KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, January 16, 2014

RAGE AOKOA JAHAZI SIMBA



KLABU ya Simba imelazimika kukopa fedha kwa wadau wake mbalimbali kwa ajili ya kuwalipa mishahara wachezaji wake.
Mwenyekiti wa Simba, Ismail Aden Rage alisema mjini Dar es Salaam jana kuwa, wamefikia uamuzi huo kutokana na klabu kutokuwa na pesa.
Rage alisema uamuzi wake huo umelenga kutimiza ahadi aliyoitoa kwa wachezaji muda mfupi kabla ya timu hiyo kumenyana na KCC ya Uganda katika mechi ya fainali ya Kombe la Mapinduzi.
Katika mechi hiyo, iliyochezwa Jumatatu iliyopita kwenye Uwanja wa Amaan, Zanzibar, Simba ilipigwa mweleka wa bao 1-0.
Wachezaji wa Simba wanadai mishahara ya mwezi uliopita na hadi juzi walikuwa hawajalipwa.
"Nimetafuta pesa kutoka kwa marafiki zangu leo na nimefanikiwa kuzipata na nimeshaziingiza benki kupitia akaunti za wachezaji ili waweze kuzipata haraka,"alisema Rage.
Mwenyekiti huyo wa Simba alisema, wadhamini wao, Kampuni ya Bia Tanzania (TBL), walishalipa fedha za mishahara kwa ajili ya wachezaji, lakini viongozi wenzake walizitumia kwa shughuli zingine.
"Nilipokuwa nje ya nchi, nimekuta wenzangu wamechukua pesa kutoka TBL, zimetumika kwa shughuli nyingine wakati mimi sipo, ndio sababu nimeamua kuokoa jahazi kwa ajili ya kulinda maslahi ya Simba,"alisema.
Rage alisema kuanzia sasa atakuwa makini kuhakikisha kuwa, fedha za wachezaji haziguswi na wanalipwa mishahara yao na posho wanazostahili kwa wakati unaotakiwa.
Uamuzi wa Rage kukopa fedha na kuwalipa wachezaji, umekuja siku chache baada ya kutunishiana misuli na mwenyekiti wa kamati ya usajili ya Simba, Zacharia Hanspope walipotembelea kambi ya timu hiyo ilipokuwa Zanzibar.
Wakati akizungumza na wachezaji, Rage aliwaahidi kuwalipa madai yao, lakini muda mfupi baadaye, Hanspope alikutana nao na kuwapa dola 10,000 za Marekani, zikiwa ni sehemu ya mishahara yao.
Wakati huo huo, Kocha Mkuu wa Simba Zdravko Logarusic, anatarajia kupanga kikosi cha kwanza cha timu yake katika mchezo wa kirafiki utakaoikutanisha timu yake na Mtibwa Sugar.
Simba na Mtibwa Sugar zitashuka dimbani keshokutwa katika mchezo wa kirafiki utakaofanyika katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

No comments:

Post a Comment