KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Wednesday, February 8, 2012

Yanga yatwaa uongozi ligi kuu

MSHAMBULIAJI Kenneth Asamoah (kulia) wa Yanga akiwania mpira na Salvatory Ntebe (kushoto) wa Mtibwa timu hizo zilipomenyana jana katika mechi ya ligi kuu ya Tanzania Bara, iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. (Picha na Emmanuel Ndege).


MABAO yaliyofungwa na washambuliaji Kenneth Asamoah,Hamisi Kiiza na Shamte Ally jana yaliiwezesha Yanga kuiengua Simba katika uongozi wa ligi kuu ya soka ya Tanzania Bara baada ya kuichapa Mtibwa Sugar mabao 3-1.
Katika mechi hiyo iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, Yanga ilijipatia mabao hayo matatu katika kipindi cha pili baada ya timu hizo kumaliza dakika 45 za kipindi cha kwanza zikiwa suluhu.
Ushindi huo uliiwezesha Yanga kutwaa uongozi wa ligi hiyo kwa tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa kati yake na watani wao wa jadi Simba, kufuatia kila moja kuwa na pointi 34 baada ya kucheza mechi 16.
Yanga sasa imefunga mabao 28 na kufungwa mabao 13 wakati Simba imefunga mabao 25 na kufungwa 10. Azam imeshuka hadi nafasi ya tatu ikiwa na pointi 32, ikiwa imefunga mabao 18 na kufungwa sita.
Mtibwa ililazimika kumaliza mechi hiyo ikiwa na wachezaji 10 baada ya Saidi Mkopo kutolewa nje kwa kadi nyekundu dakika ya 33 na mwamuzi Ibrahim Kidiwa kutoka Tanga kwa kosa la kucheza rafu mbaya Stephano Mwasika wa Yanga.
Mtibwa ilikuwa ya kwanza kubisha hodi kwenye lango la Yanga dakika ya tano wakati Vicent Barnabas alipowatoka mabeki wawili wa timu hiyo, lakini wakati akijiandaa kufunga, kipa Shabani Kado alitokea na kuokoa hatari.
Yanga ilijibu mapigo dakika ya saba wakati Davis Mwape alipofumua shuti kali akiwa ndani ya 18, lakini mpira uligonga mwamba kabla ya kuokolewa na mabeki wa Mtibwa.
Katika dakika ya 14, Saidi Rashid wa Mtibwa Sugar alimtoka beki Nadir Haroub ‘Cannavaro’ wa Yanga na kufumua shuti kali, lakini lilitoka nje ya lango.
Dakika mbili baadaye, Mwape alifanikiwa kumtoka beki Salvatory Ntebe na kufumua shuti kali, lakini liligonga mwamba wa juu wa goli na kutoka nje.
Mwape alipata nafasi nyingine nzuri ya kufunga bao dakika ya 22 alipomtoka beki Salum Sued, lakini shuti lake lilitoka nje.
Rashid aliikosesha Mtibwa nafasi zingine nzuri za kufunga mabao dakika ya 30 na 32 baada ya kupewa pasi na Barnabas na Issa Rashid, kufuatia mashuti yake kutoka nje ya lango.
Kenneth Asamoah angeweza kuifungia Yanga bao dakika ya 45 alipopewa pasi akiwa ndani ya eneo la hatari la Mtibwa, lakini shuti lake lilitoka nje. Timu hizo zilikwenda mapumziko zikiwa suluhu.
Licha ya kucheza ikiwa na wachezaji pungufu, Mtibwa ililisakama lango la Yanga mara kwa mara kipindi cha pili, lakini washambuliaji wake, Javu na Barnabas hawakuwa makini.
Uzembe wa beki Mwasika wa Yanga nusura uipatie bao Mtibwa dakika ya 64 baada ya kupokonywa mpira na Javu ndani ya eneo la hatari, lakini wakati akijiandaa kufunga, kipa Kado alitokea na kuokoa.
Yanga ilihesabu bao lake la kwanza dakika ya 73 kupitia kwa Asamoah. Alifunga bao hilo kwa shuti kali lililogonga mwamba wa goli na kutinga wavuni.
Kiiza aliiongezea Yanga bao la pili dakika ya 80 baada ya kupokea pasi kutoka kwa Mwasika kabla ya Shamte kuongeza la tatu dakika ya 86 baada ya kupokea pasi kutoka kwa Haruna Niyonzima. Bao la kujifariji la Mtibwa lilifungwa na Issa Rashid dakika ya 89.
Yanga: Shaaban Kado, Godfrey Taita/Shamte Ally, Stephano Mwasika, Nadir Haroub, Athuman Idd, Salum Telela/Juma Seif, Omega Seme, Haruna Niyonzima, Davis Mwape, Hamisi Kiiza, Kenneth Asamoah.
Mtibwa Sugar: Deogratius Munisi, Juma Jaffar, Issa Rashid, Salvantory Ntebe, Salum Sued, Shaaban Nditi, Saidi Mkopi, Awadh Issa, Saidi Rashid, Thomas Mourice/ Hussein Javu na Vincent Barnabas/ Zuberi Katwila.

No comments:

Post a Comment