'
Thursday, January 30, 2014
MOYES KUTEMBEZA CHEKECHE MAN UTD
LONDON, England
KOCHA Mkuu wa Manchester United, David Moyes amewaonya wachezaji wake nyota wanaocheza chini ya kiwango kwa kuwaambia, atawapiga chekeche iwapo watashindwa kujirekebisha.
Moyes amesema amepanga kusajili nyota wapya kadhaa kutoka klabu mbalimbali za Ulaya kwa ajili ya kuziba nafasi za wale atakaowatema.
Kocha huyo aliyerithi mikoba ya Sir Alex Fergsuon amesema, lengo lake ni kuwa na kikosi cha wachezaji wanaojituma na kutimiza wajibu wao ipasavyo uwanjani.
Tayari Moyes ameshamsajili nyota wa zamani wa Chelsea, Juan Mata kwa kitita cha pauni milioni 37 na alitarajiwa kuanza kuichezea Manchester United mwanzoni mwa wiki hii katika mechi dhidi ya Cardiff.
Kocha huyo amesema ujio wa Mata ni salamu kwa wachezaji watakaoshindwa kujirekebisha kwa vile anatarajia kusajili nyota wengine wapya hivi karibuni.
Uamuzi wa Moyes kuwapiga chekecheke wachezaji wazembe, umetokana na mwenendo usioridhisha wa Manchester United katika michuano ya ligi kuu ya England.
Kuvurunda kwa timu hiyo katika ligi na michuano mingine, kumemfanya Moyes aseme sasa basi na kuanza kuchukua hatua.
"Siwezi kuruhusu hali hii iendelee,"alisema kocha huyo, ambaye kama Ferguson, ni raia wa Scotland.
"Nimekatishwa tamaa kuona hatuko kwenye nafasi nzuri. Nimekatishwa tamaa na uchezaji wetu,"alisema kocha huyo.
"Ninapaswa kuchukua hatua. Nitasajili wachezaji wazuri zaidi. Sidhani kama nitasajili zaidi Januari, lakini timu itabadilika,"alisisitiza.
Kuondoka kwa Anderson, aliyesajiliwa kwa mkopo na Fiorentina ya Italia na pia kuondolewa kwa Wilfried Zaha na Fabio kwenye kikosi cha kwanza, kunathibitisha lengo la Moyes kukisuka upya kikosi cha timu hiyo.
Beki mkongwe Rio Ferdinand naye anatarajiwa kufungasha viraga msimu ujao wakati hatma ya mabeki wengine, Nemanja Vidic na Patrice Evra ipo shakani.
Wachezaji wengine, ambao huenda wakafungashiwa virago ni pamoja na Alexander Buttner, Nani, Ashley Young na Javier Hernandez 'Chicharito'.
Moyes ameamua kufanya marekebisho makubwa kwenye kikosi chake kwa lengo la kurejesha imani kwa mashabiki wa klabu hiyo maarufu duniani, ambao kwa sasa wamekata tamaa.
"Nimetoa nafasi kwa kila mchezaji kucheza na kuonyesha uwezo wake. Tulipata nafasi ya kuona uwezo wa kila mmoja. Kinachofuata sasa ni kuchukua hatua,"alisema kocha huyo.
"Wachezaji wanapaswa kuonyesha uwezo wao. Kama wanataka kubaki hapa na kupata namba, wanapaswa kuthibitisha hilo katika mechi wanazocheza,"alisisitiza.
Moyes alisema Manchester United ni klabu kubwa na inapaswa kuwepo kwenye nafasi za juu kwenye msimamo wa ligi na kuonyesha ushindani.
"Kwa wakati huu, tumeshindwa kufanya hivyo. Tunapaswa kulishughulikia tatizo hili,"aliongeza.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment