KAMATI ya Uchaguzi ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), imetupilia mbali rufani iliyowasilishwa na mwanachama Ishashabaki Luta wa klabu ya Yanga ya kupinga Yussuf Manji kugombea nafasi ya mwenyekiti katika uchaguzi mdogo wa klabu hiyo.
Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari jana jioni na mwenyekiti wa kamati hiyo, Deo Lyatoo ilisema kuwa, wameamua kuitupa rufani hiyo baada ya kubainika kuwa ilikuwa na kasoro kadhaa.
Alizitaja baadhi ya kasoro hizo kuwa ni pamoja na mrufani kutotimiza matakwa ya kanuni za uchaguzi ibara ya 11 (2), mrufani kutoweka wazi vielelezo vya rufani yake, anwani ya kudumu na saini yake.
Kasoro nyingine ni mrufani hiyo kushindwa kutokea wakati wa kikao cha kusikiliza rufani yake ili kutetea hoja zake. Kikao hicho kilifanyika kwa siku mbili juzi na jana kwenye ofisi za TFF zilizopo uwanja wa Karume, Dar es Salaam.
Mbali na kujadili rufani hizo, Lyatoo alisema kamati hiyo pia ilijadili mchakato mzima wa kuziba nafasi za uongozi zilizo wazi Yanga baada ya uongozi wa mwenyekiti Lloyd Nchunga na wajumbe wanne wa kamati ya utendaji kujiuzulu.
Kufuatia kutupwa kwa rufani hiyo, uongozi wa Yanga umetangaza rasmi kuanza kwa kampeni kwa ajili ya uchaguzi huo unaotarajiwa kufanyika Julai 15 mwaka huu.
Hiyo ilikuwa mara ya pili kwa Luta kumpinga Manji kugombea nafasi ya mwenyekiti katika uchaguzi huo. Mara ya kwanza alimwekea pingamizi kwa kamati ya uchaguzi ya Yanga, lakini zilitupwa baada ya kubainika kuwepo kwa dosari kadhaa.
Miongoni mwa dosari hizo ni jina la Luta pamoja na namba yake ya uanachama kutokuwemo kwenye leja ya wanachama wa Yanga na pia yeye mwenyewe kushindwa kufika kwenye kikao cha kujadili pingamizi zake.
Wakati kamati ya uchaguzi ya TFF ilipokuwa ikijadili rufani hiyo, wanachama kadhaa wa Yanga walikuwepo nje ya ofisi za shirikisho hilo wakifuatilia kwa makini maamuzi ya kamati.
Mara baada ya maamuzi kutolewa,wanachama hao walimzunguka Manji na kuanza kumshangilia na kumsindikiza hadi kwenye gari lake.
No comments:
Post a Comment