KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Wednesday, February 8, 2012

Barnaba kurekodi na Fally Ipupa mwezi ujao


MSANII nyota wa muziki wa kizazi kipya nchini, Barnaba anatarajiwa kuondoka nchini Machi 28 mwaka huu kwenda Ufaransa kurekodi wimbo wake mpya.
Barnaba atarekodi wimbo huo, unaojulikana kwa jina la ‘Tuachane kwa wema’ kwa kushirikiana na mwanamuziki nyota, Fally Ipupa wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo.
Msanii huyo kutoka katika kundi la THT amesema, maandalizi yote kwa ajili ya safari hiyo yamekamilika, ikiwa ni pamoja na kupata viza ya kuingia nchini humo.
Barnaba alisema pia kuwa, ameshapangiwa siku ya kurekodi wimbo huo katika moja ya studio maarufu katika Jiji la Paris.
Kwa mujibu wa Barnaba, wimbo huo utakuwa miongoni mwa nyimbo zake mpya, zitakazokuwamo katika albam yake itakayokuwa na nyimbo 10. Albamu hiyo inatarajiwa kukamilika Juni mwaka huu.
''Katika ndoto zangu za kimuziki, nimekuwa nikitamani sana kurekodi na mastaa wa ukweli duniani na Fally Ipupa ni mwanzo tu kwani wapo wengine, ambao tayari nimeshawasiliana nao na tayari wamenithibitishia kunipa shavu,”alisema.
Msanii huyo alisema hata Fally Ipupa alikuwa akipenda kurekodi naye baada ya kumpagawisha wakati wa moja ya maonyesho yake aliyoyafanya hapa nchini.
Mbali na kurekodi wimbo huo Ufaransa, pia alisema atarekodi video yake nchini humo na anatarajia itakuwa babu kubwa.
Alizitaja nyimbo zingine zitakazokuwemo kwenye albamu hiyo kuwa ni Gubegube, Sidhani kama na Roho si moyo, ambazo zimerekodiwa katika studio za THT.

No comments:

Post a Comment