'
Sunday, January 5, 2014
AZAM YATINGA ROBO FAINALI KOMBE LA MAPINDUZI
Visiwa vya zanziba jana vilishuhusia soka lililoundwa toka kwa vilabu vilivyoundwa, Tusker FC toka Kenya walicheza soka lililopikwa na kuiva huku Azam FC wakijibu mapigo kwa soka lililoundwa pia
Ulikuwa mtanange uliowaacha na furaha mashabiki walioushuhudia uwanjani na majumbani kupitia ZBC na Azam TV kwani baadhi yao baada ya mechi walisema viingilio vyao vilitendewa haki.
Goli pekee la mchezo huo liliwekwa kimiani kwa ufundi wa hali ya juu na mshambulaji Kipre Tchetche raia wa Ivory Coast dakika moja kabla ya mapumziko pale alipopokea pasi murua ya kiungo Himid Mao akiwa pembeni kushoto mwa eneo la hatari kisha akawapiga chenga walinzi watatu waliokuwa wamemzunguka na kabla ya kuwapita akiwa katikati yao aliuachia mkwaju mkali kwa guu la kushoto uliotinga kimiani upande wa juu kulia mwa lango la Tusker na kumwacha mlinda lango Samuel Odhiambo akiwa ameduwaa licha ya kuchupa kwa juhudi kubwa.
Kwa ujumla Azam FC walionekana tofauti kabisa katika mchezo wa jana ikilinganishwa na mchezo walioonesha pale walipocheza na Spice Stars na kushinda 2-0 kwani walikuwa na kasi pale waliposhambulia na kila mchezaji alionekana kujituma huku wakikaba wote pale walipopokonywa mipira hivyo kuwalazimisha Tusker kuwa na papala katika kutoa pasi.
Matokeo yake Tusker wanaofundishwa na kocha wa zamani wa Harambee Stars, Francis Kimanzi walijikuta wakichezewa nusu uwanja kwa muda mrefu kipindi cha kwanza na walijitahidi kurejea mchezoni kipindi cha pili wakitumia mipira mirefu na mipira ya kurusha ya Luke Ochieng lakini juhudi zao ziliishia patupu.
Nahodha wa Tusker Emannuel Ochieng ambaye ni mlinda lango aliimbia AzamTv baada ya kipenga cha mwisho kupulizwa kuwa alisikitika sana kuona walinzi wake watatu wakishindwa kumkaba mfungaji (Kipre) na hatimaye timu yake kupoteza mchezo, japo alikiri kuwa goli lilifungwa kwa ufundi kwani pamoja na yeye kuwa katika sehemu sahihi hakuweza kuzuia mpira kwani mfungaji alichangua sehemu nzuri kwake kufunga.
Naye mshmbuliaji kinda wa Azam, Joseph Kimwaga ameiambia AzamTV kuwa leo timu ilicheza tofauti kwani mkufunzi mpya, Joseph Omog raia wa Cameroon aliwaambia kuwa ni lazima kila mchezaji ajitume kwa ajili ya manufaa ya Timu hata kama akipewa dakika tano kutumika uwanjani kwani hiyo ndiyo kazi yao wanayoitegemea kuishi.
Azam watashuka tena dimbani keshokutwa Jumatatu kuwakabili Ashanti wenye pointi moja wakati Tusker wenye pointi tatu watawakabili wenyeji Spice Stars.
Kabla ya hapo kesho Jumapili kwenye Uwanja wa Amaan, kundi B litakamilisha michezo yake kwa Simba kukabiliana na wenyeji KMKM katika mchezo wa saa 2 kamili usiku ukitanguliwa na mchezo kati ya wageni KCC ya Uganda na AFC Leopards ya Kenya.
Kwa upande wa kituo cha Pemba, Jumapili ni mapunziko na michezo ya mwisho itachezwa Jumatatu kati Mbeya City na URA na mwingine ni kati ya wenyeji Chuoni na Clove Stars
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment