KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Wednesday, February 8, 2012

Barakat, Aboutrika, Motaeb wajiuzulu kuichezea Al-Ahly

Aboutrika

Emad Motaeb

Barakat


CAIRO, Misri
WACHEZAJI nyota watatu wa kimataifa wa Misri, wametangaza kustaafu kucheza soka baada ya kushuhudia mapigano yaliyotokea wiki iliyopita na kusababisha vifo vya mashabiki 74 katika mji wa Port Said.
Viungo Mohamed Barakat, Mohamed Aboutrika na mshambuliaji, Emad Motaeb wa Al-Ahly wamekieleza kituo cha televisheni cha Misri kuhusu uamuzi wao huo mara baada ya vurugu hizo.
Hata hivyo, Barakat alishindwa kuweka wazi iwapo hatarudi tena uwanjani. Alisema anaweza kurudi uwanjani iwapo tu mashabiki waliofariki katika vurugu hizo watalipwa fidia.
Vurugu hizo zilitokea wiki iliyopita mara baada ya kumalizika kwa mechi ya ligi kati ya Al-Ahly na Al-Masry iliyochezwa mjini Port Said. Katika mechi hiyo, Al-Masry iliibwaga Al-Ahly mabao 3-1.
Chanzo cha vurugu hizo ni mashabiki wa Al-Masry kuvamia ndani ya uwanja baada ya mchezo huo kumalizika na kuwashambulia wachezaji na mashabiki wa Al-Ahly. Katika vurugu hizo, zaidi ya mashabiki 800 walijeruhiwa.
Barakat, Aboutrika na Motaeb ni miongoni mwa wachezaji walioiwezesha Misri kutwaa ubingwa wa Kombe la Mataifa ya Afrika mara tatu mfululizo.
Aboutrika na Barakat walikuwemo kwenye kikosi cha Al-Ahly kilichocheza dhidi ya Al-Masry wakati Motaeb aliingizwa kipindi cha pili.
Kwa mujibu wa ripoti, mashabiki wengi walifariki dunia kutokana na kunasa kwenye njia za kutokea kwenye uwanja huo wakati walipokuwa wakikimbia mapigano.
Motaeb alikuwa amerejea uwanjani baada ya kuwa majeruhi kwa wiki kadhaa, akisumbuliwa na maumivu ya mgongo wakati Barakat naye alikuwa amerejea uwanjani baada ya kukosa mechi nne za ligi kutokana na maumivu ya misuli.
Baada ya kushuhudia vurugu hizo, wanasoka hao watatu wamesema hawawezi kuendelea kucheza soka katika klabu hiyo wakati nchi yao ikiwa katika mazingira hayo.
“Watu wanakufa na hakuna anayefanya lolote. Ni kama vita,”alisema Aboutrika alipohojiwa na kituo cha televisheni cha Al-Ahly. “Hivi maisha ni rahisi kiasi hiki?”
Aboutrika na mshindi wa zamani wa tuzo ya mwanasoka bora wa Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC) na kwa kushirikiana na Barakat na Motaeb, wameiwezesha Al-Ahly kupata mafanikio makubwa katika soka barani Afrika.
Al-Ahly imewahi kutwaa ubingwa wa ligi ya Misrimara 36 na pia kutwaa taji la ligi ya mabingwa Afrika mara sita.
Wakati nyota hao watatu wakiamua kustaafu kuichezea Al-Ahly, Kocha Mkuu wa timu hiyo, Manuel Jose ameamua kureja kwao Ureno na kuitaka klabu hiyo ivunje mkataba wake.
Jose ameelezea jinsi alivyopigwa kwa fimbo na mijeredi na pia kushuhudia mashabiki wakiuawa wakati wa vurugu hizo, zilizosababisha vifo vya mashabiki 74.
“Nilipigwa kwa fimbo na mijeredi shingoni, kichwani na miguuni,”alisema Jose.
“Niliwashuhudia mashabiki wetu wakiuawa mbele yetu na hatukuwa na uwezo wa kufanya chochote,”aliongeza kocha huyo.
Baadhi ya watu walioshuhudia tukio hilo walisema, polisi waliokuwepo uwanjani hawakufanya jitihada kubwa katika kukabiliana na vurugu hizo.
Kocha Msaidizi wa Al-Ahly, Pedro Barny alisema: “Kilichotokea ni vigumu kukielezea.”
“Tangu mwanzo wa mchezo, mashabiki wa timu pinzani waliruhusiwa kuingia uwanjani na fataki na waliturushia mawe bila kuchukuliwa hatua yoyote,” alisema Pedro.
“Mwishoni, vurugu zilikuwa kubwa bila ya maofisa wa usalama kuchukua hatua. Tulijitahidi kuokoa maisha ya baadhi ya mashabiki, lakini wengi walikufa mbele ya macho yetu,”aliongeza.
Jose (65) amewahi kuichezea na kuifundisha timu ya Benfica ya Ureno kwa miaka mingi, lakini alisema tukio hilo la Misri limebadili maisha yake.
“Hakuna kilichotokea kwa mchezaji yeyote, lakini tunajisikia kuwa na majonzi makubwa na nilirejea Ureno kimya kimya, nikiwapa heshima mashabiki wetu waliopoteza maisha,”alisema kocha huyo.
“Napaswa kufikiria maisha yangu tofauti hivi sasa. Japokuwa kila mmoja ananipenda hapa Misri, uzoefu huu umebadili kabisa mwelekeo wa maisha yangu,” alisisitiza.
Shirikisho la Soka la Misri (EFF) limetangaza kusimamisha mechi zote za ligi nchini humo na kutangaza siku tatu za maombolezo kwa ajili ya kuwakumbuka mashabiki waliopoteza maisha yao.
Wakati EFF imetangaza kusimamisha ligi, serikali ya kijeshi ya nchi hiyo imeutimua madarakani uongozi wa shirikisho hilo kutokana na vurugu hizo.
Shirikisho la Soka la Dunia (FIFA) limetaka lipatiwe maelezo kutoka EFF kuhusiana na vurugu hizo na limeitaka serikali ya kijeshi ya nchi hiyo, kuurejesha mara moja madarakani uongozi wa shirikisho hilo.
Kwa mujibu wa katiba ya FIFA, serikali za nchi zilizo wanachama wake, haziruhusiwi kuingilia kati masuala ya soka, vinginevyo nchi husika husimamishwa uanachama.
Iwapo FIFA itachukua hatua hiyo kwa Misri, klabu za Zamalek, Al-Ahly na Ismailia zitaondolewa kwenye michuano ya klabu za Afrika na kutoa nafasi kwa wapinzani wao kusonga mbele.

No comments:

Post a Comment