'
Thursday, January 30, 2014
CHUJI YAMETIMIA YANGA
UONGOZI wa klabu ya Yanga, umeamua kumsamehe kiungo mkongwe wa timu hiyo, Athumani Iddi 'Chuji', aliyekuwa amesimamishwa kwa muda usiojulikana.
Uamuzi wa kumsamehe mchezaji huyo, ulifikiwa katika kikao cha kamati ya utendaji ya Yanga, kilichofanyika juzi mjini Dar es Salaam.
Katika kikao hicho, wajumbe wa kamati hiyo walivutana kwa muda mrefu, baadhi yao wakitaka mchezaji huyo asamehewe na wengine wakitaka aendelee na adhabu ya kusimamishwa.
Wajumbe waliotaka asamehewe, walisema Chuji ameonyesha uungwana kwa kuomba radhi na kuahidi kutorudia makosa, hivyo anastahili kupata msamaha kwa vile adhabu aliyotumikia inatosha.
Lakini baadhi ya wajumbe walipinga kwa madai kuwa, mchezaji huyo ameendelea kuonyesha utovu wa nidhamu kwa kunukuliwa na vyombo vya habari akisema kuwa, Yanga haijamsaidia lolote kimaisha.
Baada ya mvutano huo, wajumbe walikubaliana kwa pamoja kumsamehe mchezaji huyo, kwa masharti kwamba apewe onyo kali.
Chuji alikabidhiwa barua hiyo jana na anatarajiwa kujiunga na wachezaji wenzake baada ya timu kurejea kutoka Tanga.
Kiungo huyo wa zamani wa Simba na Polisi Dodoma, alisimamishwa mwishoni mwa mwaka jana baada ya kuondoka uwanjani baada ya kupumzishwa wakati Yanga ilipomenyana na Simba katika mechi ya Nani Mtani Jembe.
Katika mechi hiyo iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, Simba iliichapa Yanga mabao 3-1. Chuji ni miongoni mwa wachezaji waliodaiwa kucheza chini ya kiwango.
Yanga ilitarajiwa kushuka dimbani jana kumenyana na Coastal Union kwenye Uwanja wa Mkwakwani, Tanga kabla ya kushuka tena dimbani Jumapili kukipiga na Mbeya City kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Mbali na kushiriki katika ligi, Yanga inajiandaa kwa michuano ya klabu bingwa Afrika, ambapo imepangwa kuanza raundi ya kwanza kwa kumenyana na Komoronize ya Comoro mwanzoni mwa mwezi ujao.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment