KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Wednesday, November 30, 2011

Masikini Mercy Johnson





LAGOS, Nigeria
NI vigumu kuamini, lakini habari za uhakika kutoka vyanzo mbalimbali ndivyo zinavyosema. Kwamba jicho la kulia la mwigizaji nyota wa filamu nchini Nigeria, Mercy Johnson limeharibika.
Kwa mujibu wa vyanzo hivyo vya habari, Mercy aliumia jicho lake hilo hivi karibuni wakati akiwa kwenye eneo la kuchezea filamu huko Asaba katika Jimbo la Delta.
Vyanzo hivyo vimesema mrembo huyo alipatwa na maumivu hayo baada ya kutokea ugomvi kati yake na mwigizaji mwenzake, ambaye jina lake halikuweza kufahamika mara moja.
Taarifa zinasema familia ya mcheza filamu huyo, aliyefunga ndoa hivi karibuni, imekuwa ikihaha ili kuhakikisha anafanyiwa operesheni ya kurekebisha jicho lake mjini London, Uingereza.
Kuumia kwa Mercy kumeelezwa kuwa, kumemtia majonzi makubwa kiasi cha kumfanya asiwe na raha huku akiwaza nini la kufanya ili aweze kurejea katika hali ya kawaida.
Gazeti la Sun la Nigeria lilijaribu kuwasiliana na Mercy mara kadhaa ili kupata ukweli wa tukio hilo, lakini simu yake imekuwa ikiita kwa muda mrefu bila kupokelewa.
Filamu aliyokuwa akicheza Mercy imeandaliwa na Kampuni ya Magic Movies, imeandikwa na Micheal Jaja na kuongozwa na Jaja.

Hatimaye Aki afunga ndoa


LAGOS, Nigeria
HATIMAYE msanii nyota wa filamu wa Nigeria, Chinedu Ikedieze amefunga ndoa na mchumba wake wa muda mrefu, Nneoma Hope Nwajah.
Harusi hiyo ya kimila ilifanyika Jumamosi iliyopita kwenye kanisa katoliki la St. Theresa lililopo Obolo, Isiala Mbano, Jimbo la Imo.
Miongoni mwa watu maarufu waliohudhuria harusi hiyo ni pamoja na wacheza filamu nyota nchini humo, Segun Arinze, Uche Jombo, Oby Edozien na Ejike Asiegbu.
Watu wengine maarufu waliohudhuria harusi hiyo ni Gavana wa jimbo la Abia na mkewe pamoja na swahiba mkubwa wa Aki, Osita Iheme ‘Ukwa’.
Katika harusi hiyo, Aki alikuwa kivutio kikubwa kwa wageni waalikwa kutokana na kuvaa kofia na miwani myeusi pamoja na kushika fimbo kubwa ya kutembelea.
Maharusi hao wawili walioanza kuchumbiana miaka mitatu iliyopita, walitunzwa fedha nyingi na wageni waalikwa na muda wote walionekana kujawa na furaha kubwa.
Sherehe nyingine ya harusi hiyo imepangwa kufanyika Desemba 10 mwaka huu mjini Lagos.

Msondo, Sikinde uso kwa uso Krismas


BENDI kongwe za muziki wa dansi nchini, Msondo Ngoma na Mlimani Park Orchestra zimepanga kufanya onyesho la pamoja Desemba 25 mwaka huu kwenye viwanja vya klabu ya Sigara, Chang’ombe, Dar es Salaam.
Wakizungumza na Burudani kwa nyakati tofauti mjini Dar es Salaam juzi, viongozi wa bendi hizo walisema, onyesho hilo litadhaminiwa na Kampuni ya Konyagi.
Meneja wa Msondo Ngoma, Saidi Kibiriti alisema lengo la onyesho hilo ni kuimarisha umoja na ushirikiano kati ya wanamuziki wa bendi hizo kongwe nchini.
Kibiriti alisema bendi zote mbili zimekubaliana kuporomosha nyimbo mchanganyiko, zikiwemo za miaka 50 iliyopita na za sasa kwa lengo la kuwapa mashabiki burudani yenye vionjo na ladha tofauti.
“Hili si pambano la kutafuta nani mkali kati yetu, tunawaomba mashabiki waelewe hivyo, ni onyesho na kujenga na kuimarisha mshikamano kati ya wanamuziki wetu,”alisema.
Kwa upande wake, Katibu wa Mlimani Park, Hamisi Milambo alisema, maandalizi kwa ajili ya onyesho hilo yameshaanza na yanaendelea vizuri.
Milambo alisisitiza kuwa, lengo la bendi hizo si kupambana ili kumtafuta nani mkali kati yao, bali ni kuwapa mashabiki burudani kabambe ya muziki.
Hii itakuwa ni mara ya pili kwa Msondo na Mlimani Park kufanya onyesho la pamoja mwaka huu. Zilikutana kwa mara ya kwanza Juni mwaka huu katika onyesho lililofanyika kwenye ukumbi wa Diamond Jubilee, Dar es Salaam.
Onyesho hilo lilifanyika siku chache baada ya mwimbaji machachari nchini, Shabani Dede kuihama Mlimani Park na kujiunga na Msondo Ngoma.

