ilishindwa kufurukuta
mbele ya timu ya vijana ya Zanzibar, Karume Boys baada ya kulazimishwa
kutoka nayo sare ya bao 1-1.
Mshambuliaji mpya Abdalla Juma ndiye aliyeing'arisha Simba katika mechi
hiyo baada ya kuifungia mabao yote mawili. Alifunga bao la kwanza dakika ya
27 kabla ya kuongeza la pili dakika ya 44.
Mbali na Abdalla kung'ara, pia mshambuliaji mpya Kanu Mbiyavanga kutoka
Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo alikuwa kivutio kutokana na kutoa pasi
mbili zilizozaa mabao yote mawili.
Mafunzo ilipata bao la kujifariji dakika 10 kabla ya mchezo kumalizika kupitia
kwa mshambuliaji wake, Jaku Joma.
Tofauti na ilipocheza na Express, ambapo iliwatumia wachezaji wake wengi wa
kikosi cha pili, katika mechi ya jana, Simba iliwachezesha baadhi ya nyota
wake wa kikosi cha kwanza akiwemo Danny Mrwanda, Juma Kaseja, Shomari
Kapombe, Mwinyi Kazimoto na Amir Maftah.
Hata hivyo, Simba iliendelea kuwakosa Emmanuel Okwi, aliyekwenda Italia
kufanya majaribio ya kucheza soka ya kulipwa, Felix Sunzu na Haruna Moshi
'Boban'. Katika hatua nyingine, Azam ilinusurika kufungwa baada ya kupata bao la
kusawazisha dakika ya 79 kupitia kwa Kipre Tchetche.
Karume Boys ilikuwa ya kwanza kupata bao dakika ya 45 lililofungwa kwa njia
ya penalti na Ibrahim Hamisi.
Michuano hiyo inatarajiwa kuendelea leo wakati Yanga itakapomenyana na
Jamhuri ya Pemba kwenye Uwanja wa Amaan.
No comments:
Post a Comment