Na Aboud Mahmoud, Zanzibar
WAZIRI wa Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo wa Serikali ya Zanzibar, Said Ali Mbarouk ameitaka timu ya visiwa hivyo, Zanzibar Heroes ifanye kila inaloweza kutwaa Kombe la Chalenji mwaka huu.
Mbarouk amesema iwapo Zanzibar Heroes itafanikiwa kutwaa kombe hilo, atamzawadia kila mchezaji pikipiki aina ya vespa kama motisha.
Alitoa changamoto hiyo mwishoni mwa wiki iliyopita wakati wa hafla ya kuipongeza Zanzibar Heroes kwa kutwaa nafasi ya tatu katika michuano ya Kombe la Dunia kwa nchi zisizo wanachama wa Shirikisho la Soka la Dunia (FIFA).
Waziri Mbarouk alisema mafanikio iliyoyapata Zanzibar katika michuano hiyo iliyofanyika Kurdistan, Iraq yanapaswa kuwa chachu ya kutwaa Kombe la Chalenji katika mashindano yatakayofanyika Novemba mwaka huu mjini Dar es Salaam.
“Kuanzia sasa, lengo la Zanzibar Heroes liwe ni kutwaa kombe la Chalenji. Nawaomba viongozi wa Kamisheni ya Michezo, Baraza na ZFA mjitahidi na kushirikiana ili kuhakikisha piga ua, Kombe la Chalenji mwaka huu linakuja katika ardhi ya Zanzibar, "alisisitiza waziri huyo. Mbarouk alizitaka taasisi hizo zifanye kazi kwa karibu na ushirikiano mkubwa ili ziweze kukamilisha azma hiyo, ikiwa ni pamoja na kuanza maandalizi mapema badala ya kukurupuka.
Waziri huyo aliwazawadia wachezaji wa timu hiyo sh. 250,000 kila mmoja kutokana na kushika nafasi ya tatu katika michuano ya Iraq. Pia alimwongezea mchezaji Khamis Mcha sh. 100,000 kwa kufunga mabao matatu katika mechi mbili na Nadir Haroub aliyeibuka mchezaji bora.
Akizungumza katika hafla hiyo, nahodha wa Zanzibar Heroes, Abdi Kassim Babi aliishukuru serikali kwa kuiwezesha timu hiyo kusafiri kwenda Iraq kushiriki katika mashindano hayo.
Babi alisema changamoto walizozipata wakati wa michuano hiyo zimewapa mafunzo mengi na kuwapa uzoefu zaidi wa mashindano ya kimataifa.
Zanzibar Heroes iliongoza kundi B baada ya kuzifunga raetia na Tamil Eelam mabao 6-0 na 30. Baadaye ilifungwa mabao 2-0 na Cyprus katika nusu fainali kabla ya kuichapa Provence mabao 7-2 katika mechi ya kutafuta mshindi wa tatu.
No comments:
Post a Comment