JB: Tumeweza, tunasonga mbele



MSANII mkongwe wa fani ya filamu nchini, Jacob Steven amesema, maendeleo ya fani hiyo kwa sasa ni makubwa ikilinganishwa na miaka iliyopita.
Akihojiwa na kituo cha redio cha Clouds FM cha mjini Dar es Salaam wiki hii, Jacob alisema wakati fani hiyo ilipoanza, wasanii walikuwa wachache na walishindwa kunufaika nayo.
Msanii huyo, ambaye ni maarufu zaidi kwa jina la JB alisema, kadri miaka inavyosonga mbele, wasanii wamekuwa wakiongezeka na pia yamejitokeza mabadiliko makubwa katika utayarishaji wa filamu.
JB alisema hali hiyo imekuwa ikiwafanya wasanii nao waanze kunufaika na vipaji vyao kutokana na soko la filamu kuwa kubwa.
“Maendeleo wakati ule yalikuwa madogo kwa sababu ilikuwa ndio kwanza tunaanza. Wasanii wengi wa wakati ule hivi sasa hawapo,”alisema.
Aliwataja wasanii waanzilishi wa fani hiyo, iliyoanza kujipatia umaarufu miaka ya 1900 na ambao kwa sasa wamejiweka kando kuwa ni Bishanga, Aisha, Waridi na Mama Bishanga.
“Nina hakika katika miaka michache ijayo, ushindani katika fani ya filamu utakuwa mkubwa zaidi kwa sababu wasanii watazidi kuongezeka,”alisema.
Alisema katika miaka ya hivi karibuni, kumejitokeza wasanii wengi wa mitindo ya mavazi, urembo na wasomi wa kada mbalimbali, ambao wamezidi kuzinadhifisha filamu za kibongo na kuzifanya ziwe na mwonekano wa kimataifa.
“Kwa sasa tunao wasomi kutoka vyuo vikuu mbalimbali pamoja na Taasisi ya sanaa Bagamoyo. Kujitokeza kwao kwa wingi kunadhihirisha wazi kuwa, fani ya filamu hivi sasa inakubalika,”alisema.
Mbali na ongezeko la wasanii, JB alisema teknolojia inayotumika sasa katika kutengeneza filamu nayo ni ya juu zaidi na hivyo kuufanya ushindani uwe mkali.

Twenty Percent, Man Walter sasa ni chui na paka




HUWEZI kuamini. Pia unaweza kuita ni mchezo wa kuigiza ama filamu ya mauzauza. Ni kwa sababu kilichotokea, hakuna aliyekitarajia.
Ni kwamba mshindi wa tuzo tano za muziki za Kilimanjaro mwaka jana, Abbas Kinzasa 'Twenty Percent' na prodyuza wake, John Shariza, maarufu kwa jina la Man Walter hivi sasa hawaelewani. Ni sawa na chui na paka.
Unajua kisa ni nini?
Hakuna kingine zaidi ya mkwanja. Ndivyo inavyokuwa miaka yote utakaposikia msanii na prodyuza wake wamekorofishana. Sababu kubwa huwa ni kudhulumiana malipo.
Hivyo ndivyo ilivyotokea kwa Twenty Percent na Man Walter, ambao hivi karibuni walitoleana lugha kali, kila mmoja akimshutumu mwenzake kwamba ndiye chanzo cha kutokuelewana kwao.
Akihojiwa na kituo cha Radio One Stereo mwishoni mwa wiki iliyopita, Man Walter, ambaye ndiye mmiliki wa studio ya Combination Sound alisema, chanzo cha kutokuelewana huko ni ugomvi uliotokea kati yao kabla ya kuanza kwa onyesho lililofanyika mjini Morogoro.
Prodyuza huyo alisema, aliamua kuandaa onyesho hilo kwa ajili ya kumpongeza Twenty Percent na pia kuwashukuru mashabiki kwa kumpigia kura nyingi.
Alisema kabla ya kuanza kwa onyesho hilo, alifuatwa na Twenty Percent na kumtaka ampe malipo yake mapema. Alisema alipompa kwa mara ya kwanza, msanii huyo alikataa kupokea kiasi cha pesa alicholipwa kwa madai kuwa ni kidogo.
“Akaomba akabidhiwe malipo hayo mbele ya polisi, pia akakataa kupokea. Baadaye nikwamwita Afande Sele na kumkabidhi malipo hayo mbele yake, ndipo akakubali kupokea,”alisema Man Walter bila ya kufafanua kiwango hicho cha pesa.
Kwa mujibu wa Man Walter, licha ya kupokea malipo hayo, msanii huyo alitoa lugha kali kwake, akimshutumu na kumwita tapeli, aliyetumia kipaji chake kujinufaisha kimaisha.
Aliongeza kuwa, msanii huyo pia aliapa mbele za watu kwamba, hatorekodi tena nyimbo zake kwenye studio yake na wala asitarajie kufanyanaye kazi zingine.
“Kwa kweli maneno aliyoyatamka kwangu sikuyatarajia kabisa. Hata mashabiki waliofika ukumbini kushuhudia onyesho hilo walilalamika sana na kutoka nje,”alisema Man Walter.
Prodyuza huyo alisema, kilichomsikitisha zaidi ni kumsikia msanii huyo akiapa kwamba, atamfanyia kitu mbaya. Alisema alichokifanya si haki hata kidogo.
“Mimi ndiye niliyemtoa na kumpatia umaarufu kimuziki. Kutokana na makubaliano tuliyokuwa nayo, hakupaswa kurekodi nyimbo mpya kwa prodyuza mwingine. Alipaswa kunipa angalau nyimbo mbili,”alilalamika.
Kwa upande wake, Twenty Percent alisema si kweli kwamba haelewani na Man Walter, isipokuwa amerekodi nyimbo zake mpya kwenye studio zingine kwa lengo la kuzipa ladha tofauti.
“Sina ugomvi wowote na Man Walter, isipokuwa watu walipotuona tukibadilishana maneno makali, wakachukulia kwamba ugomvi wetu ni mkubwa,”alisema.
Msanii huyo alisema yeye na Man Walter ni marafiki wakubwa, iwe kikazi ama wanapokuwa mtaani wanapoishi na amekuwa akimchukulia kama kaka yake.
Alisema sababu kubwa iliyomfanya aamue kurekodi nyimbo zake mpya kwenye studio zingine ni kutokana na Man Walter kutingwa na kazi nyingi.
“Haya ni mabadiliko ya kawaida kimuziki. Nilichokifanya ni kubadili ladha ya muziki wangu ili nitoke kivingine badala ya vile nilivyozoeleka,”alisema.
“Man Walter ni kama kaka yangu. Tunapokuwa mtaani, yeye ndiye anayenipa mawazo mbalimbali kuhusu maisha, hatuna ugomvi, tupo pamoja,”alisisitiza.

