KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, January 16, 2014

MZUNGU AANZA KUINOA YANGA UTURUKI



UONGOZI wa klabu ya Yanga, umeamua kumrejesha nchini Kocha Msaidizi wa timu hiyo, Charles Boniface Mkwasa baada ya kukabidhi timu kwa kocha mpya, Johannes Franciscus ‘Hans’ van der Pluijm.
Mkwasa, alimkabidhi rasmi timu kocha huyo kutoka Uholanzi juzi baada ya kutua Uturuki, akitokea Dar es Salaam.
Yanga imeweka kambi Uturuki kwa ajili ya kujiandaa na mzunguko wa pili wa ligi kuu ya Tanzania Bara na michuano ya klabu bingwa Afrika.
Pluijm ameingia mkataba wa kuifundisha Yanga kwa miezi sita na jukumu lake kubwa ni kuinoa timu hiyo kwa ajili ya mzunguko wa pili wa ligi kuu ya Tanzania Bara na michuano ya kimataifa.
Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Clement Sanga aliwaambia waandishi wa habari mjini Dar es Salaam jana kuwa, wamelazimika kumrejesha Mkwasa kutokana na kupatwa na matatizo ya kifamilia.
Kwa mujibu wa Sanga, Mkwasa anatarajiwa kurudi nchini keshokutwa na kwamba, kuanzia sasa, jukumu la kuinoa timu hiyo litakuwa chini ya Pluijm.
Sanga alisema tayari Mkwasa ameshamweleza kocha huyo mpya, hatua aliyofikia katika kuwapa mafunzo wachezaji wa timu hiyo, ili aweze kuendelea pale alipoishia.
Makamu Mwenyekiti huyo wa Yanga alisema, Mkwasa atarejea Uturuki baada ya kumaliza matatizo yake ya kifamilia.
Yanga ilitarajiwa kushuka dimbani jana kucheza mechi ya pili ya kirafiki dhidi ya Atlay SK ya Uturuki kabla ya kushuka tena dimbani mwishoni mwa wiki hii kukipiga na Simurg Zaqatala ya Azberbaijan.
Wakati huo huo, Sanga amesema, mbali na kuwa kocha mkuu wa Yanga, Pluijm ameteuliwa kuwa mkurugenzi wa ufundi wa klabu hiyo.
Amesema kutokana na uteuzi huo, kocha huyo atasimamia mambo yote yanayohusu ufundi katika klabu hiyo, ikiwa ni pamoja na kuandaa programu mbalimbali za kuinua soka.
Sanga amesema pia kuwa, uongozi wa Yanga utaendelea kuwachukulia hatua kali wachezaji watakaobainika kujihusisha na vitendo vya utovu wa nidhamu, ikiwa ni pamoja na kucheza mechi za mchangani.
Tayari wachezaji saba wameshapewa adhabu ya kukatwa mishahara yao kutokana na makosa mbalimbali. Wachezaji hao ni Haruna Niyonzima,Mrisho Ngasa, Athuman Idd 'Chuji', Nadir Haroub 'Cannavaro', Salum Telela, David Luhende na Simon Msuva.

No comments:

Post a Comment