KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Wednesday, June 13, 2012

Mzee Mwinyi mgeni rasmi tuzo za TASWA kesho

MSHINDI wa tuzo ya mwanamichezo bora wa Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo nchini (TASWA) anatarajiwa kujulikana leo kwenye ukumbi wa Diamond Jubilee, Dar es Salaam.
Mgeni rasmi katika hafla hiyo, itakayoanza saa mbili usiku, anatarajiwa kuwa Rais mstaafu wa awamu ya pili, Ali Hassan Mwinyi.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini Dar es Salaam jana, Katibu Mkuu wa TASWA, Amir Mhando alisema maandalizi yote muhimu yamekamilika.
Tuzo zitakazotolewa ni dola 8,000 za Marekani (sh. milioni 12) kwa mwanamichezo bora wa jumla na sh. milioni moja kwa kila mwanamichezo bora wa kila mchezo.
Pia kutakuwepo na tuzo ya heshima, ambayo itatolewa kwa mwanamichezo aliyefanya vizuri na kuiletea nchi heshima kimataifa.
Wanamichezo wanaowania tuzo za mwaka huu katika soka ya wanaume ni John Bocco (Azam), Aggrey Morris (Azam) na Juma Kaseja (Simba).
Wanaowania tuzo hiyo kwa upande wa wanawake ni Asha Rashid(Mburahati Queens), Mwanahamisi Omary (Mburahati Queens),Fatuma Mustapha (Sayari) na Eto Mlenzi (JKT).
Mabondia wa kulipwa watakaowania tuzo hizo ni Benson Mwakyembe, Nasibu Ramadhan, Francis Cheka, Nassib Ramadhan naFadhil Majia wakati mabondia wa ridhaa ni Selemani Kidunda, Victor Njaiti na Abdalla Kassim.
Tuzo ya mwanariadha bora wa kike inawaniwa na Zakia Mrisho, Mary Naali na Jaqueline Sakila wakati kwa wanaume inawaniwa na Dickson Marwa, Alphonce Felix na Fabian Joseph.
Wanaowania tuzo ya mwanamichezo bora wa Tanzania anayecheza nje ni Henry Joseph, Mbwana Samatta na Sophia Mwasikili, tuzo ya mwanamichezo bora chipukizi inawaniwa na Theresia Ojode (wavu-Jeshi Stars), Shomari Kapombe (soka-Simba) na Salum Abubakar (soka-Azam).
Tuzo ya mwanamichezo bora wa nje anayecheza Tanzania inawaniwa na Haruna Niyonzima (Yanga), Kipre Tchetche (Azam) na Emmanuel Okwi (Simba).
Watakaowania tuzo za mwanamichezo bora wa netiboli ni Lilian Sylidion na Doritha Mbunda.
Tuzo zingine zitakazowaniwa ni za michezo ya kikapu, gofu, olimpiki maalumu, michezo ya walemavu, kuogelea, judo, wavu, tennis, baiskeli, kriketi na mikono.
Mshindi wa jumla wa tuzo hiyo mwaka jana alikuwa mcheza netiboli Mwanaidi Hassan wa timu ya JKT, aliyezawadiwa gari lenye thamani ya sh. milioni 12.

No comments:

Post a Comment