MAVITUZ YA TWANGA PEPETA LONDON





MWIMBAJI wa bendi ya muziki wa dansi ya Twanga Pepeta International, Hamisi Amigolas akicheza huku akiwa amembeba mcheza shoo wa bendi hiyo, Tina Mjapan wakati wa onyesho lililofanyika mwishoni mwa wiki iliyopita mjini London, Uingereza.Juu ni mcheza shoo huyo akifanya mavituz. (Picha kwa hisani ya blogu ya Freddy Macha)

Chondechonde mwacheni Vengu-Seki


UONGOZI wa kundi la Orijino Komedi umevitaka vyombo vya habari nchini kuacha kumfuatilia msanii wake, Joseph Shamba ‘Vengu’ aliyelazwa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Dar es Salaam.
Mbali na kuviasa vyombo vya habari, kundi hilo pia limewaomba mashabiki wake kuacha kumsumbua msanii hiyo kwa kulazimisha kuingia kwenye chumba alimolazwa hospitalini hapo.
Kiongozi wa kundi hilo, Sekione David alisema mjini Dar es Salaam juzi kuwa, madaktari wanaomtibu Vengu wameshauri asibughudhiwe na watu.
“Madaktari na familia yake hawataki jambo hili liwe wazi kwa kila mtu, ugonjwa ni siri ya mgonjwa na madaktari kwa manufaa ya hospitali,”alisema Sekione, ambaye ni maarufu zaidi kwa jina la Seki.
Kiongozi huyo wa Orijino Komedi alisema, binafsi haruhusiwi kutoa taarifa zinazomhusu msanii huyo kutokana na kuzuiwa kufanya hivyo na madaktari.
“Hizi ni taratibu walizoweka madaktari na ndugu zake, hatuwezi kwenda kinyume ya hapo,”alisisitiza Seki.
Vengu amelazwa Muhimbili kwa zaidi ya miezi miwili huku ugonjwa wake ukifanywa kuwa siri kubwa. Kuna habari kuwa, msanii huyo anasumbuliwa na kichwa.
Kufuatia kulazwa hospitalini hapo kwa muda mrefu, baadhi ya vyombo vya habari vimekuwa vikitoa taarifa tofauti kuhusu ugonjwa unaomsumbua msanii huyo.
Katika kipindi cha Orijino Komedi wiki iliyopita, msanii maarufu kwa jina la Masanja alisikika akisema kwa masikitiko kwamba, hali ya Vengu bado haijatengemaa.
“Jamani jamani, Vengu anaumwa. Masikini jembe langu, linaumwa,”alisema.
Masanja alisema hayo, kufuatia mashabiki wengi wa kipindi hicho kuwapigia simu wakitaka kujua maendeleo ya afya ya msanii huyo.
Kutokana na kuthamini mchango wa msanii mwenzao, Masanja alisema wataendelea kutumia kazi zake zilizopita ili kuwaliwaza mashabiki wao.

