'
Thursday, January 16, 2014
KAJALA: JAMANI, SIJAKAMATWA NA DAWA ZA KULEVYA
MSANII nyota wa filamu nchini, Kajala Masanja amesema si kweli kwamba alikamatwa na polisi wa China hivi karibuni kwa tuhuma za kuingiza dawa za kulevya nchini humo.
Kajala amesema taarifa hizo zilizoripotiwa na baadhi ya vyombo vya habari nchini hivi karibuni, hazikuwa za kweli na kwamba zililenga kuchafua jina lake.
Akizungumza na mtandao wa Millardayo juzi, Kajala alisema ni kweli alikwenda China mwishoni mwa mwaka jana, lakini safari yake hiyo ililenga kufanya 'manunuzi'.
"Si kweli kwamba nilikamatwa uwanja wa ndege. Hata dawa zenyewe za kulevya sizijui zilivyo zaidi ya kuziona kwenye TV,"amesema.
Mcheza filamu huyo, ambaye mwaka jana alinusurika kufungwa jela baada ya kulipiwa faini ya sh. milioni 14 na msanii mwenzake Wema Sepetu, alisema inasikitisha kuona kuwa, kila msanii nyota anaporejea nchini kutoka nje, anakaguliwa kwa muda mrefu kutokana na kuhusishwa na biashara ya dawa za kulevya.
"Hivi sasa, kila staa akipita kwenye uwanja wa ndege Dar ni lazima asachiwe sana kwa sababu wanasema ‘nyinyi mastaa mnatuharibia sana kazi’ kwa hiyo lazima wakuweke pembeni kukukagua," amesema mwanadada huyo mwenye sura jamali na umbo la kuvutia.
Kajala amesema kilichompeleka China ni kununua vitu vyake binafsi kwa ajili ya filamu yake mpya, anayotarajia kuitoa mwishoni mwa mwezi huu.
"Nilikwenda huko kununua vitu vya kuvaa, sio kamera wala vifaa, ni nguo tu, shopping inazidi milioni kumi," amesema msanii huyo.
Kajala pia amekanusha madai kuwa, alikwenda China akiwa na mume wa mtu na kupiga naye picha, ambazo zilisambazwa kwenye mitandao mbalimbali ya kijamii.
"Mtu wa kwanza kuandika habari hizi alikuwa mmiliki wa blogu ndipo magazeti na mitandao mingine ikafuata, lakini haikuwa kweli. Sikutaka kuzifuatilia habari hizo kwa sababu ukweli ninaujua mwenyewe. Lakini niliumia sana, hata mama yangu aliumia na aliniuliza,"amesema Kajala.
Amesema kwenda klabu au kukutana na mtu na kupiga naye picha haina maana kwamba ameiba mume wa mtu.
"Huyo dada kama kweli angekuwa mume wake, angenifuata maana hata kuniona hajawahi, yeye yuko Hong Kong mimi niko China, ananiambia nimeiba mume wake. Huyo mwanaume anaishi huko huko,"amesema.
Kajala amesisitiza kuwa, alikwenda China kwa gharama zake binafsi na si kweli kwamba alikwenda huko na mwanaume waliyepiga picha pamoja, wakitokea Tanzania.
Amesema siku aliyopigwa picha na huyo mwanaume, ilikuwa kwenye sherehe ya kuzaliwa ya mmiliki wa klabu moja ya burudani na kwamba hakuwa akifahamu iwapo kuna mtu alikuwa akimpiga picha.
Kajala amesema kwa sasa hana mpango wa kufunga ndoa nyingine kwa sababu ndoa yake ya awali aliifunga kanisani.
"Sijui kama nitaruhusiwa kuolewa tena, kwa hiyo namsubiria labda mume wangu akitoka jela, lakini kwa sasa sina mpango wowote wa kuolewa japo napata usumbufu," alisema na kuongeza:
"Ila nawaambia tu kwamba, mume wangu yuko jela, huwa namtembelea kila wikiendi. Kukaa kwake jela kumeniathiri sana, tulikaa kwenye ndoa miezi sita tu kabla ya misukosuko kuanza, nilikuwa na mpango wa kupata mtoto mwingine wa pili ili niwe nimemaliza ila sasa hivi siwezi kuzaa, nimekaa tu namsubiria."
Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam, ilimuhukumu Kajala na mumewe, Faraja Chambo kwenda jela miaka minane au kulipa faini ya sh. milioni 13 baada ya kutiwa hatiani katika makosa ya kula njama, kuhamisha umiliki wa nyumba, na kuhamisha umiliki wa nyumba iliyokuwa imezuiwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali isiuzwe.
Hata hivyo, Kajala alinusurika kwenda jela baada ya kulipiwa faini hiyo na Wema. Mumewe anatumikia kifungo alichohukumiwa.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment