'
Thursday, January 23, 2014
VIONGOZI WAMALIZA TOFAUTI ZAO, RAGE AIONYA YANGA KUHUSU KAPOMBE
NA AMINA ATHUMANI
KAMATI ya utendaji ya Simba pamoja na Mwenyekiti wa klabu hiyo Ismail Rage wamemaliza tofauti zao .
Rage na Kamati ya Utendaji ya Simba walikuwa na mgogoro uliosababisha kutoweka kwa amani ndani ya klabu hiyo kongwe nchini.
Katika kikao cha makubaliano hayo kilichofanyika juzi usiku wamekubaliana kushirikiana na kuacha yale yote yaliyojitokeza katika kipindi cha nyuma na kusababisha kuwepo kwa mgogoro ndani ya klabu hiyo.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Rage alisema anashukuru kumaliza tofauti zao na Kamati ya Utendaji ya klabu hiyo na sasa amani imetawala.
"Kikao cha jana (juzi) tumekubaliana tuwe kitu kimoja na kufanya kazi kwa ushirikiano na hakuna tena mgogoro ndani ya klabu yetu,"alisema Rage.
Rage alitoa wito kwa wanachama wa klabu hiyo wasijaribu tena kuigawa klabu hiyo kwa kuwa inaathiri mfumo mzima wa maendeleo ya soka katika klabu hiyo.
Mgogoro wa Simba na Rage ulizuka baada ya Kamati ya Utendaji ya klabu hiyo kufanya mapinduzi ya kumsimamisha Mwenyekiti huyo kwa madai kuwa amekuwa akijiamulia mambo kinyume na matakwa ya kamati hiyo.
Hata hivyo, mapinduzi hayo yalipingwa na Shirikisho la Soka Tanzania TFF, ambalo lilisema Rage ndiye Mwenyekiti halali wa klabu hiyo.
Wakati huo huo, Rage alizionya klabu za soka nchini zinazomtumbulia macho beki wao, Shomari Kapombe kwa vile ni mali ya Simba kwani mkataba wake unamalizika 2016.
Alisema pia kuwa, suala la Kapombe na klabu ya Cannes ya Ufaransa, aliyokuwa akiichezea,
limemalizika na sasa mchezaji huyo atarejea nchini kuendelea na kabumbu.
Alisema Kapombe alikuwa akiidai klabu hiyo mshahara wake wa Novemba ambapo tayari amezungumza na mkurugenzi wa timu hiyo na ameahidi kuilipa fedha hiyo ndani ya wiki hii.
Alisema kwa mujibu wa Mkurugenzi huyo, wanamuhitaji Kapombe kwani ni mchezaji aliyeonekana na uwezo mkubwa wa kisoka.
Pia Rage alisema Kapombe alikaa nje ya uwanja siku 72 kutokana na kuwa majeruhi katika kidole gumba cha mguu hivyo hali hiyo pia ilichangia kucheleweshwa kwa mshahara huo.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment