KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, February 23, 2012

Simba yaipania Kiyovu



UONGOZI wa klabu ya Simba umeandaa mikakati kabambe kwa lengo la kuhakikisha wanaipa kipigo kikali Kiyovu ya Rwanda katika mechi ya marudiano ya michuano ya Kombe la Shirikisho. Mikakati hiyo ilianza kuandaliwa juzi katika kikao cha kamati ya utendaji ya klabu hiyo kilichofanyika mjini Dar es Salaam chini ya makamu mwenyekiti wake, Geofrey Nyange ‘Kaburu’.
Katika kikao hicho, kamati hiyo ilijadili ripoti ya Kocha Milovan Cirkovic kuhusu mechi ya awali kati ya timu hizo iliyochezwa mjini Kigali, Rwanda.
Katika mechi hiyo, Simba ilitoka sare ya bao 1-1 na Kiyovu na hivyo kujiweka kwenye nafasi nzuri ya kusonga mbele. Timu hizo zinatarajiwa kurudiana wiki mbili zijazo kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Habari kutoka ndani ya kikao hicho zimeeleza kuwa, Simba imepania kuishinda Kiyovu idadi kubwa ya mabao kwa lengo la kujenga heshima kwa klabu hiyo.
Mmoja wa wajumbe wa kamati hiyo aliieleza Burudani kuwa, moja ya sababu zilizoifanya timu hiyo ishindwe kuibuka na ushindi katika mechi hiyo ni wachezaji kuathiriwa na hali ya hewa.
Kikao hicho kiliamua kuwa, timu iingie kambini mara baada ya Taifa Stars kumenyana na Msumbiji katika mechi ya kuwania kufuzu kucheza fainali za Afrika za mwaka 2013. Mechi hiyo inatarajiwa kuchezwa Februari 29 mwaka huu.
Simba imeshindwa kuingia kambini mapema kujiandaa kwa mechi hiyo kutokana na wachezaji wake tisa kuitwa kwenye kikosi cha Taifa Stars, ambacho leo kitamenyana na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo katika mechi ya kirafiki.
Mbali na timu kuingia kambini mapema, kamati hiyo pia imepanga kuwazawadia wachezaji donge nono la fedha iwapo watashinda mechi hiyo na kusonga mbele.

No comments:

Post a Comment