KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, February 16, 2012

Simba ipo gado-Kaburu


TIMU ya soka ya Simba inaondoka nchini kesho kwenda Rwanda kwa ajili ya mechi yao ya michuano ya Kombe la Shirikisho dhidi ya Kiyovu.
Makamu Mwenyekiti wa Simba, Geofrey Nyange ’Kaburu’ alisema mjini Dar es Salaam jana kuwa, timu yake itakwenda Rwanda ikiwa na wachezaji 18 na viongozi watano.
Kaburu alisema Simba inakwenda Rwanda huku ikiwa imechukua tahadhari kubwa kwa hofu ya kuhujumiwa na wapinzani wao.
Alizitaja baadhi ya tahadhari walizochukua kuwa ni pamoja na kuwa makini na hoteli watakayopangiwa na wenyeji wao na uwanja watakaotumia kwa mazoezi.
Kiongozi huyo wa Simba alisema wamepata taarifa kutoka kwa mashushu wao kwamba, Kiyovu imepanga mbinu chafu za nje ya uwanja kwa lengo la kuwatisha na kuwapa hofu wachezaji na viongozi wa timu hiyo.
Alisema tayari baadhi ya watendaji wa Simba wameshatangulia kwenda Rwanda kwa ajili ya kuweka mambo sawa na pia kuhakikisha wanapambana na mbinu hizo.
"Tumejiandaa vizuri, tulipata kanda za michezo mbalimbali ya Kiyovu na tumezifanyia kazi. Kocha amepanga vizuri programu yake kuhakikisha tunashinda mjini Kigali,"alisema.
Kaburu amewashukuru maofisa wa ubalozi wa Tanzania nchini Rwanda kwa kuwapa ushirikiano mkubwa katika kujiandaa na mechi hiyo.
Kikosi cha Simba kinachotarajiwa kwenda Rwanda ni makipa Juma Kaseja, Ally Mustapha, Juma Nyosso, Kelvin Yondani, Saidi Nassoro, Juma Jabu, Shomari Kapombe, Patrick Mafisango, Haruna Moshi na Mwinyi Kazimoto.
Wengine ni Salum Machaku, Edward Christopher, Ramadhani Singano, Gervas Kago, Rajabu Isihaka, Uhuru Selemani, Felix Sunzu na Emmanuel Okwi.
Simba na Kiyovu zinatarajiwa kushuka dimbani keshokutwa katika mechi itakayochezwa kwenye Uwanja wa Amahoro mjini Kigali na kurudiana wiki mbili baadaye mjini Dar es Salaam.

No comments:

Post a Comment