UNAWEZA kuita ni filamu ya soka au ama igizo lililokuwa linahusu mchezo huo. Hivyo ndivyo unavyoweza kulielezea tukio lililotokea mwanzoni mwa wiki hii kwenye kambi ya timu ya Taifa, Taifa Stars.
Viongozi wa klabu za Simba, Yanga na Azam walizua kizaazaa kwenye kambi ya Taifa Stars iliyopo kwenye hoteli ya Tansoma, Dar es Salaam, baada ya kila upande kugombea kukutana na kiungo chipukizi wa timu hiyo, Frank Domayo.
Lengo la viongozi wa klabu hizo lilikuwa kumshawishi kiungo huyo anayechezea klabu ya JKT Ruvu amwage wino wa kuzichezea timu hizo katika msimu ujao wa ligi.
Lakini hatimaye ni Yanga iliyofanikiwa kumnasa nyota huyo na kumsainisha mkataba wa miaka mitatu wenye thamani ya sh. milioni 20.
Habari za uhakika kutoka kwenye kamati ya usajili ya Yanga zimeeleza kuwa, nyota huyo atakuwa akilipwa mshahara wa sh. milioni moja kwa mwezi kwa kipindi chote cha miezi mitatu.
Domayo ni miongoni mwa wachezaji waliong’ara wakati Taifa Stars ilipocheza na timu za Ivory Coast na Gambia katika mechi za mchujo za kuwania kufuzu kucheza fainali za Kombe la Dunia za 2014 zitakazofanyika nchini Brazil.
Katika mechi ya kwanza iliyochezwa mjini Abidjan, Taifa Stars ilipigwa mweleka wa mabao 2-0 na Ivory Coast kabla ya kuichapa Gambia mabao 2-1 katika mechi ya pili iliyochezwa wiki iliyopita mjini Dar es Salaam.
Kiwango kilichoonyeshwa na Domayo katika mechi hizo mbili kimewavutia wadau wengi wa soka nchini, ambao wamemtabiria kiungo huyo kwamba atakuwa mmoja wa wachezaji nyota nchini miaka ijayo.
Kiungo huyo chipukizi alicheza vizuri zaidi na kwa ushirikiano mkubwa na beki Kelvin Yondan na kiungo mwenzake, Mwinyi Kazimoto katika mechi dhidi ya Gambia.
Akizungumza na Burudani kwa njia ya simu juzi kabla ya kutia saini mkataba huo, Domayo alikiri kufuatwa na viongozi wa klabu hizo tatu na zinginezo, lakini alisema alikuwa bado hajamwaga wino kwenye klabu yoyote.
Alizitaja timu zingine, ambazo viongozi wake wamekuwa wakimshawishi ajiunge nazo kuwa ni Mtibwa Sugar ya Morogoro na Coastal Union ya Tanga.
Hata hivyo, Domayo alisema timu yoyote inayomuhitaji, inapaswa kwanza kufanya mazungumzo na uongozi wa JKT Ruvu na kuongeza kuwa, atakuwa tayari kufuata maelekezo ya mwajiri wake. Kufuatia kadhia hiyo, uongozi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) uliamua kuweka ulinzi mkali kwenye kambi ya Taifa Stars na kuwazuia viongozi wa klabu za ligi kuu kukutana na wachezaji.
No comments:
Post a Comment