WAZIRI Mkuu mstaafu Frederick Sumaye ameeleza kusikitishwa kwake na kupoteza umaarufu wa soka la Tanzania kwa sasa ukilinganisha na miaka ya 1970.
Sumaye alisema hayo juzi katika hoteli ya Double Tree By Hilton ya jijini Dar es Salaam katika hafla ya kuwatunuku washindi mbalimbali waliofanya vema kwenye ligi kuu ya Vodacom msimu wa 2011/2012.
Alisema hali hiyo inatokana na timu vilabu nguli vya Simba na Yanga kubweteka kwa moja kuifunga nyenzake na kujiona zimefika peponi kitu ambacho si dalili nzuri katika maendeleo ya soka.
“Simba kuifunga Yanga au Yanga kuifunga Simba si kigezo kizuri cha kujiona ni timu nzuri, timu inatakiwa iangalie ushindani kimataifa …ndiyo maana hata wakipangiwa timu kutoka Misri, Ivory Coast n.k mnaingiwa na hofu kubwa,”alisema.
“zamani vilabu vya nje vilikuwa vikipangwa na timu za Tanzania zinatetemeka lakini sisi sasa…kama tunataka kurudi katika heshima yetu ya zamani tujipange kimataifa, “aliongeza Sumaye.
Aidha, Sumaye alisikitishwa na migogoro katika vilabu na kusema inachangia pia kudidimiza soka hivyo amewataka viongozi kuhakikisha wanafanya kazi kwa ushirikiano sambamba na kuvihudumia ipasavyo vilabu vyao.
Sumaye ambaye ni mpenzi mkubwa wa mabingwa wa ligi kuu soka Tanzania Bara Simba, alitumia fursa hiyo kuwaasa mashabiki na wanachama wa timu za Simba na Yanga kuzomeana uwanja pindi moja ya timu inapokuwa uwanjani.
“Muwe wapinzani katika michezo lakini si uhasama, lazima tuwe na urafiki baina yetu na kuonyesha uzalendo zaidi kwa Simba kuishangilia Yanga ikicheza na timu ya nje au Yanga kuishangili Simba ikicheza na timu ya nje,”aliongeza.
Sumaye pia alitumia nafasi hiyo kuwapongeza washindi wote na kuwataka kutovimbishwa vichwa na zawadi hizo badala yake wazitumie kama kichocheo cha kujibiidiisha zaidi.
Awali Mkuu wa Masoko na Mawasiliano wa Vodacom Kelvin Twisa alisema kampuni yake imetoa zaidi ya shilingi milioni 113 kama zawadi za washindi hao na hivyo kufanya mwaka huu zwadi kuongezeka tofauti na mwaka jana zilikuwa shilingi milioni 90.8.
“Tunajivunia kuwa wadhamini wa ligi kuu bara ambapo vipaji vingi vimeonekana na viwango vya kuvutia pia katika mechi zote na ndio maana hii leo tupo katika kutoa zawadi kwa washindi,”alisema.
Katika halfa hiyo, ilitambulishwa tuzo mpya inayohusisha wachezaji vijana waliofanya vema kwenye timu hizo ambapo waliotwaa ni pamoja na Rashid Mandawa (Coastal Union), Hassan Dilunga (Ruvu Shooting) na Frank Damayo aliyekuwa anaichezea JKT Ruvu na sasa amesajiliwa Yanga ambapo kila mmoja alizawadiwa shilingi milioni moja.
Azam Fc ilifanikiwa kuongoza kwa kutwaa tuzo tano ikiwemo ile ya nafasi ya pili iliyowapatia sh.mil.22, timu yenye nidhamu (mil.7.8), kocha bora-Stewart Hall (mil.3.8), mfungaji bora- John Bocco (mil.3.9) na mchezaji bora- Aggrey Morris (mil.3.3).
Aidha mabingwa Simba walitwaa mil.50, huku kipa wake Juma Kaseja alitwaa tuzo ya kipa bora na kuzawadiwa Mil.3.3, wakati Yanga ilizawadiwa mil.15 kwa kushika nafasi ya tatu na Martin Sanya alitwaa tuzo ya mwamuzi bora na kuzawadiwa mil.3.8.
Ligi kuu ya Vodacom msimu wa 2011/2012 ilianza kutimua vumbi Agosti 20,2011 na kumalizikia Mei 6, 2012 na kuvishirikisha vilabu 14 vikiwemo Simba, Yanga, Azam Fc, African Lyon, Kagera Sugar, Mtibwa Sugara, Toto Africans, Moro United, JKT Ruvu, Ruvu Shooting, Coastal Union, Polisi Dodoma na Oljoro JKT.
No comments:
Post a Comment