KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, February 16, 2012

Niyonzima: Zamalek inafungika



KIUNGO wa klabu ya Yanga, Haruna Niyonzima amesema licha ya wapinzani wao, Zamalek kuwa ni timu kali, lakini wanafungika.
Niyonzima amesema kinachotakiwa kufanywa na wachezaji wa Yanga ni kucheza kwa ari na kujituma huku wakiwa na malengo.
Kiungo huyo wa kimataifa wa Rwanda alisema hayo wiki hii alipokuwa akizungumzia maandalizi yao kwa ajili ya pambano lao na Zamalek.
Yanga na Zamalek zinashuka dimbani keshokutwa kumenyana katika mechi ya awali ya raundi ya kwanza ya michuano ya klabu bingwa Afrika itakayochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Niyonzima alisema japokuwa Zamalek ni moja ya timu tishio barani Afrika, inaweza kufungwa na Yanga kama wachezaji watatimiza wajibu wao ipasavyo.
Alisema amewahi kucheza na Zamalek alipokuwa akichezea timu ya APR ya Rwanda na waliweza kuifunga mjini Kigali na kutoka nayo sare mjini Cairo.
‘Hakuna timu isiyofungika katika soka. Ni kweli timu za Misri zina mbinu nyingi, hasa zinapocheza kwao, lakini zinafungika,”alisema.
Kiungo huyo tegemeo wa Yanga alisema kuvurunda kwa timu yake katika baadhi ya mechi za ligi kuu ya Tanzania Bara hakuna maana kwamba haina uwezo wa kuikabili Zamalek.
Alisema mechi za ligi ni tofauti na zile za michuano ya kimataifa na kwamba wachezaji hubadilika zaidi wanapopambana na timu ngumu.
”Katika ligi, timu zinakuwa zimezoeana na kufahamiana sana kimchezo, lakini katika mechi za kimataifa, wachezaji wanabadilika. Hivyo usishangae ukiiona Yanga inacheza tofauti itakapokutana na Zamalek,”alisema.
Amewataka wachezaji wenzake wa Yanga kucheza kwa ari na kujituma katika mechi hiyo huku wakiwa na dhamira ya ushindi na kusonga mbele.
Amewatoa hofu mashabiki wa Yanga kwa kuwataka wafike uwanjani kwa wingi kuishangilia na kuondokana na hofu kwamba timu yao inaweza kufungwa idadi kubwa ya mabao.

No comments:

Post a Comment