KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, February 16, 2012

RD Dar aipasha Yanga



MKUU wa mkoa wa Dar es Salaam, Said Mecky Sadik ameutaka uongozi wa klabu ya Yanga kuacha kupapatikia kuwasajili wachezaji wenye majina makubwa.
Badala yake, Sadik ameitaka klabu hiyo kuwekeza zaidi kwenye soka ya vijana ili iweze kuibua vipaji vipya na kuviendeleza.
Sadik alitoa mwito huo mwishoni mwa wiki iliyopita katika hafla ya kuichangia timu hiyo iliyofanyika kwenye hoteli ya Peackok mjini Dar es Salaam.
Alisema anashangaa kusikia klabu ya Yanga ikihaha kutaka kumrejesha mshambuliaji wake wa zamani, Mrisho Ngasa, iliyemuuza kwa mamilioni ya pesa kwa klabu ya Azam msimu uliopita.
Mkuu huyo wa mkoa alisema huu si wakati mwafaka kwa Yanga kumsajili tena mchezaji huyo kwa kutumia fedha nyingi wakati wapo vijana wengi wenye vipaji na uwezo wa kuitumikia timu hiyo.
Sadik alisema Yanga imekuwa ikipoteza fedha nyingi kusajili wachezaji wa kigeni bila sababu wakati baadhi yao uwezo wao kisoka upo chini ikilinganishwa na wazalendo.
Alisema wakati umefika kwa Yanga kuwa na programu maalumu ya kuibua vipaji vya vijana na kuwaendeleza kama ilivyokuwa miaka ya 1970, ambapo wachezaji wengi waliong’ara baadaye, walichezea timu ya vijana ya klabu hiyo.
Mkuu wa mkoa alisema Yanga inapaswa kuiga mfano wa watani wao wa jadi Simba kwa kuwa na timu za vijana wa umri mbalimbali kwa lengo la kuwaendeleza ili waje kuitumikia timu hiyo miaka ijayo.

No comments:

Post a Comment