Shakur aipiga jeki Uhuru SC



MFANYABIASHARA Shakur Sanya ameipatia klabu ya michezo ya Uhuru vifaa vya michezo kwa ajili ya timu yake ya soka.
Shakur, ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Mipango, Uchumi na Fedha ya CCM Kata ya Jangwani, alikabidhi vifaa hivyo juzi kwa Katibu wa klabu ya Uhuru, Rashid Zahor.
Vifaa vilivyotolewa na Shakur kwa klabu ya Uhuru ni seti moja ya jezi na mipira mitatu, vyote vikiwa na thamani ya sh. 500,000.
Hafla ya kukabidhi vifaa hivyo, ambayo ilifanyika kwenye ofisi za Shakur, mtaa wa Mafia, Dar es Salaam, pia ilihudhuriwa na nahodha wa timu ya soka ya Uhuru, Mussa Hassan.
Akizungumza wakati wa kukabidhi vifaa hivyo, Shakur alisema ameamua kutoa msaada huo kwa lengo la kuiimarisha timu ya Uhuru.
“Msaada huu pia ni utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi, ambayo inasisitiza umuhimu wa kuibua vipaji vya michezo na kuviendeleza,”alisema.
Shakur alisema msaada huo ni wa mwanzo kwake kwa Uhuru, lakini hautakuwa wa mwisho, hivyo ameahidi kuendelea kuisaidia kila itakapohitaji msaada kutoka kwake.
“Ninayo taarifa kwamba timu yenu imekuwa ikisafiri mara kwa mara mikoani kucheza mechi za kirafiki na hivi karibuni mnatarajia kwenda Arusha, nitajitahidi katika siku zijazo kuendelea kuwasaidia,”alisema.
Kwa upande wake, Zahor alimshukuru Shakur kwa kuwapatia msaada huo wa vifaa vya michezo na kuahidi kuwa, watautumia kwa malengo yaliyokusudiwa.
Alisema msaada huo umekuja wakati mwafaka kwa timu yake kwa vile wamepanga kucheza mechi kadhaa za kirafiki kwa ajili ya kujiandaa na michuano ya Kombe la NSSF.
Uhuru ilitwaa kombe hilo mara mbili mfululizo mwaka 2007 na 2008 na mwaka 2009 ilishika nafasi ya pili wakati mwaka jana ilishika nafasi ya tatu. Timu ya netiboli nayo ilitwaa kombe hilo mwaka 2007.
Klabu ya michezo ya Uhuru pia imewahi kutwaa ubingwa wa jumla wa bonanza la vyombo vya habari mwaka 2010 na 2009.
Klabu ya Uhuru inaundwa na wafanyakazi wa Kampuni ya Uhuru Publications Ltd, wachapishaji wa magazeti ya Uhuru, Mzalendo na Burudani, kituo cha Radio cha Uhuru FM na ofisi ndogo ya CCM.

Friday, November 25, 2011

Asante Kotoko kutua Dar Des 9



TIMU ya soka ya Kumasi Asante kotoko ya Ghana inatarajiwa kuwasili nchini Desemba 9 tayari kucheza mchezo mmoja wa kirafiki dhidi ya kombaini ya timu za Yanga na Simba siku ya Desemba 11 kwenye uwanja wa Taifa. Mchezo huo ni sehemu ya kukamilisha maadhimisho ya sherehe za miaka 50 ya Uhuru wa Tanzania na maandalizi yake yamekwisha kamilika kwa mujibu wa mwenyekiti mtendaji wa kampuni ya Future Century Limited, Helen Masanja. Masanja alisema kuwa timu hiyo itafikia Zanzibar na baadaye kuja jijini Dar es Salaam kwenye hotel ya Lamada tayari kwa mchezo huo ambao umedhaminiwa na PPF, Kenya Airways, Vanedrick Tanzania Limited, Lamada Hotel na Vanne Fashion Tabata. Alisema kuwa wanatarajia kuwa na burudani ya aina yake kwani tayari kombaini ya timu ya Yanga na Simba itaundwa na wachezaji nyota wanaocheza Ligi Kuu ya Tanzania Bara msimu huu. Aliongeza kuwa makocha wawili, mkongwe, Abdallah “King Mputa” Kibaden na Fred “ Minziro” Felix ndiyo watakuwa wakuu wa benchi la ufundi la timu hiyo ambayo itaundwa na wachezaji 20 watakaotangazwa hapo baadaye. Wengine katika benchi la ufundi na meneja, Boniface Pawasa na daktari wa timu, Juma Sufiani. Alifafanua kuwa uteuzi wa timu hiyo hautajali uraia wa wachezaji hivyo kama wachezaji kutoka nchi za nje ambao wanachezea timu hizo watateuliwa, basi watacheza mchezo huo.Masanja alisema kuwa Yanga na Simba zimekubaliana na kuweka historia kwa mara ya kwanza tangu timu hizo zitengane mwaka 1935. Alisema kuwa historia inaonyesha kuwa timu hizo zilikuwa pamoja kuanzia mwa 1922. Mwenyekiti wa Yanga Lyod Nchunga alisema kuwa mechi hiyo itaondoa tofauti iliyopo baina ya mashabiki wa Simba na wale wa Yanga hasa zinapotokea timu hizo zinacheza mechi za kimataifa ambapo imekuwa ni kawaida mashabiki wa timu hizo kushangilia timu pinzania. Wakati Nchunga akisema hayo, Katibu Mkuu wa Simba, Evodius Mtawala alisema kuwa muungano huo utaleta tija kwa timu hizo ambapo mashabiki wa Simba na Yanga siku hiyo watakuwa kitu kimoja kwa ajili ya kuishangilia timu yao tofauti na ilivyokuwa miaka ya nyuma.Alisema kuwa huu ndiyo mwanzo wa kuanza kushirikiana katika mechi za kimataifa na kuwataka mashabiki kufika kwa wingi na kutoa sapoti kubwa kwao

