'
Wednesday, February 1, 2012
OMOTOLA: Hakuna nisichoweza kukifanya
LAGOS, Nigeria
KWA sura na umbo, msanii Omotola Jalade wa Nigeria ana mvuto wa aina yake. Ni mcheza filamu, mwanamuziki, mama wa watoto wanne na ni mke wa rubani wa ndege.
Mwanamama huyo anashika nafasi ya nane kwa utajiri miongoni mwa wachezaji filamu wa kike nchini Nigeria. Utajiri wake unakadiriwa kufikia Naira milioni 75 za Nigeria.
Mbali na kucheza filamu nyingi, Omotola amerekodi albamu zaidi ya mbili za muziki wa dansi. Kwa kiasi kikubwa, mapato yake yanatokana na filamu, muziki na matangazo ya biashara.
Mwaka 2011 ulikuwa wa mafanikio makubwa kwa Omotola. Katika mwaka huo, alishiriki kucheza filamu tano kubwa, mbili alizicheza mwanzoni na zingine tatu mwishoni. Pia aliteuliwa kuwa balozi wa shirika la kimataifa la kutetea haki za binadamu nchini Nigeria.
Katika mahojiano na mtandao wa Nigeria Films hivi karibuni, Omotola alielezea kwa kina jinsi alivyoweza kupata mafanikio katika fani ya filamu, ushindi wake wa tuzo mbalimbali pamoja na masuala mengine ya kimaisha.
“Ninachokifanya ni kutekeleza majukumu yangu ya siku hadi siku. Ninayatambua na pia nakabiliana nayo kila yanapokuja mbele yangu. Hakuna nisichoweza kukifanya. Kusema kweli nimekuwa na bahati.
“Naishi maisha yangu. Naamini kile ninachokiamini. Siishi maisha yangu kwa lengo la kumridhisha mtu yeyote, hivi ndivyo nilivyo.
“Msemo wangu niupendao ni kwamba, kile unachokiona ndicho unachokipata. Kamwe siwezi kusema chochote nyuma yako, ambacho siwezi kukisema mbele yako. Hivi ndivyo nilivyo,”alisema mwanamama huyo mantashau.
Omotola alieleza kushangazwa kwake na taarifa,ambazo zimekuwa zikiripotiwa mara kwa mara kwenye vyombo vya habari vya Nigeria kwamba haelewani na baadhi ya wacheza filamu wenzake.
Alisema siku zote amekuwa akiziona habari hizo kama kituko ama kichekesho na kujikuta akicheka. Hata hivyo, alisema anaelewa ni kwa nini taarifa hizo zimekuwa zikiripotiwa mara kwa mara.
Mwanamama huyo alisema binafsi hayupo karibu na watu wengi si kwa sababu ya kazi ama ugomvi, bali kutokana na kutojihusisha na maisha wanayoishi.
“Kwanza, naishi mbali. Pili, katika makuzi yangu, sikuwa na marafiki wengi walionizunguka,”alisema Omotola.
Aliongeza kuwa, yeye si mtu wa kuhudhuria tafrija mara kwa mara ama kushindana na wenzake katika masuala ya mavazi na urembo. Alisema siku zote hapendi kujihusisha na mambo yanayoweza kumletea matatizo.
Omotola alisema hana muda wa kujengeana bifu na wacheza filamu wenzake kuhusu nani mkali kuliko mwenzake. Alisema kamwe huwa hapendi kujihusisha na masuala hayo.
“Sina marafiki wa karibu. Ninao watu ninaowapenda katika fani hii, na ambao naweza kusema nawaelewa. Ninapokuwa kazini, ninashirikiana na kila mtu. Nataniana na kila mtu,”alisema.
Hata hivyo, Omotola alikiri kuwa, ushindani katika fani ya filamu ni jambo zuri na kuongeza kuwa, binafsi anapenda kuwepo kwa ushindani.
“Lakini navutiwa nao pale unapokuwa na faida, kinyume na hapo, nitaanza kuuchukia na kujiweka kando,”alisema mwanamuziki huyo.
“Napenda ushindani kwa sababu unamfanya msanii apanuke zaidi kiakili. Fikiri iwapo angekuwa Omotola pekee, anayeigiza, ingechosha.
“Kuna haja ya kuwepo kwa damu changa na lazima awepo mtu wa kukupa changamoto hapa na pale. Ushindani ukiwa na manufaa, unavutia na kumsaidia kila mmoja kujiweka vizuri. Yeyote asiyependa ushindani, ni adui,”aliongeza.
Wakati huo huo, Omotola wiki hii aliwapa tuzo maalumu wanawake 10 wajane kwa kuwaremba na kuwapa zawadi mbalimbali.
Omotola ameonyesha upendo huo kwa wanawake hao, akiwa na lengo la kumuenzi mama yake mzazi, ambaye alifariki dunia miaka 10 iliyopita.
Mwanamama huyo alitumia siku tano kubadili mwonekano wa wanawake hao kwa kuwapeleka klinini ya urembo, ambako walihudumiwa na wataalamu wa fani hiyo.
Baada ya kupatiwa huduma hiyo, wanawake hao walionekana tofauti na walivyokuwa awali, ambapo wamekuwa na mvuto wa aina yake.
Mbali na kuwapiga sopusopu, Omotola pia aliwanunulia wanawake hao nguo na kisha kupigwa picha na mtaalam wa kazi hiyo. Picha za wanawake hao kabla na baada ya kupewa huduma hiyo, zinapatikana kwenye mtandao wa Nigeria Films.
Wanawake hao pia walipatiwa zawadi ya magunia ya mchele, vifaa vya jikoni na vitu vingine kadhaa. “Hiki ni kitu ambacho natamani mtu mwingine angekifanya kwa mama yangu. Ukiwapa pesa wanawake hawa, watazitumia kwa ajili ya watoto wao.
“Wakati mama yangu alipokuwa hai, sikuelewa kwamba ningempoteza haraka. Hiki ni kitu, ambacho ningependa kukifanya kwa mama yangu, ambaye alikuwa mjane kwa miaka 10,”alisema Omotola.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment