KIPA namba mbili wa klabu ya Simba, Ally Mustafa 'Barthez' amesajiliwa na klabu ya Yanga kwa ajili ya msimu ujao wa ligi.
Habari kutoka ndani ya Yanga zimeeleza kuwa, Barthez ametia saini mkataba wa kuichezea timu hiyo kwa miaka miwili.
Uamuzi wa Yanga kumsajili Barthez umekuja baada ya kuamua kumuacha kwenye usajili wake, kipa wa zamani wa timu hiyo, Shaaban Kado.
Chanzo cha habari kutoka ndani ya kamati ya usajili ya Yanga kimeeleza kuwa, tayari Barthez ameshatia saini mkataba wa kuichezea Yanga baada ya kulipwa donge nono la fedha.
Hata hivyo, mmoja wa wajumbe wa kamati hiyo, aliyezungumza na Burudani, hakuwa tayari kutaja kiwango cha fedha alicholipwa kipa huyo.
Mjumbe huyo pia alithibitisha kutemwa kwa Kado, ambaye anatarajiwa kurejea katika klabu yake ya zamani ya Mtibwa Sugar ya Morogoro.
Kwa mujibu wa mjumbe huyo, uamuzi wa kumuacha Kado ulifikiwa kutokana na mapendekezo ya wajumbe wa kamati hiyo, inayoongozwa na Salum Rupia, ambao walidai kuwa, kiwango cha kipa huyo kimeshuka.
Chanzo hicho kilisema suala la Kado lilizua ubishani mkubwa miongoni mwa wajumbe wa kamati hiyo kabla ya kukubaliana kwa pamoja kumuacha kwenye usajili. Kado ameichezea Yanga kwa msimu mmoja.
Kado huenda akarejea Mtibwa kwa ajili ya kuziba pengo la Beniventura Mushi 'Dida', ambaye amejiunga na Azam kwa ajili ya msimu ujao.
Katika hatua nyingine, winga Kigi Makasi wa Yanga amejiunga rasmi na Simba kwa ajili ya msimu ujao wa ligi.
Kigi ametua Simba baada ya kutia saini mkataba wa kuichezea timu hiyo kwa miaka miwili. Kigi ni miongoni mwa wachezaji kadhaa waliotemwa na Yanga msimu huu.
Wachezaji wa Simba wameanza mazoezi jana kwenye gym moja iliyopo barabara ya Nyerere na Chang'ombe mjini Dar es Salaam.
Miongoni mwa wachezaji walioonekana kwenye mazoezi hayo ni pamoja na Kigi, Amri Kihemba, Abdalla Juma, Patrick Mbiyavanga na Machaku Salum.
Makamu Mwenyekiti wa kamati ya usajili ya Yanga, Seif Ahmed 'Magari' alithibitisha jana kuhusu kuachwa kwa Kigi na Kado na kuwatakia maisha mema wachezaji hao katika klabu zao mpya.
No comments:
Post a Comment