Wachezaji wa Ghana wakishangilia bao lao la kuongoza dhidi ya Guinea. Timu hizo zilitoka sare ya bao 1-1.
FRANCEVILLE, Gabon
GHANA juzi ilifuzu kucheza robo fainali ya michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika baada ya kutoka sare ya bao 1-1 na Guinea katika mechi ya mwisho ya kundi D iliyochezwa mjini hapa.
Sare hiyo haikuwa na manufaa kwa Guinea, ambayo imetolewa hatua ya awali, kufuatia Mali kuibwaga Botswana mabao 2-1 katika mechi nyingine ya kundi hilo.
Ghana ilikuwa ikihitaji pointi moja ili iweze kutwaa uongozi wa kundi hilo na ilijipatia bao lake dakika ya 28 kupitia kwa Emmanuel Agyemang Badu.
Guinea ilisawazisha dakika chache kabla ya mapumziko kupitia kwa mshambuliaji wake, Abdoul Razzagui Camara.
Guinea ililishambulia lango la Ghana mara kwa mara kipindi cha pili, lakini washambuliaji wake, Sadio Diallo na Ismael Bangoura walishindwa kuzitumia vyema nafasi walizopata kufunga mabao.
Kwa matokeo hayo, Ghana sasa itakutana na Tunisia katika mechi ya robo fainali wakati Mali itacheza na Gabon.
Wakati huo huo, bao lililofungwa na mshambuliaji Seydou Keita dakika 15 kabla ya mchezo kumalizika, juzi liliiwezesha Mali kuibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Botswana.
Botswana ilikuwa ya kwanza kupata bao sekunde chache baada ya kuanza kwa kipindi cha pili kupitia kwa mshambuliaji wake, Mogakolodi Ngele.
Mali ilisawazisha dakika sita baadaye kwa bao lililofungwa na mshambuliaji Modibo Maiga, kufuatia kazi nzuri iliyofanywa na Abdou Traore.
No comments:
Post a Comment