'
Wednesday, February 22, 2012
Real Madrid yanywea kwa CSKA Moscow
MOSCOW, Russia
MCHEZAJI Debutant Wernbloom wa CSKA Moscow ya Russia juzi alizima furaha ya Real Madrid ya Hispania baada ya kufunga bao la kusawazisha dakika za majeruhi.
Wernbloom alifunga bao hilo dakika ya 93 kwa shuti lililombabatiza beki Alvaro Arbeloa wa Real Madrid na kuzima furaha ya mashabiki wa timu hiyo waliokuwa na uhakika mkubwa wa kuiona timu yao ikitoka uwanjani na ushindi.
Katika mechi hiyo ya awali ya hatua ya mtoano iliyochezwa kwenye uwanja wa Luzhniki mjini Moscow, Real Madrid ilikuwa ya kwanza kupata bao dakika ya 28 kupitia kwa Cristiano Ronaldo, likiwa bao lake la 38 msimu huu.
Kufuatia sare hiyo, timu yoyote itakayoshinda mechi ya marudiano itakayochezwa Machi 14 mwaka huu mjini Madrid, itasonga mbele.
Katika mechi hiyo, mshambuliaji Karim Benzema wa Real Madrid alilazimika kutolewa uwanjani mapema baada ya kuumia. Nafasi yake ilichukuliwa na Gonzalo Higuain.
Kocha Jose Mourinho wa Real Madrid alikiri baada ya mechi hiyo kuwa, wapinzani wao walikuwa wagumu na wakali.
Hata hivyo, Mourinho alisema ameridhika na matokeo hayo, ingawa alilaumu kushindwa kupata mabao kipindi cha pili akidai Real Madrid ilicheza kwa kiwango bora.
"Tuliwabana wapinzani wetu, hawakuweza kupata nafasi ya kufunga. Tulipata nafasi nzuri za kufunga kipindi cha pili, lakini tulishindwa," alisema Mourinho.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment