PORT SAID, Misri
WAKATI Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) limetaka maelezo kutoka Chama cha Soka cha Misri kutokana na vifo vya watu 74 katika mechi ya soka, wachezaji wote wa timu ya Al-Ahly wamejiuzulu.
Mashabiki wa timu ya Al Masry walivamia uwanja mjini Port Said baada ya kupata ushindi uliowashangaza wa mabao 3-1 dhidi ya Al-Ahly, klabu yenye maskani yaka mjini Cairo, na kusababisha vifo vya watu hao.
Inadaiwa kuwa maofisa usalama na polisi hawakutuliza ghasia hizo kwa kina, na kwamba vurugu hizo zilizochochewa na tofauti za kisiasa zilizoikumba nchi hiyo tangu mwaka jana.
FIFA sasa imekitaka chama cha soka cha Misri kutoa maelezo ya kina juu ya chanzo cha vurugu hizo.
Wakati huo huo, kipa wa Al-Ahly, Sharif Ikrami, ambaye aliumizwa kutokana na vurugu hizo, amesema wachezaji wote wa timu hiyo wamejiuzulu mchezo wa soka.
Alisema ameshuhudia miili ya watu waliokufa ikipitishwa mbele yake katika chumba cha kubadilishia nguo.
"Kuna watu walikuwa wanakufa mbele yetu. Wote tumeamua hatuwezi kucheza soka tena. Hatuwezi kufikiria hilo tena,"alisema.
Mashabiki wa soka wa klabu hizo zenye upinzani wa jadi miaka mingi, wamelaumiwa kwa kusababisha soka ya Misri kuingia historia mbaya.
Kipa wa zamani wa Al-Ahly, Hani Seddik aliiambia BBC: "Sifikiri hili kama limetokana na soka. Waliosababisha fujo hawakuwa mashabiki wa mpira wa miguu."
No comments:
Post a Comment