KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Wednesday, February 8, 2012

Chaneta kuandaa fainali za Afrika


CHAMA cha Netiboli cha Afrika (NA) kimekipa Chama cha Netiboli Tanzania (CHANETA) nafasi ya kuandaa michuano ijayo ya netiboli ya Afrika.
Kaimu Katibu Mkuu wa CHANETA, Rose Mkisi alisema mjini Dar es Salaam jana kuwa, uamuzi huo ulifikiwa katika mkutano mkuu wa NA uliofanyika hivi karibuni mjini Windhoek.
Rose alisema michuano hiyo, ambayo itafanyika nchini kwa mara ya kwanza, imepangwa kufanyika kati ya Mei 8 na 18 mwaka huu Dar es Salaam.
"Hakika hii ni faraja kubwa kwetu na kwa wadau na mashabiki wa mchezo wa netiboli, ambao umeonekana kukua kila kukicha na kuiletea sifa kubwa nchi yetu katika michuano ya kimataifa," alisema.
Rose alisema hivi sasa uongozi wake unajipanga kusaka fedha na wadhamini ili kufanikisha michuano hiyo. Alisema chama chake kinahitaji sh. milioni 187 ili kiweze kuandaa michuano hiyo kwa ufanisi.
Kwa mujibu wa Rose, tayari chama chake kimeshaanza kuwasiliana na kampuni, taasisi na wadau mbalimbali ili kuwashawishi wajitokeze kudhamini michuano hiyo.
Rose alisema nchi 18 zilizo wanachama wa NA zinatarajiwa kushiriki katika michuano hiyo. Alizitaja baadhi ya nchi hizo kuwa ni Zambia, Zimbabwe, Afrika Kusini, Lesotho, Namibia na Uganda. Zingine ni Kenya, Malawi, Botswana, Rwanda, Burundi, Sudan, Ethiopia na wenyeji Tanzania.
Wakati huo huo, CHANETA inatarajia kuendesha semina yenye lengo la kukuza na kuboresha viwango vya makocha na waamuzi wa mchezo huo kati ya Machi 12 na 13 mwaka huu mkoani Dar es Salaam.
Rose alisema semina hiyo itaendeshwa na wakufunzi wawili, ambapo alisema mmoja atakuwa wa ndani na mwingine atatoka nje ya nchi.

No comments:

Post a Comment