'
Wednesday, February 1, 2012
Jahazi yamsimamisha mwimbaji wake nyota
KIKUNDI cha taarab cha Jahazi kimemsimamisha kazi mwimbaji wake nguli, Fatma Kassim kwa muda wa wiki mbili.
Fatma, ambaye anatamba kwa kibao chake cha Hakuna mkamilifu, alisimamishwa mwishoni mwa wiki iliyopita.
Mwimbaji huyo ameithibitishia Burudani kuhusu uamuzi huo wa kumsimamisha kazi, lakini hakueleza sababu za kusimamishwa kwake.
"Ni kweli nimesimamishwa kwa muda wa wiki mbili, lakini hadi sasa sijajua kosa langu, lililosababisha nisimamishwe," alisema.
Uamuzi wa kumsimamisha mwimbaji huyo, unadaiwa kufanywa na mmoja wa viongozi wa kundi hilo na amekuwa akifanya hivyo wakati mkurugenzi, Mzee Yussuf akiwa hayupo.
Kwa sasa, Yussuf yupo nchini Marekani alikokwenda kwa ziara ya maonyesho kadhaa ya muziki.
Imedaiwa kuwa, kila Yussuf anaposafiri nje ya nchi, hukabidhi madaraka kwa kiongozi huyo, anayedaiwa kufanya maamuzi kadri anavyopenda.
Katika hatua nyingine, kikundi cha Jahazi kimeanzisha klabu ya michezo inayojulikana kwa jina la Jahazi Sports Club.
Klabu hiyo ilianzishwa hivi karibuni, ikiwa na maskani yake maeneo ya Morogoro mjini Dar es Salaam.
Mkurugenzi wa klabu hiyo, Hamis Boha alisema juzi kuwa, kwa kuanzia, wameanzisha timu ya soka, ambayo inatarajiwa kushiriki katika mashindano mbalimbali.
Boha alisema lengo lao ni kuiwezesha timu hiyo ishiriki katika michuano ya ligi kuu.
Alisema timu hiyo imesheheni wachezaji wengi chipukizi na wenye vipaji vya kucheza soka na kuahidi kutoa ushindani kwa timu zingine.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment