MSHAMBULIAJI wa Simba, Uhuru Selemani, akiwa amebanwa na mlinzi wa JKT Oljoro, Kalage Mgunda, timu hizo zilipokwaana katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, uliochezwa jana, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, ambapo Simba iliibuka na ushindi wa mabao 2-0. (Na Mpigapicha Wetu).
SIMBA jana iliendelea kujiimarisha kileleni katika msimamo wa ligi kuu ya soka ya Tanzania Bara baada ya kuichapa JKT Oljoro mabao 2-0.
Katika mechi hiyo iliyopigwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, Simba ilijipatia mabao hayo mawili katika kipindi cha pili kupitia kwa mshambuliaji wake nyota, Emmanuel Okwi.
Simba ililazimika kucheza sehemu kubwa ya pambano hilo ikiwa na wachezaji 10 baada ya mshambuliaji wake, Haruna Moshi ‘Boban’ kutolewa nje kwa kadi nyekundu kipindi cha kwanza.
Boban alionyeshwa kadi hiyo dakika ya 43 na mwamuzi Isihaka Shirikisho baada ya kumchezea rafu mbaya Omari Mtaki wa JKT Oljoro. Awali, Boban alikuwa ameonyeshwa kadi ya njano.
Kwa ushindi huo, Simba inaendelea kuongoza ligi hiyo ikiwa na pointi 34 baada ya kucheza mechi 15, ikifuatiwa na watani wao wa jadi Yanga wenye pointi 31. JKT Oljoro ni ya nne ikiwa na pointi 26.
JKT Oljoro ilianza mchezo huo kwa kufanya shambulizi la kushitukiza dakika ya tano baada Bakari Kigodeko kufumua shuti lililodakwa na kipa Juma Kaseja.
Dakika ya nane Simba ilitaka kujibu shambulizi hilo, lakini Haruna Moshi 'Boban' alifanyiwa madhambi na Omari Hamisi na dakika 16 Nassor Masoud alipiga mkwaju wa adhabu kufuatia Mwinyi Kazimoto kuchezewa rafu.
JKT Oljoro nusura ipate bao dakika 24 baada ya Kalage Gunda kupiga shuti lililopaa juu ya lango la Simba kabla ya Boban kufumua shuti dakika 30 lililotoka nje kidogo ya lango. Timu hizo zilikwenda mapumziko zikiwa suluhu.
Shangwe kwa mashabiki wa Simba zilianza dakika ya 78 wakati Okwi alipofunga bao la kwanza kufuatia kazi nzuri ya Uhuru Selemani kabla ya kuongeza la pili dakika ya 80.
Simba: Juma Kaseja, Nassor Masoud, Amir Maftah, Kevin Yondani, Shomari Kapombe, Jona Gerrard, Mwinyi Kazimoto, Patrick Mafisango, Gervais Kago, Haruna Moshi na Uhuru Selemani.
JKT Oljoro: Said Lubawa, Omari Hamisi, Ally Omari, Omari Mtaki, Marcus Ndeheli, Ally Mkanga, Kalage Gunda, Sunday Paul, Bakari Kigodeko, Amir Omari na Rashid Nassor.
No comments:
Post a Comment