KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, June 14, 2012

Nsajigwa, Kijiko kutua Simba

SIKU chache baada ya kupigwa kumbo na Yanga katika usajili wa beki Kelvin Yondan, klabu ya Simba imepanga kujibu mapigo kwa kuwasajili nyota wawili wa Jangwani.
Habari kutoka ndani ya kamati ya usajili ya Simba zimeeleza kuwa, klabu hiyo imeanza kuhaha kufanya mipango ya kuwasajili beki Shadrack Nsajigwa na kiungo Juma Seif Kijiko.
Kwa mujibu wa habari hizo, Simba imeshaanza kufanya mazungumzo ya awali na wachezaji hao, lakini tatizo kubwa lipo kwenye kiwango cha malipo ya usajili.
Mkataba wa Nsajigwa kuichezea Yanga umemalizika hivi karibuni na wiki iliyopita iliripotiwa kuwa, beki huyo alikwenda Kenya kwa ajili ya kufanya mazungumzo na viongozi wa Gor Mahia.
Uamuzi wa Simba kutaka kumnasa Nsajigwa umekuja siku chache baada ya kuripotiwa kuwa, beki wake wa kulia, Saidi Nassoro Chollo ameumua na hataweza kucheza soka kwa msimu mzima ujao.
Imeelezwa kuwa, maumivu aliyoyapata Chollo ni sawa nay ale aliyoyapata Uhuru Selemani mwaka juzi, ambayo yalimfanya ashindwe kucheza soka msimu mzima.
"Nsajigwa bado ni mchezaji mzuri sana na uwezo mkubwa na kikubwa zaidi ni uzoefu alionao, ambao ni hazina kubwa kwa klabu kama yetu ambayo sasa tunajaribu kuingiza vijana wadogo kama akina Singano na ndio maana tumeamua kuanza harakati za kumsajili,” kilisema chanzo cha habari.
Akimzungumzia Kijiko, chanzo hicho cha habari kimeeleza kuwa, lengo la kumsajili ni kulipa kisasi kwa Yanga, ambayo pia imemsajili kipa namba mbili wa timu hiyo, Ally Mustafa Barthez.
Chanzo hicho cha habari kilieleza kuwa, tayari mazungumzo ya awali kati ya uongozi wa Simba na kiungo huyo yameshaanza kufanyika, lakini bado hayajamalizika.
Kwa mujibu wa chanzo hicho, Kijiko bado ana mkataba wa kuichezea Yanga, hivyo kinachotazamwa ni lini mkataba huo utamalizika na iwapo wanaweza kuuvunja.

No comments:

Post a Comment