KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, January 23, 2014

YANGA UTAIPENDA, INAREJEA NCHINI KESHO





Na Baraka Kaziguto, Uturuki

KOCHA Mkuu mpya wa Yanga,  Hans Van Der Plyum, amesema amefurahishwa na nidhamu iliyoonyeshwa na wachezaji wa timu hiyo katika muda wote aliokaa nayo kambini Uturuki.

Hans amesema wachezaji wote waliosajiliwa na Yanga wana uwezo mzuri wa kucheza soka, wanajituma, wana nidhamu na upendo wa hali ya juu miongoni mwao.

Kocha huyo kutoka Uholanzi, alisema hayo jana baada ya mazoezi yaliyofanyika asubuhi kwenye hoteli ya Sueno iliyoko katika mji wa Antalya.

"Nina uzoefu na soka ya Afrika kwa takribani miaka 15. Wachezaji niliowakuta hapa
wana uwezo mzuri wote, wanajituma, wana nidhamu na upendo wa hali ya juu kitu ambacho kwa mwalimu yoyote lazima atafurahia mazingira hayo kwani hata ufanyaji wake kazi unakuwa mzuri, "alisema Hans.

Kocha huyo aliyerithi mikoba ya Mholanzi mwenzake, Ernie Brandts, alisema kwa muda wa siku tisa alizokaa na timu hiyo Uturuki, anaamini kikosi chake kipo tayari kutetea ubingwa wa ligi kuu na kufanya vizuri katika mashindano ya kimataifa.

Hans alisema kwa siku 14, ambazo Yanga imeweka kambi nchini humo, wachezaji na benchi la ufundi wameweza kutimiza wajibu wao vizuri kwa kufanya mazoezi kwa bidii na kucheza mechi za kirafiki za kujipima nguvu

Yanga imecheza mechi nne za kirafiki dhidi ya Ankara Sekerspor na Altay SK zinazoshiriki ligi daraja la pili Uturuki kabla ya kuivaa KS Flumartari ya Albania na
Simurq PIK ya Azerbajain. Ilishinda mechi mbili na kutoka sare mbili.
  
   KUREJEA NCHINI KESHO
Wakati huo huo, kikosi cha Yanga kilichokuwa kambini Uturuki, kinatarajiwa kuondoka hapa leo mchana kurejea nchini.

Yanga ilifanya mazoezi yake ya mwisho jana asubuhi na jioni, chini ya Kocha Hans kwa ajili ya kurekebisha mapungufu yaliyojitokeza katika mechi nne za kirafiki ilizocheza.

Kocha Hans alisema jana kuwa, hadi sasa hakuna mchezaji aliye majeruhi na kwamba wachezaji wote wapo fiti tayari kwa mechi yao ya kwanza ya mzunguko wa pili wa ligi kuu dhidi ya Ashanti.

Yanga na Ashanti zinatarajiwa kushuka dimbani keshokutwa katika mechi itakayopigwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Katika mechi ya mzunguko wa kwanza, Yanga iliibugiza Ashanti mabao 5-1.

   SEIF ATAMBA
Katika hatua nyingine, Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano ya Kimataifa wa Yanga, Seif  Ahmed 'Magari' amesema watahakikisha kikosi chao  hakifungwi katika mechi za mzunguko wa pili wa ligi kuu.

Akizungumza kwa njia ya simu kutoka Zanzibar jana, Seif alisema kamati yake itatoa ushirikiano wa hali ya juu kwa wachezaji na benchi la ufundi ili kuwaongezea ari ya kufanya vizuri na kutetea ubingwa wa ligi.

Seif alisema mara baada ya timu hiyo kutua nchini kesho alfajiri ikitokea Uturuki, itakwenda kambini moja kwa moja kwa ajili ya maandalizi ya mechi yao ya ligi dhidi ya Ashanti.

Yanga na Ashanti zinatarajiwa kushuka dimbani keshokutwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Katika mechi ya mzunguko wa kwanza, Yanga iliibugiza Ashanti mabao 5-1.

"Tumepanga kukutana na wachezaji na kocha baada ya timu kurejea nchini Ijumaa kutoka Uturuki ili kupanga mikakati. Safari hii nawahakikishia wanachama na wapenzi wa Yanga kwamba hatutafungwa mechi yoyote,"alitamba.

Seif alisema pia kuwa, wameshaanza kufanya upelelezi dhidi ya timu ya Komorozine Sports ya Comoro, watakayopambana nayo katika michuano ya klabu bingwa Afrika mwezi ujao.

No comments:

Post a Comment