Tenga awa balozi wa malaria



Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania, Leodegar Tenga ambaye pia ni Rais wa CECAFA, akipokea tuzo baada ya kutangazwa kuwa Balozi wa United Against Malaria Tanzania na mmoja wa viongozi wa taasisi ya Johns Hopkins nchini, Anna McMartney (kushoto) katika hafla ya kuyakaribisha mashindano ya Tusker Challenge Cup yanaliyoanza kutimua vumbi jijini Dar es Salaam jana. Hafla hiyo iliyoandaliwa na United Against Malaria ilifanyika jana jijini humo.

KANIKI, JOHN WILLIAM WAPATA TIMU SWEDEN





Wachezaji wawili wa kitanzania, Joseph Kaniki (Golota) na William John wamefanikiwa kujiunga na timu ya ligi daraja la pili KonyaSpor (KIF) nchini Sweden, baada ya kufanikiwa kupita katika majaribio( Trials). Majaribio hayo yalijumuisha wachezaji zaidi ya thelathini ambapo wachezaji watano walichaguliwa kujiunga na klabu hiyo ya ligi daraja la pili KonyaSpor (KIF)

DIAMOND AIPUA ALBAMU MPYA



Nyimbo yangu mpya inaitwa Mawazo, nimerekodi studio za AM RECORD, producer Maneke, inapatikana katika albam yangu mpya ya inayoitwa LALA SALAMA, album ina nyimbo kumi ambazo ni

1) Moyo Wangu

2) lala salama

3) Chanda chema

4) Nimpende nani

5) najua

6) Mawazo

7) Kwanini

8) Gongolamboto

9) Natamani

10)Kizaizai

FAINALI KOMBE LA UHAI YASOGEZWA



Mechi ya fainali ya michuano ya soka ya vijana wenye umri chini ya miaka 20 ya Kombe la Uhai (Uhai Cup) kwa klabu za Ligi Kuu sasa itachezwa kesho (Novemba 26 mwaka huu) saa 3.00 asubuhi kwenye Uwanja wa Karume.

Awali fainali hiyo kati ya Simba, ambayo iliingia hatua hiyo kwa kuitandika Toto Africans mabao 4-1 na Azam, iliyofuzu kwa kuizamisha Serengeti Boys (timu ya Taifa ya vijana chini ya miaka 17) mabao 3-0, ilikuwa ichezwe leo (Novemba 25 mwaka huu) saa 9.00 kwenye uwanja huo.

Mabadiliko hayo yamefanyika ili kutoa nafasi kwa mashabiki kushuhudia mechi za michuano ya Kombe la Chalenji inayoanza leo (Novemba 25 mwaka huu) kwenye Uwanja wa Taifa.

Kila siku kwenye michuano ya Chalenji zinachezwa mechi mbili; ya kwanza saa 8.00 mchana na nyingine saa 10.00 jioni.

Michuano ya Kombe la Uhai inadhaminiwa na Kampuni ya S.S. Bakhresa kupitia maji Uhai ambapo bingwa atapata sh. milioni 1.5, mshindi wa pili sh. milioni moja wakati wa tatu atapata sh. 500,000.

Mbali ya fedha hizo, bingwa atapata medali za dhahabu, makamu bingwa medali za fedha na mshindi wa tatu medali za shaba. Mchezaji bora sh. 400,000, mfungaji bora (sh. 300,000), kipa bora (sh. 300,000) na timu yenye nidhamu sh. 300,000.

VIINGILIO MICHUANO YA KOMBE LA CHALENJI

Viingilio kwa mechi za hatua ya makundi kwa michuano ya Kombe la Chalenji inayoanza leo (Novemba 25 mwaka huu) kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam vitakuwa kama ifuatavyo;

Kwa viti vya rangi ya bluu na kijani ambavyo ni zaidi ya 30,000, kiingilio kitakuwa sh. 1,000 wakati viti vya rangi ya chungwa ambavyo ni zaidi ya 10,000 kiingilio kitakuwa sh. 3,000. VIP C na B ambayo jumla ya viti vyake ni 8,000 kiingilio kitakuwa sh. 5,000 wakati VIP A yenye viti 700 kiingilio ni sh. 10,000.

Tenga achaguliwa tena kuongoza CECAFA



TENGA ACHAGULIWA TENA CECAFA

Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Leodegar Tenga amechaguliwa tena kuwa Mwenyekiti wa Baraza la Vyama vya Mpira wa Miguu Afrika Mashariki na Kati (CECAFA).

Tenga amechaguliwa leo (Novemba 24 mwaka huu) bila kupingwa baada ya mpinzani wake Fadoul Hussein wa Djibouti kutotokea kwenye uchaguzi.

Kutokana na hali hiyo, mjumbe kutoka Uganda alitoa hoja ya Tenga kupitishwa bila kupingwa, hoja ambayo iliungwa mkono na Kenya, Tanzania, Uganda, Sudan, Zanzibar, Ethiopia, Burundi na Eritrea.

