KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Wednesday, February 8, 2012

SMZ yazipiga jeki Mafunzo na Jamhuri



SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) imeamua kuzipiga jeki timu za soka za Mafunzo na Jamhuri kwa kuzipatia sh. milioni 15 kila moja.
Msaada huo umelenga kuziwezesha timu hizo zishiriki vyema katika michuano ya klabu za Afrika, inayotarajiwa kuanza wiki ijayo.
Mafunzo inatarajiwa kushiriki katika michuano ya klabu bingwa Afrika wakati Jamhuri itashiriki katika michuano ya Kombe la Shirikisho.
Kwa mujibu wa ratiba, Jamhuri imepangwa kumenyana na Hwange ya Zimbabwe katika mechi itakayopigwa Februari 18 mwaka huu kwenye Uwanja wa Gombani, Pemba wakati Mafunzo itacheza na Muculamana de Maputo ya Msumbiji katika mechi itakayopigwa Februari 19 mwaka huu kwenye Uwanja wa Amaan, Zanzibar.
Uamuzi huo wa serikali kuzipiga jeki timu hizo umekuja siku chache baada ya kuunda kamati maalumu ya kuendeleza michezo Zanzibar (KUMIZA).
Msemaji wa kamati hiyo, Ali Saleh alisema wiki hii mjini hapa kuwa, timu hizo mbili zinahitaji msaada mkubwa ili kufanikisha ushiriki wao katika michuano hiyo.
Mbali ya kutoa kiasi hicho cha pesa, serikali pia imetoa dola 9,000 za Marekani (sh. milioni 13.5) kwa ajili ya kuwagharamia waamuzi watakaochezesha mechi ya Mafunzo na Hwange.
Saleh alisema serikali haijatoa pesa hizo kwa Jamhuri kwa vile timu hiyo imesema inao uwezo wa kumudu gharama za waamuzi.
Kamati hiyo iliyoundwa na serikali inaongozwa na Sharifa Khamis, katibu wake ni Suleiman Mahmoud Jabir na wajumbe ni Khamis Abdalla, Ali Khalil Mirza na Saleh.
Serikali imesema kamati hiyo imeundwa kwa lengo la kusaidia michezo yote visiwani Zanzibar badala ya mchezo wa soka pekee.

No comments:

Post a Comment