KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, June 7, 2012

Azam waanza mazoezi ya Kombe la Kagame

UONGOZI wa klabu ya Azam umetangaza kuwa, timu hiyo itaanza mazoezi ya kujiandaa kwa michuano ya soka ya Kombe la Kagame kuanzia kesho kwenye uwanja wa Chamazi, Dar es Salaam.
Meneja wa Azam, Patrick Kahemele alisema juzi kuwa, tayari wachezaji wa timu hiyo wameshaanza kuwasili Dar es Salaam kwa ajili ya maandalizi ya michuano hiyo.
Kahemele alisema wachezaji kutoka nje ya Tanzania wameshaanza kuwasili Dar es Salaam kwa maandalizi ya makazi kabla ya kuanza kwa mazoezi hayo kesho.
Katika hatua nyingine, klabu ya Azam imesema imeshamaliza usajili wake wa wachezaji kwa ajili ya msimu ujao wa ligi wa mwaka 2012/2013.
Katibu Mkuu wa Azam, Idrisa Nassoro ameueleza mtandao wa klabu hiyo wiki iliyopita kuwa, katika usajili wao, hawajamuacha mchezaji hata mmoja.
Idrisa alisema mchezaji Luckson Kakolaki alikuwa wa mwisho kufunga usajili wa timu hiyo kwa msimu ujao.
Kakolaki ni beki kisiki, ambaye amekuwa akiichezea Azam tangu ilipokuwa madaraja ya chini hadi ligi kuu. Beki huyo ndiye aliyeshinda tuzo ya mchezaji mwenye nidhamu msimu uliopita.
Kwa mujibu wa Idrisa, Kakolaki alimwaga wino wa kuichezea Azam wiki mbili zilizopita na kuzima uvumi uliozagaa kwamba kuna moja ya timu kubwa nchini iliyokuwa ikimuwania.
Idrisa alisema hakuna mchezaji yeyote wa Azam aliyejiunga na klabu nyingine kwa ajili ya msimu ujao na kuongeza kuwa, katika usajili wao, wamesajili wachezaji wawili wapya wa kigeni kutoka nje ya nchi. Aliwataja wachezaji hao kuwa ni George ‘Blackberry’ Odhiambo kutoka Randers FC ya Denmark na Deo Munishi Dida kutoka Mtibwa Sugar.
Alisema Blackbery anachukua nafasi ya Wahab Yahaya wa Ghana wakati Dida anachukua nafasi ya kipa Obren Curkovic kutoka Serbia.
Katibu Mkuu huyo wa Azam alisema timu yake imesajili wachezaji 27 kwa ajili ya msimu ujao na kuwapeleka kwa mkopo wachezaji wanne katika klabu zingine kwa ajili ya kuwapa uzoefu.
Alisema Kocha Stewart Hall aliamua wachezaji hao wauzwe kwa mkopo kutokana na mlundikano wa wachezaji katika nafasi wanazocheza.
Wachezaji wapya wa Azam ni pamoja na beki wa zamani wa Simba, Joseph Owino na nyota wengine kutoka kikosi cha vijana wa chini ya miaka 20, Aishi Salum, Juckson Wandwi, Dizana, Ibrahim Rajab Jeba na Joseph Kimwaga.
Kikosi kamili cha Azam FC kwa ajili ya msimu ujao ni kama ifuatavyo:Makipa ni Mwadini Ally, Deo Munishi ‘Dida’, Aishi Salum na Jackson Wandwi
Mabeki wa pembeni kulia ni Ibrahim Shikanda na Erasto Nyoni na wa kushoto ni Waziri Salum na Samih Haji Nuhu. Mabeki wa kati ni Luckson Kakolaki, Said Moradi, Joseph Owino na Aggrey Morris
Viungo ni Kipre Bolou, Abdulhalim Humud, Himid Mao, Salum Abubakar, Abdi Kassim Sadala, Ramadhani Selemani Chombo, Abdulghani Ghulam, Ibrahim Rajab Jeba, Jabir Aziz Stima na Ibrahim Joel Mwaipopo
Washambuliaji wa pembeni ni Kipre Tchetche, Mrisho Ngasa, Zahoro Pazi, Khamis Mcha na Odhiambo wakati washambuliaji wa kati ni Gaudence Mwaikimba na John Bocco ‘Adebayor’.

No comments:

Post a Comment