Jumla ya nchi wanachama zilizopiga kura katika uchaguzi uliofanyika hoteli ya New Africa ni kumi na moja, na kila moja ilikuwa na kura moja tu.

Kwa upande wa nafasi nne za wajumbe wa Kamati ya Utendaji kulikuwa na wagombea wanane. Waliopita katika raundi ya kwanza na kura zao kwenye mabano ni Abdiqani Saeed Arab wa Somalia (8), Tariq Atta Salih wa Sudan (8) na Raoul Gisanura wa Rwanda (8). Wengine katika raundi ya kwanza na kura walizopata kwenye mabano ni Sahilu Wolde wa Ethiopia (4), Justus Mugisha wa Uganda (4), Tesfaye Gebreyesus wa Eritrea (4), Hafidh Ali Tahir wa Zanzibar (2) naAbubakar Nkejimana wa Burundi (3).

Mjumbe aliyefanikiwa kushinda katika raundi ya pili na kuingia kwenye Kamati ya Utendaji ni Wolde wa Ethiopia aliyepata kura tano dhidi ya nne za Mugisha na mbili za Gebreyesus. Mwenyekiti anakaa madarakani kwa miaka minne wakati wajumbe wa Kamati ya Utendaji wanachaguliwa kila baada ya miaka miwili.

ZIMBABWE YAZIBA NAFASI YA NAMIBI

Timu ya Taifa ya Zimbabwe (Might Warriors) imeteuliwa na CECAFA kushiriki michuano ya Kombe la Chalenji inayoanza Novemba 25 mwaka huu jijini Dar es Salaam kuziba nafasi ya Namibia iliyojitoa. Zimbabwe itawasili Novemba 26 mwaka huu jijini Dar es Salaam na itakuwa kundi A pamoja na timu za Tanzania Bara, Rwanda na Djibouti.

KIKOSI CHA KILIMANJARO STARS

Kocha Mkuu wa timu ya Tanzania Bara (Kilimanjaro Stars), Charles Boniface Mkwasa ametaja kikosi cha mwisho cha wachezaji 20 kwa ajili ya michuano hiyo inayoanza kesho.

Wachezaji waliobaki kati ya 28 waliokuwa wameitwa awali ni Juma Kaseja (Simba), Shabani Kado (Yanga), Shomari Kapombe (Simba), Godfrey Taita (Yanga), Juma Jabu (Simba), Ibrahim Mwaipopo (Azam) ,Juma Nyoso (Simba), Said Murad (Azam), Erasto Nyoni (Azam) na Shabani Nditi (Mtibwa Sugar), Nurdin Bakari (Yanga), Haruna Moshi (Simba) na Mwinyi Kazimoto (Simba).

Wengine ni Said Maulid (Angola), Musa Mgosi (DC Motema Pembe, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo-DRC), Mrisho Ngassa (Azam), Ramadhan Chombo (Azam), Thomas Ulimwengu (TP Mazembe, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo- DRC), Mbwana Samata (TP Mazembe, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo- DRC) na Rashid Yusuf (Coastal Union).

Kilimanjaro Stars itacheza mechi yake ya kwanza Novembe 26 mwaka huu dhidi ya Rwanda.

Wednesday, November 23, 2011

GOFU KUSAIDIA WAGONJWA WA MACHO



Benki ya NIC Tanzania kwa kushirikiana na klabu ya Lions ya Dar es Salaam, imejitokeza kudhamini mashindano ya mchezo ya gofu kwa lengo la kusaidia watu wenye matatizo ya macho. Katika mashindano hayo, benki hiyo imetoa jumla ya dola za Kimarekani 2,000 (sawa na sh. milioni 3.5 za Tanzania) kwa lengo la kuinua afya za wananchi, hasa wanaosumbuliwa na matatizo ya macho.Pichani, Mkurugenzi na Mtendaji Mkuu wa NIC Tanzania, James Muchiri (kushoto) akiwa katika picha ya pamoja na Meneja Mikopo wa benki hiyo, Regina Mwengi, Prisalla Karobia na David Muthungu kabla ya kuanza kwa michuano hiyo iliyofanyika juzi kwenye viwanja vya Gymkhana, Dar es Salaam.

