Msafara wa Yanga utakaokuwa uwanjani kwa ajili ya mechi ya marudiano ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Zamalek itakayochezwa wikiendi ijayo nchini Misri unatakiwa kuwa na watu wasiozidi 40.
Kwa mujibu wa maelekezo ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) yaliyotumwa jana Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), ni idadi hiyo tu inayotakiwa kwa vile Zamalek inakabiliwa na adhabu ya kucheza mechi hiyo bila washabiki.
Adhabu ya Zamalek kutocheza mechi mbili za nyumbani za michuano hiyo bila washabiki ilitolewa Aprili 20 mwaka jana na Bodi ya Nidhamu ya CAF iliyokutana jijini Johannesburg, Afrika Kusini.
Mechi dhidi ya Yanga ndiyo itakayokuwa ya kwanza kwa Zamalek kuanza kutumikia adhabu hiyo iliyotakana na washabiki wake kufanya fujo kwenye mechi ya michuano hiyo mwaka jana ilipocheza dhidi ya Club Africain ya Tunisia.
Hivyo kila timu (Yanga na Zamalek) katika mechi hiyo inatakiwa kuwa na wachezaji ambao wana leseni za CAF kwa ajili ya Ligi ya Mabingwa 2012. Pia benchi la ufundi katika kila timu linatakiwa kuwa na watu watano.
Kwa klabu zote mbili, kila moja imeruhusiwa kuingia na wajumbe wake wa Kamati ya Utendaji wasiozidi kumi. Mbali ya klabu hizo mbili, wengine waliotajwa kuruhusiwa kuingia uwanjani ni vijana 20 watakaofanya kazi ya kuokota mipira (ball-boys). Mechi hiyo itachezeshwa na waamuzi kutoka Morocco ambao ni Jihed Redouane, Rouani Bouazza na Bekkali Mimoun wakati mwamuzi wa akiba atakuwa Gihed Greisha wa Misri. Kamishna wa mchezo huo ni Ben Khadiga wa Tunisia.
MSUMBIJI KUTUA NCHINI FEBRUARI 26
Timu ya Taifa ya Msumbiji (Mambas) itawasili nchini kesho (Februari 26 mwaka huu) kwa ndege ya South African Airways. Ndege hiyo yenye mruko namba SA 186 inatarajia kutua Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) saa 7.55 mchana.
Msafara wa Mambas kwa ajili ya mechi dhidi ya Taifa Stars itakayochezwa Jumatano (Februari 29 mwaka huu) saa 10 kamili jioni kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam utakuwa na watu 29. Kati ya hao, 19 ni wachezaji wakati waliobaki ni maofisa wa timu hiyo.
Mwamuzi wa mechi hiyo Farouk Mohamed na wasaidizi wake Ayman Degaish, B.T Abo El Sadat na Gihed Greisha kutoka Misri watawasili nchini kesho (Februari 26 mwaka huu) kwa ndege ya Egypt Air. Kamishna ni Loed Mc Ian kutoka Afrika Kusini.
Tiketi kwa ajili ya mechi hiyo zitaanza kuuzwa Jumanne (Februari 28 mwaka huu) katika vituo vya vya Shule ya Sekondari Benjamin Mkapa, Kituo cha mafuta cha Bigbon kilichopo Msimbazi (Kariakoo), mgahawa wa Steers ulioko Barabara ya Samora/Ohio, Kituo cha mafuta cha Oilcom Ubungo na Uwanja wa Taifa.
No comments:
Post a Comment