KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, June 7, 2012

Mawakala wamgombea Okwi

KLABU ya Simba imesema mawakala kutoka nchi kadhaa wamejitokeza kutaka kumpeleka mshambuliaji, Emmanuel Okwi kwenda kufanya majaribio ya kucheza soka ya kulipwa katika nchi tatu barani Ulaya.
Mwenyekiti wa klabu ya Simba, Ismail Aden Rage aliwaambia waandishi wa habari mjini Dar es Salaam jana kuwa, mawakala hao wanataka kumpeleka Okwi katika nchi za Serbia, Uingereza na Austria.
Rage alisema klabu yake haina kipingamizi cha kumpeleka Okwi kufanya majaribio katika nchi hizo, isipokuwa inataka taratibu zifuatwe.
Hata hivyo, Rage hakuzitaja klabu, ambazo zinamtaka mchezaji huyo wala majina ya mawakala waliowasilisha maombi hayo.
Mwenyekiti huyo wa Simba alisema, klabu yake itakuwa tayari kumuuza Okwi kwa euro 500,000 (sh. milioni 990) iwapo itajitokeza klabu inayotaka kumsajili.
Rage alisema mchezaji huyo, ambaye kwa sasa yupo kwao Uganda, anatarajiwa kwenda katika moja ya nchi hizo wakati wowote kwa ajili ya kufanya majaribio hayo.
Okwi anatarajiwa kuichezea Uganda mwishoni mwa wiki hii katika mechi ya michuano ya kuwania kufuzu kucheza fainali za Kombe la Dunia za 2014.
Kwa mujibu wa Rage, uongozi wa Simba itamuandalia utaratibu mzuri mchezaji huyo wa kwenda kufanya majaribio hayo baada ya kuichezea Uganda katika mechi hiyo.
“Iwapo atafuzu majaribio hayo, tutamuuza kwa kiwango hicho cha pesa sio chini ya hapo,”alisema Rage,ambaye pia ni mbunge wa Tabora Mjini kwa tiketi ya CCM.
Akizungumzia usajili wa beki Kevin Yondan, anayedaiwa kuwa amesajiliwa na Yanga, Rage alisema madai hayo hayana msingi kwa sababu walishamalizana na mchezaji huyo.
Rage alisema ameshangazwa na taarifa zinazosambazwa na baadhi ya vyombo vya habari kwamba Yondan amesajiliwa na Yanga wakati ameshatia saini mkataba wa kuichezea Simba.
“Ninachoweza kusema ni kwamba, Yanga wanaweza kumsajili Yondan baada ya sisi kumuacha, lakini si vinginevyo,” alisema.
Alipoulizwa kuhusu hatma ya mchezaji Uhuru Selemani, Rage alisema mkataba wake unatarajiwa kumalizika mwishoni mwa mwezi huu na kwamba wanajipanga kumuongeza mkataba mwingine.
Katika hatua nyingine, Rage amesema timu yake inatarajiwa kuondoka mjini Dar es Salaam wiki ijayo kwenda katika mikoa ya Shinyanga na Mwanza kwa ajili ya ziara ya mechi za kirafiki.
Rage alisema Simba inatarajiwa kuondoka Juni 15 mwaka huu na kuongeza kuwa, ziara hiyo pia imelenga kutembeza kombe la ubingwa wa ligi kuu msimu huu kwa mashabiki wa mikoa hiyo.
Alisema Simba itacheza mechi yake ya kwanza ya kirafiki Juni 16 kwa kumenyana na Toto Africans mjini Shinyanga kabla ya kucheza mechi nyingi siku inayofuata dhidi ya timu watakayopangiwa na wenyeji wao.

No comments:

Post a Comment