Ferej alalamikia ukiukwaji wa katiba ZFA


VURUGU zinazotokea mara kwa mara katika Chama cha Soka cha Zanzibar (ZFA) ni matokeo ya kukiukwa kwa katiba na kanuni za kuendesha mchezo huo.
Hayo yamesemwa na Rais wa ZFA, Ali Ferej Tamim wakati wa mkutano mkuu wa dharula wa chama hicho uliofanyika mwishoni mwa wiki iliyopita mjini hapa.
Mbali na kujadili masuala mbalimbali, mkutano huo uliitishwa kwa lengo la kufanya marekebisho ya katiba ya chama hicho.
Ferej alitoa kauli hiyo baada ya baadhi ya wajumbe wa kamati ya utendaji ya chama hicho kutoka Pemba, kulalamika kuwa, kimekuwa kikitoa maamuzi mengi bila ya kufuata katiba.
Wajumbe hao walilalamikia uamuzi wa ZFA wa kuirejesha Malindi katika ligi kuu bila kufuata taratibu ama kuishirikisha kamati ya utendaji ya chama hicho katika kutoa maamuzi.
Akijibu malalamiko hayo, Ferej alisema katika soka, hakuna kitu kinachoitwa makubaliano, kinachotakiwa ni kufuatwa kwa katiba na kanuni katika kutoa maamuzi.
Ferej alisema ni kweli kwamba yeye ni mwanachama wa klabu ya Malindi, lakini hawezi kutoa maamuzi kwa lengo la kuibeba.
Rais huyo wa ZFA alisema tatizo kubwa linaloikabili soka ya Zanzibar ni ukiukwaji wa kanuni na kusisitiza kuwa, iwapo halitapatiwa ufumbuzi, litakwamisha maendeleo ya mchezo huo.
Alisema yapo baadhi ya mambo, ambayo klabu zinaweza kukubaliana kama vile mfumo wa mgawo wa mapato, lakini si uendeshaji wa ligi.
“Katika hili, ni kweli kwamba kanuni zimevunjwa na timu zilizoshuka daraja, zimeonewa,”alisema rais huyo wa ZFA, ambaye ameichezea Malindi kwa miaka 11 na pia kuiongoza kwa kipindi kama hicho.

Kambi ya Misri yaipa jeuri Zanzibar Heroes


TIMU ya soka ya Zanzibar, Zanzibar Heroes imerejea nchini juzi kutoka Misri, ilikokwenda kuweka kambi kwa ajili ya kujiandaa na michuano ya Kombe la Chalenji.
Ofisa Habari wa Chama cha Soka cha Zanzibar (ZFA), Munir Zakaria alisema mjini hapa juzi kuwa, timu hiyo iliweka kambi Misri kwa wiki mbili.
Mbali ya kuweka kambi, Munir alisema timu hiyo ilicheza mechi tatu za kirafiki dhidi ya timu za Misri, ambapo ilishinda mechi moja na kufungwa mechi tatu.
Munir alisema timu hiyo ilipata ushindi wake wa pekee dhidi ya timu ya taifa ya vijana wa chini ya miaka 17 ya Misri. Katika mechi hiyo, Zanzibar Heroes ilishinda mabao 3-2.
Zanzibar Heroes ilikwenda Misri ikiwa chini ya Kocha Hemed Morocco, ambaye ndiye atakayeiongoza katika michuano ya Kombe la Chalenji, inayotarajiwa kuanza kesho.
Akizungumzia kambi hiyo, Munir alisema ilikwenda vizuri na kwamba mechi nne za kirafiki walizocheza, zimewaweka wachezaji katika hali nzuri kwa ajili ya Kombe la Chalenji.
Alisema kikosi hicho kwa sasa kipo fiti kwa ajili ya michuano hiyo na kuongeza kuwa, wachezaji wana ari kubwa ya kuibuka na ushindi.
Wakati huo huo, Munir amesema hatma ya Kocha John Stewart kutoka Uingereza kwa sasa ipo mikononi mwa ZFA.
Stewart, ambaye pia ni Kocha Mkuu wa Azam FC, alishindwa kujiunga na Zanzibar Heroes ilipokuwa Misri kwa madai kuwa, hati yake ya kusafiria ilikuwa imejaa.
Hata hivyo, utetezi wake huo umepingwa na baadhi ya viongozi wa chama hicho kwa madai kuwa, alifahamu mapema kuhusu safari hiyo.
Licha ya kuifundisha Azam, inayoshiriki michuano ya ligi kuu ya Tanzania Bara, Stewart pia ana mkataba wa kuifundisha Zanzibar Heroes wakati wa michuano mbalimbali.

SMG afurahia kuitwa Kilimanjaro Stars

MSHAMBULIAJI Saidi Maulid ‘SMG’ anayecheza soka ya kulipwa nchini Angola, amesema amefurahia kuitwa kwenye kikosi cha Tanzania Bara, Kilimanjaro Stars kitakachoshiriki katika michuano ya mwaka huu ya Kombe la Chalenji.
SMG alisema hayo mjini Dar es Salaam juzi, alipokuwa akizungumzia kuitwa kwake kwenye kikosi hicho baada ya kuachwa kwa zaidi ya miaka mitano.
Alisema kwa mchezaji yeyote wa kulipwa anayecheza nje ya nchi yake, huwa ni fahari kubwa kwake kuitwa kwenye timu ya taifa kwa sababu kunaonyesha anavyothaminiwa.
Mshambuliaji huyo wa zamani wa klabu za Simba na Yanga alisema, amekuwa akiisubiri nafasi hiyo kwa muda mrefu na baada ya kuipata amepania kuonyesha uwezo wake.
Hata hivyo, SMG alisema kufanya vizuri kwa Kilimanjaro Stars katika michuano hiyo kutategemea ushirikiano wa wachezaji uwanjani na kutiwa moyo na mashabiki.
Alisema wao kama wachezaji, watajitahidi kucheza kadri ya uwezo wao, lakini wanahitaji sapoti kubwa kutoka kwa mashabiki.
SMG aliichezea Taifa Stars mwanzoni mwa miaka ya 2000 ilipokuwa chini ya makocha wazalendo na baadaye Marcio Maximo kutoka Brazil, lakini alitemwa baada ya kwenda Angola.
Awali, SMG hakuwemo kwenye kikosi hicho, lakini makocha Charles Boniface Mkwasa na Jamhuri Kihwelu walilazimika kumwita baada ya kuumia kwa John Bocco.
Mkataba wa mshambuliaji huyo kucheza Angola unatarajiwa kumalizika Desemba 2012.

Mwaikimba amwaga wino Azam FC


MSHAMBULIAJI Gaudence Mwaikimba wa Moro United amejiunga rasmi na Azam FC kwa ajili ya mzunguko wa pili wa michuano ya ligi kuu ya Tanzania Bara.
Ofisa Habari wa Azam, Jafari Iddi alisema mjini Dar es Salaam juzi kuwa, tayari mshambuliaji huyo ameshatia saini mkataba wa kuichezea timu hiyo.
Jafari alisema wameamua kumsajili Mwaikimba kwa lengo la kuziba pengo la mshambuliaji wao kutoka Ghana, ambaye ameachwa kutokana na kiwango chake kushuka.
Msemaji huyo wa Azam alisema, Mwaikimba anatarajiwa kuanza mazoezi na timu hiyo mara baada ya kumalizika kwa michuano ya Kombe la Chalenji.
Alisema wanaamini, Mwaikimba atashirikiana vyema na mshambuliaji John Bocco na Mrisho Ngassa kuunda safi kali ya ushambuliaji.
Kwa mujibu wa Jafari, lengo la timu yake ni kuhakikisha kuwa, wanamaliza msimu huu wa ligi wakiwa mabingwa ama kushika nafasi ya pili ili waweze kushiriki michuano ya kimataifa mwakani.
Kwa sasa, Mwaikimba yumo kwenye kikosi cha Tanzania Bara, Kilimanjaro Stars kitakachoshiriki michuano ya Kombe la Chalenji, inayotarajiwa kuanza kesho mjini Dar es Salaam.
Mwaikimba alianza kujipatia umaarufu alipokuwa akichezea Ashanti kabla ya kuchukuliwa na Yanga na baadaye kuhamia Kagera Sugar ya Bukoba.
Mchezaji huyo alikuwemo kwenye kikosi cha timu ya Taifa, Taifa Stars kilipokuwa chini ya Kocha Marcio Maximo kutoka Brazil kabla ya kutemwa kwa madai ya kiwango chake kushuka.

Tenga ni kusuka au kunyoa leo


UCHAGUZI mkuu wa Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) umepangwa kufanyika leo kwenye hoteli ya JB Belmont mjini Dar es Salaam.
Katika uchaguzi huo, mwenyekiti wa sasa wa CECAFA, Leodegar Tenga atakuwa akitetea nafasi hiyo dhidi ya Fadoul Hussein wa Djibouti.
Kwa sasa, Fadoul ni makamu mwenyekiti wa baraza hilo, lakini ameamua kuwania wadhifa wa juu kwa kumpinga bosi wake.
Uamuzi wa Fadoul kugombea nafasi hiyo, unamweka Tenga kwenye wakati mgumu kwa vile atalazimika kutegemea zaidi kura za nchi jirani ya Tanzania.
Kutokana na mazingira yalivyo, Fadoul atategemea zaidi kura kutoka Djibouti, Eritrea, Somalia na Sudan wakati kura za Tenga huenda zikatoka katika nchi za Tanzania Bara, Zanzibar, Kenya, Uganda, Rwanda na Burundi.
Hata hivyo, Tenga ndiye anayepewa nafasi kubwa ya kushinda wadhifa huo kutokana na kuungwa na nchi nyingi zilizo wanachama wa baraza hilo, akiwemo Katibu Mkuu, Nicholas Musonye.
Uchunguzi wa Burudani umebaini kuwa, nchi nyingi zinamuunga mkono Tenga kutokana na utendaji wake mzuri wa kazi, uwazi na pia ushirikiano na viongozi wenzake.
Tenga ndiye aliyeiwezesha CECAFA kupata udhamini wa michuano ya Kombe la Chalenji kutoka Kampuni ya Bia ya Serengeti (SBL) kwa miaka miwili mfululizo na kuhudhuriwa na mashabiki wengi zaidi kuliko nchi zingine.
Musonye alikaririwa hivi karibuni akisema kuwa, baraza lake linafurahia zaidi michuano hiyo kufanyika hapa nchini kutokana na kuwepo kwa udhamini mzuri na pia idadi kubwa ya mashabiki wanaofika uwanjani.
Mbali na uchaguzi wa mwenyekiti, pia watachaguliwa wajumbe wanne wa kamati ya utendaji. Wanaogombea nafasi hizo ni wajumbe wanane.
Wagombea hao ni Abdiqani Saeed Arab (Somalia), Tariq Atta Salih (Sudan), Justus Mugisha (Uganda), Tesfaye Gebreyesus (Eritrea), Hafidh Ali Tahir (Zanzibar), Sahilu Wolde (Ethiopia), Raoul Gisanura (Rwanda) na Abubakar Nkejimana (Burundi).